Na Seif Mangwangi, Arusha
BODI ya Mikopo ya elimu ya juu nchini (HESLB), imetenga Shilingi bilioni 787 kwaajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaosomea masomo ngazi ya shahada na stashahada katika fani mbambali nchini.
Akiwasilisha taarifa yake katika kikao kazi kilichokutanisha watendaji wa bodi hiyo wakiongozwa na Mtendaji wake Mkuu Dkt Bill Kiwia, a maafisa mikopo kutoka vyuo vyote vikuu nchini pamoja na vyuo vya kati leo jijini hapa, Mkurugenzi wa upangaji na utoaji wa mikopo katika bodi hiyo Dkt. Peter Mmari amesema kiasi hicho cha fedha kimetengwa kutumika kwaajili ya mwaka wa masomo 2024/2025, huku wanafunzi 252,000 wakitarajiwa kunufaika na mkopo huo.
Dkt Mmari amesema kati ya fedha hizo zilizotengwa bodi ya mikopo inatarajia kuwapatia mikopo wanafunzi 80,000 wa mwaka wa kwanza wanaoingia vyuoni wakisomea masomo ya shahada na stashahada na fedha zingine zitatolewa mkopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao.
Amesema katika mwaka wa masomo 2023/2024, bodi ya mikopo iliweza kupitisha lengo la kutoa mikopo kwa wanafunzi ambapo kwa msimu huo jumla ya wanafunzi 79200 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 12 walipatiwa mikopo.
“msimu uliopita tulitoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi ambapo lengu letu lilikuwa ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 75,000 pekee lakini walizidi hadi kufikia 79200 ikiwa ni ongezeko la asilimia 12, haya yote ni mafanikio ya serikali ya awamu ya sita,”amesema.
Amesema kupitia nia ya dhati ya Serikali ya awamu ya Sita, mwaka wa masomo 2022/2023 bodi ya mikopo ilianzisha mpango wa kutoa Scholarship kwa wanafunzi wa Diploma waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi inayojulikana kama STEM ambapo jumla ya wanafunzi 1200 wanafaidika na mfumo huo.
Dkt. Mmari amesema pamoja na mafaniko yote, kumekuwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni kucheleweshwa kwa matokeo ya wanafunzi baada ya kufanya mitihani yao, vyuo kuanzisha program mpya bila kuijulisha bodi ya mikopo na baadhi ya wanafunzi kufuata maelekezo ya maombi na kujikuta wakikosa mkopo.
“ Changamoto ni nyingi za wanafunzi kukosa mkopo lakini tunajitahidi kukabiliana nazo mfano wanafunzi wengi wamekuwa wakishindwa kujaza fomu za mikopo kwa kutoweka taarifa sahihi, kama bodi tumeanza kutoa elimu kwa wanafunzi lakini pia wale wate wanaokosa bado wana nafasi ya kuomba tena na kupata,”amesema.
Amesema kumekuwa na dhana potofu kuwa mwanafunzi akikosa mkopo mwaka wa kwanza hawezi kupata tena jambo ambalo sio kweli na kutoa wito kwa wanafunzi kuendelea kuomba mkopo kwa kuwa ni haki yao.
Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Dkt Bill Kiwia amesema katika kikao hicho mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo maboresho ya mfumo wa Tehama na kuondokana na mfumo wa makaratasi lengo likiwa ni kurahisisha utendaji kazi, pia watajadili mfumo wa malipo serikalini, mfumo wa maboresho kidijitali, mfumo wa urejeshwaji wa mikopo (repayment portal) na utaratibu wa malipo ya mkopo kupitia mfumo wa MUSE na mambo muhimu ya kuzingatia.