Manchester United wametupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora baada ya kuonyesha kiwango kibovu mbele ya Sevilla na kukubali kichapo cha 2-1 Old Trafford.
Wissam Ben Yedder aliyetokea benchi kwa upande wa Sevilla ndiye aliyepeleka kilio kwa Man u baada ya kufunga magoli yote mawili dakika mbili tu baada ya kuingia uwanjani.
Kipindi cha kwanza Man U ilikosa kuongoza baada ya mikwaju ya Marouane Fellaini na Jesse Lingard kuchezwa vyema na mlinda mlango wa Sevilla Sergio Rico aliyeonyesha kiwango bora kwenye mchezo huo.
Romelu Lukaku alifunga kwa upande wa United zikiwa zimesalia dakika saba lakini goli lake halikusaidia kitu.
United inaungana na Tottenham kuyaaga mashindano hayo lakini kinara wa EPL Manchester City na Liverpool tiyari wamefuzu hatua ya robo fainali na sasa wanasubiria kupangwa kwa droo siku ya Ijumaa.
Chelsea wanaweza kuungana nao iwapo wataiondosha Barcelona siku ya Jumatano.