Mwandishi wetu, Babati
Babati. Timu ya soka ya Mdori FC, juzi imetwaa ubingwa wa michuano ya chemchem CUP mwaka 2019, iliyokuwa na lengo la kupiga vita ujangili na kuendeleza utalii, baada ya kushinda kwa penati 4-3 dhidi ya timu ya Majengo FC katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Mdori wilayani Babati.
Katika mchezo huo wa fainali, ambao ulikuwa umevuta maelfu ya watu, timu hizo zilitoka sale kwa kufungana goli 1-1 kwa dakika 90 na ndipo bingwa akapatikana kwa mikwaju ya penati, Manyara ndio walikuwa wa kwanza kupata gori dakika ya 57 kupitia kwa Andason Agustin na Mdoro walisawazisha dk 87 kupitia Rajabu Said
Baada ya fainali hiyo, Mdori walikabidhiwa kikombe chenye thamani ya zaidi ya sh 1.5 milioni na fedha taslimu sh 1.7 milioni na Spika wa hifadhi ya jamii ya Burunge, Marceli Yeno ambapo washindi wa pili walipewa zawadi ya fedha taslimu 1.1 milioni na kikombe zawadi zote zilizotolewa na mwekezaji wa Chemchem.
Washindi wa tatu wa michuano hiyo, timu ya Kisangaji ilipewa zawadi wa sh 650,000 na washindi wa nne timu ya Sangaiwe ilipata zawadi ya sh 300,000 na upande wa timu za mpira wa pete mabingwa walikuwa Mdori waliopewa zawadi ya sh 250,000 ,wa pili Mbuyuni 150,000 na timu ya tatu walimu 100,000.
Akizungumza baada ya michuano hiyo, Mratibu wa miradi ya jamii ya taasisi ya Chemchem Association ambayo, imewekeza hoteli na utalii wa picha katika eneo hilo,Walter Pallangyo alisema lengo la taasisi yao kudhamini mashindano hayo ni kuhamaisha vijana kupenda uhifadhi, kupiga vita ujangili na kuendeleza utalii.
“tunaamini Chemchem kama wawekezaji katika eneo hilo, michezo hii inasaidia pia kuwakutanisha vijana na kutambua vipaji vyao na baadhi wamekuwa wakipata fursa ya kuchaguliwa timu za nyingine nchini”alisema
Katibu wa chama cha soka wilaya ya Babati,Ramadhani Mnyoti alipongeza michuano hiyo, kwa kueleza imekuwa ikiibua vijaji lakini pia kusaidia kukuza utalii na kupiga vita ujangili kupitia michezo.
Michuano ya Chemchem CUP ambayo, ilikuwa inashirikisha timu 20 kutoka vijiji vinavyozunguka hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge,lengo lake ni kupiga vita ujangili, kuendeleza uhifadhi na Utalii katika eneo hilo.