Kaimu Meneja wa
TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu akizungumza.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha Miaka mitatu imepokea Fedha Shilingi Bilioni 47.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na matengenezo ya Barabara Mkoani humo.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu amesema kwa kipindi cha Miaka mitatu ya Fedha 20212022, 20222023 na 20232024 TANROADS imepokea Fedha Bilioni 47.2 ambapo imetekeleza miradi ya maendeleo kupitia wakandarasi wazawa.
Kaimu Meneja huyo ametaja maeneo yanayohudumiwa na TANROADS Mkoa wa Shinyanga huku akiishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta Fedha hizo kama sehemu ya kuimarisha usalama Barabarani.
“Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Shinyanga tunahudumia mtandao wa Barabara wenye jumla ya Kilomita 1,177.74 na jumla ya Madaraja 309 Barabara kuu ni 277.10, kilomita 787.54 ni Barabara za Mkoa na kilomita 113.1 ni Barabara zilizokasimiwa lakini kati ya kilomita 1,177.74 Barabara za Lami ni kilomita 261.02 na Barabara za Changarawe ni kilomita 916.72”.amesema Mhandisi Samwel Mwambungu
“Kwa kipindi cha Miaka mitatu ya Fedha 20212022, 20222023 na 20232024 tumepokea jumla ya shilingi Bilioni 47.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matengenezo ya Barabara kwa Mkoa wa Shinyanga ili kufanya mtandao wa Barabara uweze kupitika kipindi chote cha Mwaka”.
“Napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Fedha nyingi mahususi kwa ajili ya Mkoa wa Shinyanga ili kuifungua Shinyanga na kukuza uchumi kwa ujumla pia Mhe. Rais ameendelea kuleta Fedha kila Mwaka kwa ajili ya matengenezo ya Barabara ili zipitike kwa kipindi chote cha Mwaka ambapo kwa Miaka mitatu jumla ya Bilioni 325 zimeletwa kwa ajili ya miradi yote mikubwa na matengenezo”.amesema Mhandisi Samwel
Amesema katika jitihada za kukabiliana na Mvua za El nino tayari Serikali kwa kushirikiana na TANROADS imetenga Fedha za dharula kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 ili kuhakikisha Mvua hizo hazileti madhara makubwa kwenye sekta ya miundombinu na kwamba Barabara zilizonufaika na mpango huo ni Kahama – Solwa kilomita 79.96 ambayo mawasiliana ya Barabara yalikatika na kwa sasa inapitika vizuri.
Mhandisi Mwambungu amesema katika kipindi cha Miaka mitatu TANROADS Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kusimika jumla ya Taa 395 kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.18 katika miji na vijiji vya Tinde, Isaka, Kagongwa, Kahama, Segese na Bulige ambapo amesema zoezi hilo linaendelea na kwamba maeneo yatakayonufaika mengine ni pamoja na vijiji vya Solwa na Ngaya.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu amesema Mkoa wa Shinyanga una jumla ya Mizani mbili (2) ambayo ni Tinde na Mwendakulima inayotumika kudhibiti uzito wa Magari ili kulinda miundombinu ya Barabara.
Ameielezea miradi ya kitaifa inayosimamiwa na TANROADS Mkoa wa Shinyanga ikiwemo upanuzi au ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli Shinyanga, Ujenzi wa Barabara ya Mwigumbi – Lamadi kwa kiwango cha Lami ambayo sehemu ya kwanza ni Mwigumbi – Maswa ni kilomita 50.3
Miradi mingine inayosimamia na TANROADS Mkoa wa Shinyanga ni ujenzi kwa kiwango cha Lami Barabara ya Kagongwa – Bukooba – Nzega kilomita 66 ambapo 11.34 zipo Mkoani Shinyanga pamoja na ujenzi wa kiwango cha Lami Barabara ya Kahama – Kakola kilomita 73.
“Ofisi ya Meneja Wakala wa Barabara Mkoa wa Shinyanga imepewa jukumu la kusimamia ujenzi au upanuzi wa uwanja wa Ndege kwa kiwango cha Lami kilomita 2.2 kwa gharama ya shilingi Bilioni 44.803 Mkandarasi ni kutoka Kampuni ya CHICO ya China ndiyo inayotekeleza mradi huu chini ya usimamizi wa Mhandisi mshauri kutoka Kampuni ya SMEC Ltd kwa gharama ya shilingi 23,735554.00 na za kimarekani USD 2,602, 343.00 mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na European Investment Bank (EIB) hali ya utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 10.51 ambapo jumla ya ajira zilizotolewa ni 101 na 86 wakiwa watanzania ni asilimia 85.1 na 15 wakiwa wageni”.
“Mkoa wa Shinyanga unasimamia mradi wa kitaifa wa ujenzi wa kiwango cha Lami Barabara ya Mwigumbi – Maswa kilomita 50.3 ujenzi huu unatekelezwa na Mkandarasi wa Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Company Ltd (CHICO) pamoja na Mhandisi mshauri wa Kampuni ya KYONDONG Engineering Co. Ltd gharama ya mradi ni Fedha za kitanzania shilingi Bilioni 72.2 ajira zilizotolewa ni 224 na 205 wakiwa watanzania asilimia 91.5”.
“Ujenzi wa kiwango cha lami Barabara ya Kagongwa – Bukooba – Nzega upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujenzi wa Barabara ya Kagongwa – Bukooba (kilomita 18) – Nzega kwa kiwango cha Lami ulikwisha kamilika kwa asilimia mia moja (100)”.
“Ujenzi wa kiwango cha Lami Barabara ya Kahama – Kakola kilo mita 73 mradi huu umefadhiliwa na Kampuni ya uchimbaji Madini ya Barrick Gold Mine kwa jumla ya Dola za kimarekani Milioni 40 ambapo utekelezaji wa mradi huu unategemewa kuanza mara baada ya mfadhili na Mkandarasi kusaini mkataba kwa sasa hatua za kupata Mkadarasi zimekamilika na taratibu za kusaini mkataba ziko kwenye hatua za mwisho zikiratibiwa na Wizara ya Ujenzi”.
“Miradi iliyofanyiwa upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha Lami nipamoja na Barabara ya Kolandoto – Lalago kilomita 53 (Simiyu Border) ambapo upembuzi yakinifu wa kina wa Barabara hiyo ulikwisha kamilika kwa asilimia mia moja (100) kwa kiasi cha shilingi Milioni 450 utekelezaji wa ujenzi wa Barabara hiyo kwa kiwango cha Lami unasubiri kudhibitishwa kwa bajeti yake kwa ajili ya utekelezaji”.
“Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Salawe – Old Shinyanga ( sehemu ya Solwa – Old Shinyanga kilomita 64.66 ulikwisha kamilika kwa asilimia mia moja (100) na upembuzi huu uliratibiwa na ofisi ya Meneja Wakala wa Barabara Mkoa wa Shinyanga kwa gharama za shilingi Milioni 384”.
“Upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Mpanda – Kaliua – Ulyankulu – Uyogo – Nyamilangano – Nyandekwa – Kahama ulikwisha kamilika kwa asilimia mia moja (100) huku usanifu wa kina ukiwa unaendelea kwa shilingi Milioni 500”.
“Usanifu wa Barabara Old Shinyanga Bubiki kilomita 35 umekamilika na Serikali itatekeleza ujenzi wake baada ya kupata Fedha”.amesema Mhandisi Samwel Mwambungu
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kulinda miundombinu ya Barabara ikiwemo alama za Barabarani na Taa, kutomwanga Mafuta na Oil kwenye lami, wasafirishaji kutozidisha uzito kwenye Magari ili kulinda Barabara, waendesha vyombo vya moto kuheshimu alama za Barabarani ili kuepuka ajali pamoja na kulinda na kutovamia hifadhi ya Barabara.
Kaimu Meneja wa
TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Samwel Mwambungu akizungumza.