Dkt pima na wenzake wafutiwa mashtaka na kusomewa upya

 Na Seif Mangwangi, Arusha

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imewaachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Jijini la Arusha Dkt Pima na wenzake baada ya Mkurugenzi  wa mashtaka wa Serikali (DPP), kueleza mahakama hiyo kuwa  hana nia ya kuendelea na kesi hizo.

Hata hivyo baada ya kuwaachia huru, washtakiwa wote walisomewa tena mashtaka mapya ya uhujumu uchumi baada ya Mkurugenzi wa mashtaka kuieleza mahakama ya Hakimu Mkazi kuwa baada ya kuondoa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili Sheria inamruhusu kufungua tena shauri jipya dhidi ya makosa yale yale.

” Mheshimiwa Hakimu, kwa mujibu wa kifungu Cha 91  kifungu cha 1,  sura ya 20 marejeo ya Mwaka 2022,  kinamruhusu DPP kushtaki upya akiona kama inafaa, hivyo tayari DPP amesajili shauri jipya dhidi ya watuhumiwa wanne na litalitajwa pale litakapoitwa mbele ya mahakama yako,”amesema Mwendesha mashtaka wa Serikali Kyaka.

Alisema kuwa tayari mkurugenzi wa mashtaka ametoa idhini pamoja na cheti kuruhusu kesi hiyo isikilizwe upya katika mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi.

Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha Fadhili Mbelwa, aliieleza mahakama kuwa tayari mahakama yake imeshapokea cheti Cha kuruhusiwa kusikiliza kesi hizo na kutoa ruhusa kwa waendesha mashtaka wa Serikali kuendelea kuwasomea watuhumiwa hao mashtaka mapya kama walivyosajili katika Mahakama hiyo.

Hakimu Mbelwa aliuhoji upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na Wakili Sabato Ngogo kuhusiana na maelezo ya upande wa DPP, kuendelea kuwasomea wateja wao mashtaka mapya ambapo Wakili Ngogo aliieleza mahakama kuwa wako tayari kusikiliza mashtaka mapya na kuiomba mahakama waweze kupatiwa hati hiyo ya mashtaka.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Habel Kyaka aliieleza mahakama kuwa ofisi hiyo imefunguka kesi mpya ya uhujumu uchumi ambayo itajulikana kama kesi namba3 ya uhujumu uchumi ya Mwaka 2024. 

Akiwasomea maelezo ya awali Kyaka ameieleza mahakama kuwa katika shtaka la kwanza lenye mashtaka nane ndani yake washtakiwa ni, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt John Pima (45), Mariam Mshana ( 43), aliyekuwa  mkuu idara ya fedha na biashara, Innocent Maduhu(40), aliyekuwa Mkuu wa idara ya  fedha na mipango na Nuru Saqware Ginana (40), aliyekuwa mchumi.

Kyaka aliieleza mahakama kuwa katika kesi hiyo namba3 ya uhujumu uchumi, watuhumiwa wote wanne wanatuhumiwa kwa udanganyifu na kufanya ufujaji na ubadhirifu wa fedha ya umma kiasi Cha Tsh milioni65  katika kosa walilolifanya kati ya Aprili14,2022 na Aprili16,2022.

Shtaka la pili walilosomewa ni watuhumiwa wote wanne wanatuhumiwa kutumia nyaraka kudanganya mwajiri, katika kosa waliofanya  kati ya 14.04.2022 na 16.04.2022 ndani ya Jiji , kupitia dokezo sabili kuhusu majukumu ya mwajiri ambalo lilikuwa na masikisio sio sahihi, likieleza kwamba mchumi Ginana, aliomba fedha mil65 kununua Moram kwaajili ya kuisambaza kwenye  masoko ya  soko kuu, samunge, mbauda, morombo na  kilombero jambo ambalo sio kweli.

Shtaka la tatu walilosomewa Dkt Pima na wenzake  ni kutumia nyaraka kudanganya mwajiri, huku shtaka la nne katika kesi hiyo, ni kutumia nyaraka kudanganya katika kosa waliofanya  26.04.2022 kuhusu  marejesho ya masurufu safari and special imprest ambayo ilikuwa na maelezo ya uongo. 

Shtaka la tano kutumia nyaraka kudanganya mwajiri, katika kosa wanalodaiwa kulifanya kati ya 14.04.2022 na 28.04.2022 ambapo nyaraka hiyo ilichanganua kiwango Cha fedha zilizotumika kununulia Moram na kwamba  walitumia nyaraka iliyobeba maelezo ya uongo.

Kwa mujibu wa Mwendesha mashtaka Kyaka, shtaka la sita linalowakabili Dkt Pima na wenzake ni kutumia nyaraka ya uongo ambayo ni fomu ya upokeaji na usambazaji wa moram iliyonunuliwa jambo ambalo sio kweli ambapo kosa hilo wanaidaiwa kulifanya kati ya 14.04.2022 na 28.04. 2022.

Kosa la Saba walilosomewa ni matumizi mabaya ya nafasi kosa ambalo wanadaiwa kulifanya kati ya 14.04.2022 na 28 .04.2022w wakidaiwa kuitumia vibaya nafasi zao kuandaa na kuthibitisha malipo ya mil65 kinyume na kifungu 115 ya manunuzi ya umma, kwa lengo la kujipatia manufaa binafsi na shtaka la nane dhidi yao ni kusababishia hasara Mamlaka, ya shilingi mil65

Hakimu wa Mahakama hiyo Fadhil Mbelwa aliwahoji watuhumiwa wa kila kosa walilosomewa na wote walikana kutenda mashtaka hayo.

Wakili anayewatetea Dkt Pima na wenzake watatu, Sabato Ngogo aliomba mahakama hiyo kuwapatia dhamana wateja wake kwa kuwa kosa wanaloshtakiwa nalo lina dhamana.

Hakimu Mbelwa alisema mahakama yake Haina pingamizi na dhamana endaolpo watuhumiwa watakidhi vigezo.

Baada ya maelezo hayo ya Hakimu, Wakili Ngogo aliomba Mahakama kutumia vielelezo vya dhamana vilivyotumika hapo awali kwa kuwa kesi ya mwanzo ilishafutwa na Hakimu aliruhusu kwa kutoa muda wa mapumziko kuruhusu wadhamini kufuatia nyaraka hizo katika masjala ya Mahakama

Hata hivyo mtuhumiwa wa nne katika kesi hiyo Nuru Saqware Ginana aliyekuwa akijiwakilisha mwenyewe mahakamani hapo alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kuamriwa apelekwe mahabusu Hadi atakapokamilisha masharti ya dhamana yake.

SHTAKA LA PILI

Kama ilivyokuwa katika kesi namba3, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Habel Kyaka aliieleza mahakama kuwa Mkurugenzi wa mashtaka ameamua kutoendelea na shauri namba 4 ya Mwaka 2022  ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili watuhumiwa wanne ambao ni Dkt John Pima (45), aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Mariam Mshana ( 43), aliyekuwa  mkuu idara ya fedha na biashara, Innocent Maduhu(40), aliyekuwa Mkuu wa idara ya  fedha na mipango na Alex Daniel Tilhema (40), aliyekuwa mchumi wa Jiji.

Aidha aliieleza mahakama kuwa Mkurugenzi amefungua kesi mpya ya uhujumu uchumi ya Mwaka 2024, na kuwasomea upya mashtaka watuhumiwa wanne ambao ni Dkt John Pima (45), aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Mariam Mshana ( 43), aliyekuwa  mkuu idara ya fedha na biashara, Innocent Maduhu(40), aliyekuwa Mkuu wa idara ya  fedha na mipango na Alex Daniel Tilhema (40), aliyekuwa mchumi wa Jiji.

Akiwasomea mashtaka mapya, Mwendesha mashtaka wa Serikali Henry chaula aliieleza mahakama ya Hakimu Mkazi kuwa watumiwa wanne Dkt John Pima (45), aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Mariam Mshana (43), aliyekuwa  mkuu idara ya fedha na biashara, Innocent Maduhu(40), aliyekuwa Mkuu wa idara ya  fedha na mipango na Alex Daniel Tilhem wanakabiliwa na mashtaka nane ya uhujumu uchumi.

Shtaka la kwanza  ni ubadhirifu ambao wanadaiwa kuufanya kati ya 14.4.2022 na 16.04.2022 wakiwa watumishi, walibadilisha matumizi ya mil65 kwa matumizi binafsi.

Shtaka la pili ni kutumia nyaraka kudanganya mwajiri. kati ya 14.4.2022 na 16.4.2022 kuandaa dokezo sabili likihusisha shughuli za mwajiri na kuonyesha Alex ameomba apewe mil65  kwaajili ya kununulia kifusi arekebishe barabara zilizoko Jiji la Arusha kumbe sio kweli.

Shtaka la tatu ni kutumia nyaraka kudanganya mwajiri ambapo kati ya 14.4.2022 na 16.04.2022 waliandaa maombi ya masurufu, ambapo Alex aliomba apatiwe Milionin65 kwaajili ya kununua kifusi kufanya marekebisho barabara za Arusha wakijua wanamdanganya mwajiri

Shtaka la nne ni matumizi ya nyaraka ambayo ni marejesho ya masurufu ya milioni65 alizodaiwa kupewa Alex katika kosa wanalodaiwa kulifanya  26.04.2022 

Shtaka la tano wanadaiwa kulifanya kati ya 16.4.2022 na tareh26.04.2022 ni kujaza form ya usambazaji na upokeaji wa moram, nyaraka ambayo inadaiwa kuwa ni ya uongo

Shtaka la sita wanadaiwa pia kulifanya kati ya 16.04.2022  na 26.04.2022 likihusiana na  fomu ya usambazaji na upokeaji wa Moram taasisi za Serikali likionyesha James Rafael alitoa huduma za usambazaji wa Moram kwa idadi ya vifusi  na kiwango Cha fedha kwa kila tripu jambo ambalo inadaiwa sio kweli.

Shtaka la Saba ni matumizi mabaya ya nafasi na kosa la nane dhidi yao ni kusababishia Serikali hasara ya shilingi mil65.Watuhumiwa wote walikana mashtaka yote.

Mwenendo wa kesi ulikuwa kama ifuatavyo baada ya upande wa mashtaka kumaliza kusoma tuhuma zinazowakabili Dkt.Pima na wenzake,

Jamhuri: Mheshimiwa Hakimu upelelezi wa shauri umekamilika na kwa mujibu wa kifungu Cha 91(3), sura ya 20 marejeo ya Mwaka 2022, upande wa mashtaka Uko tayari kuanza kusikiliza na hoja za awali ziko tayari.

Utetezi: Wakili Sabato Ngogo anasenma kwa kuwa watuhumiwa wote wamekana, mashtaka tunaomba wadhaminiwe, na kwa Sasa hatuko tayari kuendelea. 

Jamhuri: shauri hili ni la muda mrefu na limetokea 2022, lengo la Bunge kuunda kifungu hiki ni kukimbiza usikilizaji wa mashauri yanayotolewa na kurudishwa mahakamani, nasikitika juhudi za bunge zinafifishwa

DPP hana pingamizi na dhamana lakini tunaomba mahakama izingatie matakwa ya lazima ya kifungu Cha 36 (4e na 5 na 6), Cha Sheria ya uhujumu uchumi sura 200 marejeo2022 kwa Sasa, 

Hakimu: Mahakama imekubaliana na Mwendesha mashtaka ndugu Kyaka, kama shtaka limerudishwa mahakamani basi upande wa mashtaka lzm uwe na uhakika kwamba linasikilizwa.

Hata hivyo Mahakama imezingatia muda, haiwezi kuendelea kusikiliza. kwaajili ya fare trial hakuna dhambi shauri hili litapangiwa tarehe nyingine kuja kusikilizwa, na mahakama imekubaliana na dhamana, sharti kila mmoja awasilishe nusu ya kiasi kinachodaiwa kuibiwa kwa mwajiri, jumla tsh65, sawa na Mil32.5n

“Na sababu wako washtakiwa wako wanne wadeposit Mil8 au hati iliyofanyiwa tathmini ambayo itakuwa na thaman ya Tsh8m na kila Mshtakiwa awe na mdhamini mmoja atakayekuwa tayari kusaini dhamana ya m5 na barua ya utambulisho na kitambulisho na mwisho Mshtakiwa yoyote hatatakiwa kutoka nje ya Arusha mpaka apate kibali Cha mahakama,”amesema Hakimu.

Utetezi: Wakili Ngogo aliomba Mahakama kuwapa tena muda wa kumalizia kukamilisha zoezi la kurejeshewa nyaraka zao za wadhamini baada ya kesi ya mwanzo kuondolewa mahakamani ambapo Hakimu aliruhusu na kutoa pumziko la dakika45 na kwamba mahakama itarudi kwaajili ya kusikiliza ombi la dhamana.

Mahakama iliporejesha, upande wa utetezi uliwasilisha nyaraka za dhamana ambazo zilikaguliwa na upande wa Mwendesha mashtaka wa Serikali pamoja na Hakimu na kuwapatia dhamana Dkt.John Pima, Mariam na Maduhu huku Alex aliyekuwa akijitetea mwenyewe alishindwa kukamilisha nyaraka za dhamana na kuamriwa kwenda mahabusu Hadi atakapokamilisha nyaraka za dhamana.

Hakimu Mbelwa aliahirisha kesi hiyo Hadi Aprili 9, 2024 itakapokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa.