TANZANIA inapambana na rushwa kwa kuanzisha Divisheni ya Mahakama kuu – Chalamila.

Na Mwandishi wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kupambana na rushwa nchini (Takukuru), Crispin Chalamila amesema Serikali ya Tanzania imekuwa ikipambana na Rushwa kwa kuimarisha mifumo ya sheria na ya kitaasisi ikiwemo kuanzishwa kwa Divisheni ya Mahakama Kuu inayoshughulikia masuala ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Chalamila ameyasema hayo leo katika Jiji la Beijing China wakati akiwasilisha mada iliyojulikana kama ‘ANTI CORRUPTION AND INSTITUTIONAL LEGAL FRAME WORK IN TANZANIA’ kwa Wakuu wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa wanaoshiriki kwenye kongamano la 5 la Kimataifa linalohusu mapambano dhidi ya rushwa (‘The 5th Global Operational Network of Anti Corruption Law Enforcement Authorities – GlobE Network’).

Kongamano hilo ni mahususi kwa ajili ya Mamlaka za Kuzuia na Kupambana Rushwa Duniani kubadilishana uzoefu na utaalamu katika jukumu la kuzuia na kupambana na Rushwa.

Aidha kongamano hilo la siku tano, linahudhuriwa na Mamlaka 219 za Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka nchi 121 Duniani ikiwemo Tanzania ambapo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wanashiriki.

Pamoja na mambo mengine, Kongamano hilo linaelezaa kuhusisha Wakuu wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana Rushwa duniani kutoa uzoefu wao wa namna Serikali zinavyofanikiwa kudhibiti Rushwa katika mataifa yao.

Kupitia Warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Francis Chalamila ametoa uzoefu wa namna ambavyo Mfumo wa Sheria na Kitaasisi nchini Tanzania unawezesha Mapambano Dhidi ya Rushwa kufanikiwa.

Kongamano hili linahudhuriwa na Mamlaka 219 za Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka nchi 121 Duniani – Tanzania ikiwa ni kati ya Nchi 70 zilizopewa fursa ya kutoa wasilisho.

Mtandao wa GlobE ulianzishwa 2021 kwa lengo la kubadilishana taarifa, uzoefu na utaalamu katika mapambano dhidi ya Rushwa na TAKUKURU ilijiunga na Mtandao huu Mwaka 2022.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Crispin Francis Chalamila, amemtembelea Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Khamis Mussa Omar Septemba 23, 2024 kwa lengo la kujitambulisha.

Akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu, Balozi Omar ameipongeza TAKUKURU kwa jitihada inazozifanya katika kuzuia na kupambana na rushwa na kuisisitiza TAKUKURU kutumia vema fursa ya ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na ya China kwani kuna mambo mengi ya kujifunza.

Vilevile, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Chalamila ametumia mkutano huo kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa baadhi ya Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa wanaoshiriki Mkutano wa GlobE Network unaoendelea Jijini Beijing China kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya TAKUKURU na Mamlaka hizo.

Viongozi aliokutana nao ni kutoka National Commission of Supervision ya China Beijing (NCS), Independent Commission Against Corruption (ICAC) ya China Hong Kong na National Prosecutions Authority – (NPA) ya Afrika Kusini.

Mazungumzo ya Mkurugenzi Mkuu na viongozi hawa yamelenga maeneo yafuatayo Mafunzo ya uchunguzi, Ufuatiliaji na Urejeshwaji wa mali, Forensic Evidence, Intelijensia, Uzuiaji Rushwa, Uelimishaji umma, Vitendea kazi pamoja na Ziara za mafunzo

Kwa ujumla wake viongozi hao wamepongeza jitihada za TAKUKURU katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na ushirikiano walionao Kikanda na Kimataifa na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.