Mwekezaji Salim Alamry asota Mahabusu kwa uhujumu uchumi

*Kesi yake yatajwa mahakamani na kuahirishwa

*DPP atajwa kuwa kikwazo kutoa idhini ianze kusikilizwa

Na Seif Mangwangi, Arusha
MWEKEZAJI na mfanyabiashara katika sekta ya uwindaji wa kitalii nchini, Salehe Salim Alamry ameendelea kushikiliwa mahabusu ya gereza la Kisongo Jijini Arusha huku Mahakama ikishindwa kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa kukosa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.

Wakizungumza Jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Aisha Ndosi ambapo mfanyabiashara huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya pili na kesi yake kutajwa na kuahirishwa kwa mara nyingine, waendesha mashtaka wa Serikali wamedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika lakini pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),hajatoa hati kuruhusu mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.
Wakili wa Serikali pia alisema bado hawajajua ni makosa yapi watawawashitakia nayo watuhumiwa.

Alamry pamoja na Wakili wa kujitegemea Sheck Mfinanga wanakabiliwa na mashtaka 26 ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha ikiwemo kufanya udanganyifu na kughushi nyaraka mbalimbali za uwekezaji dhidi ya wanahisa wenzake ikiwa ni kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu [CAP.16

Mwekezaji na mfanyabiashara Salim Saleh Alamry akiwasili mahakama

Watuhumiwa hao wanadaiwa kwa nyakati tofauti wakiwa katika miji ya Arusha, Dar es salaam na maeneo mengine nchini Machi 2019 kwa makusudi huku wakijua ni kosa kisheria walifanya ulaghai kuhusu mgawanyo wa umiliki wa hisa katika kampuni ya Sunset Tarangire Limited.

Wakili wa utetezi upande wa mfanyabiashara Salehe Salim Alamry, Moses Mahuna anayeongoza jopo la mawakili wanaomtetea aliiomba Serikali kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kwa kuwa mteja wake anaendelea kuteseka magereza na shughuli zake kukwama kufuatia kesi yake kutokuwa na dhamana.

“Tunaomba uchunguzi ufanyike haraka sababu mshtakiwa yuko mahabusu zaidi ya mwezi sasa, tungeomba pia upande wa mashtaka utoe idhini kwa Mahakama hii kusikiliza kesi yetu ili tuone mashtaka ambayo hayahitaji upelelezi kukamilika ili tuweze kuendelea nayo,”ameomba Wakili Mahuna.

Aidha mwekezaji huyo Saleh Alamry anadaiwa kufanya udanganyifu na kughushi nyaraka mbalimbali za umiliki wa kampuni ya Sunset Tarangire limited akidaiwa kutengeneza hati za uongo za makubaliano kati yake (MOU), na washirika wenzake Khaled Alrajhi na Abdulkarim Alrajhi kama ni washirika katika kampuni hiyo huku wakionyeshwa kusaini hati hiyo jambo ambalo ni uongo.

Makosa yote hayo mwekezaji Salehe Salim Alamry anadaiwa kuyafanya kwa tarehe tofauti tofauti katika miji ya Arusha na Dar es salaam.

Hata hivyo kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi niAisha Ndosi baada ya mahakama hiyo kutokuwa na kibali cha kuruhusu kuisikiliza kutoka kwa Mkurugenzi wa makosa ya jinai(DPP).

Mbali ya Wakili Moses Mahuna, awakili wengine anayemtetea Mwekezaji Alamry ni Faisal Rukaka huku mshtakiwa wa pili Sheck Mfinanga ambaye yuko nje kwa dhamana kufuatia mashtaka yanayomkabili kudhaminika anatetewa na Wakili Mariam mrutu.

Mawakili wanaomtetea Mwekezaji Salim Alamry na Wakili sheck Mfinanga wakiwa wanaingiza katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwaajili ya kusikiliza kesi inayomkabili wateja wao.