WEGS KUMUINUA MTOTO WA KIKE.

Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.

Suala la mtoto wa kike limekuwa likijadiliwa kwa kina na kwa upana wake kwa muda mrefu, kwa sababu licha ya jitihada kubwa za Kimataifa na kitaifa za kumkomboa mtoto wa kike, bado asilimia kubwa ya jamii yetu haijatambua umuhimu wa kuelimika kwa mtoto wa kike.

Taifa na Wazazi wanapaswa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha pamoja na kuwa majasiri kwenye kupigania nafasi za uongozi na maamuzi katika jamii.

Mtoto wa kike akisoma anapata uwezo wa kujitambua na kujiamini, Kujitambua huko kunaendana na uwezo wa mtu kujua haki zake na wajibu wake katika jamii, kujiamini katika kutoa uamuzi, kushiriki katika masuala yote ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kufanya maamuzi ya msingi.

Licha ya jitihada kubwa za kumkomboa mtoto wa kike duniani changamoto ambazo amekuwa akikabiliana nazo ni pamoja na ubaguzi, unyanyasaji wa kijinsia, kudhulumiwa haki zake ikiwemo haki ya kupata elimu, ukatili, na hata ndoa za utotoni.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu Duniani UNFPA kwa msisitizo, linataka kila nchi, jamii na mtu mmoja mmoja kuhakikisha haki za mtoto wa kike zinalindwa.

Sambamba na UNESCO, UNFPA, UN, WHO na mengineyo, Shirika la Women Economy and Gender Support (WEGS) kupitia mradi wa Promote Potential for Adolescent Girls, mradi unamfundisha mtoto wa kike kujitambua, kujitetea, kujua haki zake za msingi na kujifunza stadi za maisha ili kumuandaa kuwa mwanamke mwenye malengo na anayejitambua kwa siku za usoni.

Mkurugenzi wa Shirika hilo, Joyce Mwanga amesema Mradi huo unatelekezwa kwenye shule 10 za secondari za mikoa mitatu ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara unakusudia kumvusha mtoto wa kike katika kipindi cha Ugoli chenye mabadiliko mengi ya mihemuko kumpa elimu, ushauri na msingi mzuri ili aweze kufikia malengo yake bila kizuizi chochote.

“Mradi huu unaolenga kumvusha na kubadilisha mtazamo wa mtoto wa kike katika jamii, kuachana na mawazo ya kudhoofisha fikra zake kwamba mtoto wa kike hawezi, ni wa kuolewa na kuzaa tu na hawezi kumiliki uchumi na kupata nafasi za uongozi, pia tumekuwa tukiwashirikisha watoto wa kiume ili wabadilishe mtazamo juu ya mtoto wa kike mapema, ndio maana tupo hapa leo” amesema Mwanga.

WEGS kwa kutambua juhudi za wanafunzi walioshiriki katika mafunzo ya stadi za maisha limewatunukia wanafunzi 67 vyeti vya ushiriki na ushindi wa Shule za Sekondari Nduruma na Kikwe zote za jijini Arusha.

Motisha huo ulitolewa kwa wanafunzi sita wa kike kutoka shule zote mbili kila mmoja kiasi cha shilingi 120,000 na wavulana sita kutoka shule hizo kiasi cha shilingi 50,000 kila mmoja huku wanafunzi 48 wakipata vyeti.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kikwe Julius Sindato, amelipongeza Shirika la WEGS kwa mradi wenye lengo la kusaidia wasichana na wavulana kwa ujumla ili sambamba na masomo ya darasani pia waweze kupata ujuzi wa kazi za mikono na kuibadilisha jamii.

“Kipekee ninafarijika mno kuona jitihada hizi, nawashukuru WEGS na ninaomba muendelee kushirikiana nasi kuwapa elimu watoto wetu, hii ilikuwa kazi yetu kwa agizo la serikali lakini mkaona umuhimu wa kuleta mradi shuleni hapa na kunufaisha watoto wetu, ikiwezekana mafunzo haya yawe kwa mwaka mzima kwa sababu naamini matokeo yake ya baadaye yatabadilisha fikra na mtazamo kwa wanafunzi wengi” amesema Mwalimu Sindato.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la DKA Nchini Tanzania lililopo nchini Austria Amina_Anna Ndiko amesema Shirika hilo linasapoti miradi ya maendeleo nchini, ikiwemo ya kumuendeleza mtoto wa kike na kuhakikisha anatambua fursa, kuweka mipango na kufikia malengo yake ya hapo baadae.

Amefafanua kwamba, Shirika hilo kufadhili mradi wa (Promote Potential for Adolescent Girls) ni mkakati wa muda mrefu Kimataifa katika jitihada kumuinua mtoto wa kike na kuielimisha jamii kutambua usawa wa kijinsia.

“Katika jitihada za kufanikisha lengo la mtoto wa kike kujitambua na kutimiza ndoto zake, tunawashirikisha watoto wa kiume na kuwapa elimu kuondokana na dhana potofu za mapokeo ya mababu zetu kwamba mtoto wa kike hana haki, ataolewa na ataondoka kwenda jamii nyingine bila kuwa na msingi wowote wa maisha” amefafanua Ndiko.

Aidha Afisa Mradi wa Promote Potential for Adolescent Girls Emmanuel Mwenera, ameeleza malengo ya kuwafundisha wanafunzi stadi za maisha ni kuona wanapata kitu cha kufanya pale watakapomaliza masomo yao ya kidato cha nne kwa ule muda wanapokuwa wakisubiri matokeo.

Mwonera ameeleza kwamba, wanafunzi wengi wanamaliza masomo lakini wachache ndio hufanikiwa kuendelea na masomo ya ngazi ya juu, wakati huo waliofeli wengi wao wakibaki na maulizo juu ya kesho yao.

“Naiomba serikali kuangalia upya juu ya shule zote nchini kufundisha masomo ya kazi za mikono, ili kuwasaidia watoto kupata maarifa na ujuzi wa maisha badala ya kila anayemaliza masomo kuwaza kufanya kazi ofisini” ameomba Mwenera.

Sambamba na hayo Afisa ushauri katika mradi huo Noreen Teri, ameeleza mategemeo yake kwa wanafunzi waliopata elimu ya mradi ni kuhakikisha wanabadilika na kuwa mfano bora, kutambua vipaji vyao, kufahamu malengo yao ya muda mrefu na mfupi katika umri wa ujana.

“Natamani wasichana wasichezee fursa yoyote inayoweza kubadili historia yao katika maisha, na kutambua kwamba hakuna kinachoshindikana mbele ya bidii, nia na nidhamu” amesisitiza Noreen.

Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SASA Foundation linalofanya kazi ya kuwajengea uwezo wa kuwainua wanawake kiuchumi, kuangalia changamoto na kuzitatua, limetoa fursa kwa wanafunzi wote walioshiriki masomo ya stadi za maisha kupata ujuzi zaidi katika chuo chake cha SASA Foundation.

“Mara zote tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na WEGS, nami kwa kutambua jitihada zake katika jamii juu ya mtoto wa kike, nimetoa fursa kwa wasichana na wavulana wote wa kidato cha nne walioshiriki masomo ya stadi za maisha katika chuo changu, kujifunza lugha ya kingereza, mapishi, biashara na upambaji ili waongeze ujuzi na maarifa” ameeleza Mlay.

Mwanafunzi Peace Kaaya wa kidato cha nne kutoka Kikwe Sekondari aliyejinyakulia shilingi 120,000 amesema amepata mwanga na ameamini anaweza kusimamia mradi wake wa kufuga kuku wa kisasa aina ya SASO kutokana na maarifa na msingi aliojengewa na mradi wa Promote Potential for Adolescent Girls.

“Sikuwahi kufikiri kama inawezekana kutimiza ndoto zangu, kwa sababu ukifikiria mtaji, mtazamo wa jamii juu ya msichana lakini pia uelewa mdogo wa namna ya kujisimamia kimaisha ilikuwa kikwazo, baada ya mafunzo haya nimebadilisha mtazamo hata nikiendelea na masomo tayari nitakuwa na msingi wa jinsi gani nifanye nipige hatua” amefafanua Peace.

Vivyo hivyo Makamu Mkuu wa shule ya sekondari Nduruma Hamidu Abdul ameomba Mashirika na Taasisi mbalimbali kuiga mfano wa WEGS kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika mashindano, hali itakayoongeza chachu na kutambua umuhimu wa kile kinachofundishwa.

Hamidu anasema “kwa hakika stadi za maisha ni msingi wa maisha, natamani serikali ibadilishe mitaala na kurudisha masomo ya stadi za maisha kama ilivyokuwa zamani, kwa sababu hali ya sasa ya vijana kiujumla ni mbaya, unakuta kijana kasoma lakini akimaliza masomo hana cha kufanya, hatimaye anakata tamaa na kuilemea jamii, naipongeza WEGS imefanya kitu kizuri”.

Mwanafunzi Bryson Mollel kutoka Nduruma Sekondari, amesema atazingatia elimu ya stadi za maisha ili imfae baadae.

“Naomba mikakati ya kumuinua mtoto wa kike inapowekwa basi na sisi watoto wa kiume tukumbukwe vile vile.

October 11 kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike. inayokuja na Kaulimbiu mbalimbali zinazolenga kumuinua mtoto wa kike ambapo mwaka Jana ilisema “Haki Zetu ni Hatma Yetu: Wakati ni Sasa”