ORXY wamuunga Mkono Gambo kampeni kugawa vifaa saidizi

  • Ni kwa wenye ulemavu, yatoa mitungi500 ya gesi

Na Mwandishi Wetu, Arusha
Kampuni ya Orxy Gas Tanzania Limited inayozalisha na kusambaza nishati ya gesi za majumbani imemuunga mkono Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo kwa kutoa msaada wa mitungi midogo 500 kwa familia zenye Watoto wenye ulemavu.

Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na Mbunge huyo kwaajili ya kugawa vifaa saidizi kwa watoto wenye ulemavu Jijini Arusha jana, Meneja masoko wa Orxy Energy, Peter Ndomba amesema msaada huo ni sehemu ya misaada mbalimbali ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiitoa kwa familia duni nchini lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kuokoa mazingira yetu.

Akitoa elimu ya matumizi sahihi ya nishati ya gesi, Ndomba amewatahadharisha watumiaji wa nishati hiyo kuwa makini na bidhaa hiyo kwa kutofunga milango wakati wa matumizi ili kuepuka athari kubwa endapo itatokea ikalipuka.

” Ningependa kuwapatia elimu kidogo ya matumizi ya nishati ya gesi, ukiwa nyumbani wakati unatumia gesi hakikisha milango Iko wazi ili hewa iweze kuingia na kutoka, lakini pia gesi yetu imetengenezwa kwa kuwekwa harufu kama yai viza, lengo ni kama ikatokea gesi ikavuja ni rahisi kusikia harufu tofauti na mtumiaji kuchukua tahadhari,” Amesema.

Kwa upande wake Mrisho Gambo amewashukuru wadau mbalimbali kujitokeza kugawa vifaa hivyo ikiwemo kadi za bima ya Afya kwa watoto wenye ulemavu.

” Zoezi hili sio mara ya kwanza kulifanya hapa Arusha, tangu nimekuwa Mbunge mwaka 2000 tumekuwa tukigawa vifaa mbalimbali kwa walemavu lakini pia tumekuwa na utaratibu wa kusaidia kulipia bima ya Afya, namshukuru Rais Samia kwa kurejesha Bima kwa watoto, hii imesaidia sana,” amesema.

Amesema katika zoezi hilo la ugawaji wa vifaa tiba, Watoto 600 watapatiwa bima ya Afya ambapo kati yake yeye binafsi amelipia Watoto 210, mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Mount Meru Petroleum Atul Mittal amelipia Watoto 100, Satbir HansPaul pamoja na marafiki zake Watoto 100 na Jiji la Arusha kupitia kwa mkurugenzi wake Juma Hamduni wamelipia Watoto 200.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Juma Hamsini amesema ofisi yake imeamua kumuunga mkono Mbunge huyo kwa kuwa kazi anayoifanya ni sadaka kwa Mungu lakini pia anatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

“Kwa kuwa kazi hii inayofanywa na Mbunge ni kazi ya Mungu sisi kama Jiji tunamuunga mkono na tunaahidi kulipia bima ya Afya Watoto 200 pamoja na baiskeli mwendo (wheel chair), tatu, hivyo Jumatatu nitakabidhi hundi ya milioni 11,” amesema.

Gambo amesema pamoja na idadi hiyo ya Watoto kuonekana kuwa kubwa bado Kuna uhitaji wa Watoto wengine zaidi na ameshawasiliana na Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Kuji ambaye ameahidi kuchangia Watoto 223.

Awali akitoa salamu, Mkurugenzi wa Mount Meru Petroleum, Atul Mittal aliwataka walemavu kutokata tamaa na kujionea huruma na badala yake wawe maono ya kujiendeleza kwa kuwa wanauwezo wa kufanya hivyo.

” Nafikiri kila mmoja wenu hapa ameona nilivyonyanyuka kwenye kiti na ninavyotembea, naweza kusema na Mimi pia ni mlemavu, nilipata shida nikalala kitandani zaidi ya miaka miwili nakula na kujisaidia kitandani, lakini Leo hii naweza kusimama na kufanyakazi zangu kwa hiyo na wewe usikate tamaa,” alitoa ushauri Atul.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel alimpongeza Gambo kwa Upendo wake anaoonyesha kwa wakazi wa Arusha na kumtaka kuendelea kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo kwa kuwa hilo ndio jambo la kwanza ambalo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiliagiza kwa wateule wa Chama hicho.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha sekta ya Afya kwa kununua vifaa vya kisasa vya matibabu na kutibia magonjwa sugu ambayo awali yalikuwa hayatibiki nchini mpaka nje ya nchi na kwa gharama kubwa jambo ambalo lilisababisha watu wengi kupoteza maisha.

Mbali ya kugawa mitungi ya gesi na kutoa bima ya Afya kwa watoto walemavu pia katika hafla hiyo Mbunge Gambo alikabidhi vyereheni kwa vituo vinavyolelea Watoto yatima, vitanda na magodoro pamoja na baiskeli mwendo ambazo zimetolewa na hospitali ya CCBRT kwa bei ya punguzo ya Shilingi 100,000 kwa kila baiskeli.

Peter Ndomba mwenye kofia nyekundu akiwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt Godwin Mollel na Mbunge wa Arusha Mrisho Gambo pamoja na viongozi Maaskofu na shekh wa Mkoa wa Arusha pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wakimpatia jiko la Gesi mmoja wa wazazi mwenye Watoto wenye ulemavu