TAKUKURU Arusha yahimiza watoa rushwa wasichaguliwe wakati wa uchaguzi

Na Claud Gwandu, Arusha.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Arusha imewata wapiga kura katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kutumia kura zao kuchagua wagombea wasiotoa rushwa.

Imesema,kura ni chanzo cha maendeleo pale wanapochaguliwa viongozi waadilifu na wenye kujali maslahi ya taifa.

Kamanda wa TAKUKURU mkoani humo,Zawadi Ngailo amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake leo kuwa taasisi hiyo imejipanga kutoa elimu ya kuzuia rushwa katika makundi mbalilmbali ya kijamii mkoani humo.

“Kura ni kitu cha thamani sana na dhamana kwa Kiongozi.Ni chanzo cha maendeleo pale tutakapopata viongozi waadilifu na wenye kujali maslahi ya taifa.

” Kila mpiga kura atumie kura yake ipadavyo kuchagua mgombea asiyeshawishi kuchaguliwa kwa kutoa rushwa, iwe katika nafasi yoyote Ile.

“Wahenga walisema,nchi yoyote hujengwa na wananchi wenyewe, na inaweza kubomolewa pia na wananchi hao hao,” anasisitiza,na kuongeza:

“Ewe Mtanzania, tuijenge Tanzania kwa kukataa na kukemea vitendo vya rushwa katika uchaguzi,chagua Kiongozi bora, usidanganyike kwa fedha,vinywaji na fadhila zozote.”

Kamanda huyo alitaja maeneo yenye ushawishi wa rushwa wakati wa uchaguzi kuwa ni pamoja na wakati wa uteuzi wa wagombea ngazi ya chama na kipindi cha kampeni ambako kuna matumizi ya fedha ngazi ya chama,Tume na mgombea.

Maeneo mengine,kwa mujibu wa Kamanda huyo,ni pamoja na wakati wa upigaji kura,kujumlisha na kutangaza matokeo na kipindi cha kushughulikia malalamiko baada ya kura.

Aidha,alitaja baadhi ya vitendo vya rushwa vinavyofanyika katika uchaguzi kuwa ni pamoja na ugawaji wa fedha taslimu, ugawaji wa vitu kama kanga, fulana,vinywaji na vyakula na ahadi mbalilmbali zikiwemo za ajira,mikopo na upendeleo maalum.

Vitendo vingine ni kutumia lugha za vitisho,nguvu na mabavu ili kuwalazimisha kupiga kura au kuwazuia kupiga kura.

Kuhusu athari za rushwa katika chaguzi,Kamanda huyo anaeleza kuwa zinaathiri mchakato mzima wa demokrasia ya uwakilishi na maendeleo ya taifa.

Anataja athari zaidi kuwa ni kunyima mpiga kura haki ya kuchagua mgombea anayemtaka na kunyima mgombea asiyetoa rushwa haki na fursa ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.

Athari nyingine ni pamoja na kuminya utoaji wa haki na kuchaguliwa kwa kiongozi anayetumia muda wa uongozi kurejesha fedha alizotumia wakati wa uchaguzi badala ya kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hufanyika kila baada ya miaka mitano na mwaka huu umepangwa kufanyika nchini kote Novemba 27.

Waandishi wa habari wakifuatilia mazungumzo ya Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha