Cbe yaanza kufundisha shahada za umahiri kwa mtandao

Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara, (CBE) Profesa Edda Lwoga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu chuo hicho kuanzisha kozi za Shahaza za Umahiri mtandaoni (online masters degree) kwa fani sita. Kushoto ni  Dk Shima Banele ambaye ni Mkurugenzi wa Taaluma na kulia ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Dk William Gomera.

Na Mwandishi Wetu

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka watanzania kuchangamkia fursa za masomo ya Shahada za Umahiri mtandaoni kwani wataokoa muda na gharama kulinganisha na kusoma darasani

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuanzishwa kwa kozi hizo.

Alisema  CBE imekuwa ikitoa Shahada za Umahiri  takribani 10 katika fani za biashara na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA na sasa wameona ni wakati muafaka kuanza kufundisha kwa njia ya mtandao.

“Kwa sasa tumeanzisha Shahada sita za umahiri mtandaoni ‘Online Master’s Degree’ kwa fani sita ambapo tayari tumeanza kupokea maombi kwa muhula wa Machi na kusoma kwa njia ya mtandao (Online) kuna faida kadhaa ambazo zimefanya njia hii ya kujifunza kuwa maarufu na yenye ufanisi kwa watu wengi,” alisema

Aidha, Profesa Lwoga alitaja faida za kusoma kwa njia ya mtandao kuwa kunamwezesha mtu kusoma kutoka mahali popote na wakati wowote unaofaa  bila kujali eneo lake au muda wa siku.

“Kusoma kwa mtandao  mara nyingi hupunguza gharama zinazohusiana na elimu, kama vile usafiri, malazi, na vifaa vingine. Hii inafanya elimu kuwa nafuu zaidi na inawapa watu fursa ya kufuata masomo bila kuhitaji kuhamia au kutenga bajeti kubwa,” alisema Profesa Lwoga.

Alisema njia hiyo inawapa wasomi uwanda mpana wa kuchagua programu na inaruhusu wanafunzi kuchagua masomo yanayolingana na malengo yao na maslahi yao, bila kujali wanavyoishi.

Profesa Lwoga alisema kusoma kwa mtandao mara nyingi humuunganisha mwanafunzi na teknolojia za kisasa kama vile majukwaa ya mtandao, mabaraza ya mazungumzo na zana za ushirikiano na inaboresha uzoefu wa kujifunza.

Alisema njia hiyo inamwezesha mwanafunzi kushirikiana na wenzake kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema kupitia njia hiyo wanafunzi wanaweza kusoma kwa kasi yao wenyewe, kurudia sehemu zenye changamoto, au kuchunguza zaidi masomo yanayowavutia na kwamba inaruhusu kila mtu kujenga uelewa imara wa mada wanazojifunza.

“Kusoma kwa njia ya mtandao huleta ubunifu wa rasilimali za kujifunza, na mara nyingi huja na rasilimali nyingi za dijitali kama vile video, vitabu vya elektroniki, na michezo ya kujifunza na hii inaboresha njia za kufundisha na kufanya masomo kuwa ya kuvutia zaidi na yenye kuvutia,” alisema.

Alisema wanafunzi wa kusoma mtandaoni wanapata uzoefu wa matumizi ya teknolojia, ambayo ni ujuzi muhimu katika ulimwengu wa kisasa wa kazi na  inawawezesha kuwa tayari kwa changamoto za teknolojia kazini.

“Kwa ujumla, kusoma Online kunaweza kuwa chaguo linalowavutia wengi kwa sababu ya urahisi, ufanisi wa gharama na upatikanaji wa rasilimali za kujifunza,” alisema.

Alisema CBE imewekeza katika miundombinu bora, teknolojia ya kisasa na mazingira mazuri ya kujifunzia, huku ikiweka mkazo kwenye maadili ya kitaaluma na utawala bora mambo ambayo yameifanya CBE kuwa chaguo bora kwa wanaotafuta elimu ya biashara.