Mkuu wa Mkoa Manyara awapa Kongole Vijana Maonyesho nane nane Kaskazini

Egidia Vedasto

Arusha.

Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga amepongeza idadi kubwa ya vijana wanaotoa elimu kwenye mabanda katika maonyesho ya Nane nane na kusema hiyo ni ishara ya mabadiliko makubwa katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza wakati wa kufunga maonyesho ya nanenane Kanda ya Kaskazini, RC Sendiga amesema sekta ya Kilimo na ufugaji imekuwa ni mhimili mkubwa nchini katika kuinua kipato Cha mtanzania.

Amewataka Maafisa Ugani kuwa mfano bora katika uzalishaji, kutoa ushauri na ushirikiano kwa wakulima na wafugaji ili kuimarisha zaidi sekta hiyo ili kujihakikishia usalama wa chakula na kuwainua watanzania kiuchumi

Aidha RC Sendega amewapongeza wazazi kuwaruhusu wanafunzi kufika katika maonyesho hayo na kujifunza namna bora ya kufanya kilimo, uvuvi na ufugaji kwa njia za kisasa.

“Jitihada zetu Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji shughuli za uzalishaji, kufanya Wakulima wavune mwaka mzima kwa kutumia Kilimo cha umwagiliaji, Wafugaji kufuga kisasa na kuotesha nyasi zinazosaidia kuwa akiba katika kipindi cha kiangazi na Wavuvi kutumia nyenzo bora, hii itatusaidia kuzidi kuimarisha uchumi wetu” amesema Sendiga.

Mshiriki wa maonyesho anayejikita kuzalisha mbegu za mbogamboga na nafaka, Afisa kilimo , Philpo Matombo kutoka SEEDCO, amesema maonyesho ya mwaka huu yamekuwa na muitikio mkubwa wa watu wanaotaka kujifunza na kutumia mbegu zao.

“Mbegu zetu ni nzuri na wakulima wanashuhudia wanavyonufaika kwa mavuno mengi, kwani tunazingatia ubora unaokwenda na mabadiliko ya tabia ya nchi”amefafanua Matombo.

Bwana Shamba Philpo Matombo wa SeedCo akiwapitisha Viongozi mbalimbali akiwemo RC Kilimanjaro Nurdin Babu wa tatu kutoka kushoto katika mashamba ya mbogamboga

Kwa upande wake Afisa Uwekezaji wa Kituo cha Uwekezaji TIC Valentine Kagombora, amewataka wakulima, wafugaji, wavuvi na Watanzania wote kwa ujumla kuwekeza kwani mazingira ni rafiki yanayompa nafasi ya kupata huduma jumuishi.

“Wawekezaji wote wawe wazawa au wageni mazingira yameboresahwa hakuna kuzunguka bali huduma zote kama BRELA, TANESCO, TRA, NIDA, UHAMIAJI, IDARA YA KAZI, ARDHI na nyinginezo zote zinapatikana kwa pamoja, hii yote ni kumrahisishia mteja wetu na kumfanya awe huru” ameeleza Kagombora.

_Afisa Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji (TIC) Valentine Kagombora katika maonyesho ya nanenane, akieleza mazingira bora yaliyoboreshwa kwa Wawekezaji wazawa na wageni_