- Lengo kuu ni kuibua vipaji vya wanafunzi
- Agawa vifaa vya michezo, Timu nane kushiriki
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Mtanzania Ashok Mittal (17), anayesoma elimu ya juu Dubai katika falme za nchi za Kiarabu (UAE), ameanzisha mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana wa shule za Sekondari kwa lengo la kuhamasisha michezo kwa vijana shuleni.
Mashindano hayo yaliyoanza Leo Agosti1,2024 yanayojulikana kama ” Champion of Tomorrow” yameshirikisha timu nane za Sekondari ikiwemo washiriki kutoka Sekondari za Serikali na binafsi.
Shule zinazoshiriki michuano hiyo ni pamoja na Sekondari za Serikali za Lemara, Sombetini, Sinoni na Mateves huku Sekondari binafsi zikiwa ni St.Patrick, Renea, Kilimanjaro modern Boys Academy na Brainy Heroes zote za Jijini Arusha.
Ashok amesema timu zote zinazoshiriki michuano hiyo zimepata udhamini kupitia kampuni mbalimbali hapa nchini ambapo zitapewa jozi za viatu vya kuchezea mpira, t-shirt, mpira na gloves kwaajili ya makipa.
“Nina furaha kubwa kuanzisha ‘Champions of Tomorrow Football League’ hapa Arusha. Lengo langu ni kutoa fursa kwa vijana wasio na uwezo kutimiza shauku yao ya mpira wa miguu na hatimaye kufikia viwango vya kitaaluma, kwa kutoa vifaa muhimu vya michezo,” anasema na kuongeza:
“Kwa kushirikiana na makocha wa timu zote pamoja na baadhi ya wakufunzi kutoka katika vituo vinavyolelea Watoto wenye vipaji vya mpira wa miguu(scout) Jijini Arusha, tutaweza kuwawezesha malengo na ndoto za vijana wetu kutimia na kuchangia maendeleo chanya katika jamii yetu,”.
Amesema mpango huo ni juhudi za pamoja kati yake binafsi pamoja na ushirikiano wa misaada kutoka kwa wadhamini mbalimbali waliojitokeza kudhamini michuano hiyo.
Mashindano hayo yanayoendeshwa kwa njia ya mtoano yatafikia kilele chake Agosti 8,2024 ambapo itachezwa fainali kwa timu ambazo zitakuwa zimefanikiwa kufikia hatua hiyo baada ya kupenya katika hatua ya mtoano.
Katika mchezo wa kwanza Leo hii timu za Sekondari ya St. Patrick na Sombetini zilitoshana nguvu kwa goli 2-2 katika mchuano mkali uliofanyika kwenye viwanja vya mpira vya shule ya kimataifa ya UWC.
Ramadhani Abbasi na Emmanuel Masanja ndio walioipatia timu ya Sekondari ya St.Patrick magoli huku Sekondari ya Sombetini ikipata magoli yake kupitia kwa wachezaji wake mahiri Boniface Exaveri na Yusuf Kassim.
katika mchezo wa pili timu ya Sekondari ya Lemara iliinuka kidedea dhidi ya Sekondari ya Kilimanjaro modern Academy kwa jumla ya goli 1-0. Goli hilo la Sombetini Sekondari lilifungwa na Hajiru Nassoro aliyewazidi ujanja walinzi wa timu ya Kilimanjaro.
Kocha wa timu ya mpira ya Sekondari ya St.Patrik Dennis Shemtoe amempongeza muandaaji wa michuano hiyo na kushauri kufanyike kwa maandalizi mazuri zaidi hapo baadae kufuatia kuwepo kwa changamoto ya waamuzi wasaidizi.