Na Mwandishi Wetu, APC BLOG
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Tanzania imeibuka mshindi wa kwanza katika Taasisi za Elimu kanda ya kaskazini.
Akizungumzia ushindi huu Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof Emmanuel J. Luoga, amesema kuwa, Ushindi huo ni motisha na hatua muhimu kwa taasisi hasa katika kufanya tafiti na ugunduzi ili kutatua changamoto za Viwanda na Jamii.
Prof. Luoga amesema tafiti zilizokuwa sehemu ya maonesho ya Taasisi ni pamoja na, matokeo ya utafiti juu ya namna ya kuboresha uzalishaji wa migomba inayostahimili ugonjwa wa mnyauko, ndizi kwa kuchanganya samadi pamoja na mbolea za viwandani.
Pia matokeo ya utafiti juu ya njia ya kibaiolojia ya kudhibiti magugu vamizi katika malisho ya wanyama na mashambani ambapo utafiti huo unafanyikia katika hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha.
Anasema utafiti mwingine ni pamoja na utafit juu ya Madawa asilia yanayoweza kutumika katika kuchakata ngozi, kuiongezea thamani kwa matumizi mbalimbali kama kutengenezea viatu, mikoba ya akina dada na bidhaa nyinginezo.
“Utafiti juu ya teknolojia ya kuondoa Magadi/Chumvi kwenye maji kwa matumizi salama nyumbani na viwandani, utafiti juu ya mfumo wa Tehama wa kujifunzia kwa watoto wadogo
pamoja na hayo Taasisi ilikuwa ikiendesha mafunzo mbalimbali kwa wakulima, Wafugaji na wadau mbalimbali,’ anasema.
Anasema wakulima na wafugaji waliotembelea mabanda yao walipata fursa ya kufundishwa njia bora za kuongeza thamani ya zao la ngozi katika mfumo mzima wa kuongeza thamani
tangu ikiwa kwenye mnyama hadi inapotolewa, Matumizi mbalimbali ya Aloe hapa Tanzania ikiwemo faida na hasara za aina mbalkimbali za Aloe.
“ Pia walifundishwa njia bora za kuzuia magonjwa ya mlipuko baina ya binaadamu na wanyama pamoja na mazingira kwa Afya moja (One Health), uhifadhi wa bayoanuai kwa afya yetu na uchumi wa nchi, mambo ya kuzingatia wakati wa uandaaji wa uji lishe kwa mtoto mwenye umri wa miezi 6 hadi 24,”anasema.