Niko tayari kuondolewa mpango wa TASAF, wengine waingie: Veneria

  • Asema elimu ya ujasiriamali imemuondolea umaskini

Na Seif Mangwangi, APC Media- Moshi

ELIMU ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha ni miongoni mwa nyenzo kuu ambayo imewasaidia wafaidikaji wa ruzuku inayotolewa na mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF na kuwaondoa kwenye umaskini.

Hayo yamebainishwa na Veneria Agusti (56), mkazi wa kata ya boma ya mbuzi mtaa wa relini katika Manispaa ya Moshi ambaye anasema yuko tayari kuondolewa kwenye mpango wa TASAF baada ya hali yake kiuchumi kuimarika.

” Kwa kweli nashukuru sana TASAF kwa msaada mkubwa ambao wamenipatia, nimefaidika sana na elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha, nilianza nikiwa fukara lakini hivi sasa naweza kuhudumia familia, nimejenga nyumba kwa biashara zangu za ufugaji,” anasema.

Veneria Agusti Teti akifanya mahojiano na Mwandishi Veronica Natalis nje ya nyumba yake aliyoijenga baada ya kuwekeza fedha kidogo kidogo kupitia mpango wa TASAF

TASAF iko kwenye tathmini ya mwisho ya awamu ya pili ya mpango wa tatu wa kuwezesha kaya maskini nchini kuhakiki wafaidikaji wa mfuko huko ambao hali zao za maisha zimeimarika kutoka katika hali ya awali ya ufukara ili kuziondoa na kuingiza kaya zingine.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, Shedrack Mziray Hadi kufikia Septemba 2024 kaya Laki nne zitaondolewa na kuanza mchakato wa kuingiza kaya mpya zenye hali duni ya maisha.

Veneria Agusti Teti akiwa nje ya nyumba yake ya udongo yenye chumba kimoja aliyokuwa akiishi na familia yake kabla ya kujenga nyumba ya tofali, hivi sasa anatumia chumba hicho kufungua kuku

Veneria Agusti anasema hapo mwanzo alianza kupokea Shilingi 46000 kutoka TASAF ambazo zilimwezesha kununulia chakula na kusomeshea wanae lakini baadae aliweza kuhifadhi fedha kidogo anayopokea na kuanzisha mradi wa kufuga kuku wa kienyeji.

“Kupitia ruzuku ya TASAF nimeweza kufuga kuku, nikaanzisha mradi wa kuuza maandazi na kitembeza mtaani, baadae nikajiunga kwenye kikundi ambacho tulisaidiwa na wataalam wa TASAF ambapo tunawekeza hisa, tunakopeshana na baadae tunagawana faida, hii imenisaidia sana kumudu maisha yangu tofauti na mwanzo,” anasema.

Anasema hivi karibuni alipokea ruzuku ya 350,000 kutoka TASAF ambapo anatarajia kutumia fedha hiyo kuanzisha mradi mkubwa wa kufuga kuku wa kisasa ambao utaweza kumuingizia fedha nyingi zaidi.

Nyumba ya Veneria Agusti Teti inavyoonekana kwa mbele, pembeni ni sehemu ya kuku wa kienyeji anaowafuga hivi sasa