Vijana 500 Afrika wakutana Arusha kujadili changamoto ya umiliki Ardhi kwa vijana

Na Claud Gwandu, Arusha.

MKUTANO wa Kimataifa wa Vijana na Utawala wa Ardhi barani Afrika(CIGOFA) unaanza kesho jumatatu jijini hapa kujadili,pamoja na mengine,changamoto ya umiliki wa Ardhi kwa vijana barani humo.

Zaidi ya vijana 500 kutoka pande zote za bara hilo watashiriki katika mkutano huo wa nne utakaofanyika pia kwa njia ya Mtandao(Zoom).

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Vijana kwa ajili ya Ardhi barani Afrika(YILAA), Innocent Antoine Houedji amesema mada kuu katika mkutano wa mwaka huu ni Kuhakikisha Haki za Vijana katika Ardhi.

“CIGOFA 4 inalenga kuwawezesha vijana kwa kutoa jukwaa la mazungumzo,kubadilishana maarifa,na ushirikiano katika masuala muhimu yanayohusiana na haki za Ardhi kwa vijana

“Pia watajadili mabadiliko ya tabia nchi na vijana,na maendeleo endelevu,” amesisitiza Ofisa Mtendaji huyo Mkuu.

Mkutano huo utawahusisha washiriki kutoka sekta mbalilmbali, ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa serikali,mashirika ya kiraia,vijana,washirika wa maendeleo, wasomi na viongozi wa vijana.

Mratibu wa nchi zinazozungumza Kiingereza katika Jumuiya hiyo, Deborah Oyugi amesema pia mkutano huo utajadili nafasi ya mwanamke na mtoto wa kike katika umiliki wa Ardhi barani Afrika.

” Kutokana na maazimio yaliyotolewa katika mikutano mingine mitatu ya CIGOFA, tutajadil nafasi ya mwanamke na mtoto wa kike katika masuala ya umiliki wa Ardhi.

” Sasa hivi kundi hilo wanashirikishwa kwa kiasi fulani katika masuala ya Ardhi, lakini tunataka washirikishwe zaidi hadi katika ngazi ya maamuzi,” anasema Mratibu huyo.

Mratibu wa Jukwaa la Ardhi Tanzania, Bernard Baha amesema pamoja na jitihada mbalilmbali za kuwashirikisha vijana katika masuala ya Ardhi,bado elimu zaidi inahitajika ili waelewe haki katika umiliki wa Ardhi

Mwakilishi wa YILAA nchini Tanzania, Augustine Nyakatoma anasema kuwa hadi sasa hakuna utaratibu wa kisera nchini uliowekwa Kuhakikisha vijana wanamiliki Ardhi na kunufaika nayo.

“Tunataka kuwe na utaratibu wa kisera utakaosaidia kukuza uelewa wa vijana katika umiliki wa Ardhi,”anasisitiza.

Mkutano huo umeandaliwa kwa pamoja na YILAA kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika(AU),Shirika la Maendeleo la Ujerumani(GIZ) na Muungano wa Kimataifa wa Ardhi (ILC).

Washirika wengine waliofanikisha mkutano huo ni Mtandao wa Vijana wafanyao upimaji(FIG), LANDESA,Muungano wa Ardhi wa Tanzania na wadau wengine.