Mihimili ya nchi yatakiwa kutoingilia Demokrasia

Egidia Vedasto

APC Media, Arusha.

Tunu ya Amani ya Nchi iliyoachwa na Waasisi wa Nchi hii imetakiwa kulindwa na kutunzwa, pasipo kuingiliwa na nguvu ya mhimili wowote.

Hayo yamesemwa na Askofu wa KKKT Dayosisi Karagwe, Kagera Dkt. Benson Bagonza katika hafla ya usiku wa kufunga Wiki ya CSO Jijini Arusha, na kuitaka serikali kuwa makini na vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu vinavyoendelea nchini ili kuondoa mashaka na hasira mioyoni mwa watu.

“Naogopa vurugu za Wasio na Matumaini kuliko wenye Madaraka, hatuwezi kuendelea hivi ikiwa hakuna Uchumi na Demokrasia huru” amesema Dkt. Bagonza.

Aidha ameonya kuchezewa kwa mfumo kama ilivyo sasa, mashaka ya wananchi juu ya kesho yao, kukosekana kwa uhuru wa kutoa maoni binafsi, udikteta ndani ya vyama vya siasa, Mfumo kuwanyima kuwajibishwa wakati huo wakiwataka wananchi kutoa fadhila, Mfumo kuruhusu kupiga kura badala ya kuchagua na kuingilia mfumo wa dola katika maamuzi.

“Imefikia wakati wanasiasa wa chama kilichoko madarakani hawako huru kutoa maoni kukosoa wanapoona mambo hayaendi sawa, Wanasiasa wa vyama vingine nao wanaogopa kutoa maoni yao, hata nyie AZAKI mna hofu kutoa maoni yenu juu ya mwenendo wa nchi, hii ni hatari na giza kwa kesho yetu, hakuna serikali isiyokosolewa duniani kote, hii inasaidia kuwakumbusha wajibu wao na sio kuwaogopa” ameeleza Dkt.Bagonza.

Mtendaji Mkuu wa Vodacom Mkoa wa Arusha George Venant amesema kwamba, wamewaezesha vijana 30 kuhudhuria Wiki ya CSO na kuahidi kuendeleza ushirikiano na Taasisi hiyo.

George amesema, “Tunategemea mwakani wateja wetu kuongezeka zaidi ili ifikapo 2050 malengo yetu yaweze kufikiwa”.

Wakati huohuo Rais wa AZAKI Dkt.Stagmata Tenga amezitaka taasisi zote nchini kuendeleza ushirikiano katika kuongoza jamii ili ziwe imara na rasilimali watu wenye uwezo na kuelewa ikizingatiwa haki na utu wao.

“Tunahitaji nguvu ya pamoja kufikia malengo yetu, na kila mmoja kukaa vizuri katika nafasi yake namna ya kubadilisha uchumi na mtazamo wa jamii inayotuzunguka” ameeleza Dkt. Tenga.

Washiriki kutoka Taasisi na Mashirika mbalimbali wakiwa katika Jukwaa la Wiki ya CSO Jijini Arusha