Mchango wa wanawake kutokomeza ujangili ushoroba wa kwakuchinja

Na Zulfa Mfinanga, APC Blog

Arusha.

Janeth Sanga, askari uhifadhi wa
Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) ambaye amekuwa
mstari wa mbele kukabiliana na uharibifu wa ushoroba wa Kwakuchinja. (Picha na Baraka Ndoto)
 

 

Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani zilizoridhia mkataba
wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) uliopitishwa na
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN Council) mwaka 1979.

Mkataba huu umewapa haki Wanawake kushiriki shughuli
mbalimbali ambazo awali zilionekana zinawafaa Wanaume pekee kama vile kupiga
kura, kupata elimu, afya pamoja na ajira.

Kufuatia mkataba huo, mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania
yamechukua hatua zote zinazofaa ikiwa ni pamoja na kutunga sera na sheria ili
wanawake waweze kufurahia haki zao za msingi na uhuru wa kushiriki katika
shughuli za maendeleo.

Janeth Sanga (36), Askari wa Wanyamapori wa Jumuiya ya
Uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) iliyopo Wilaya ya Babati Mkoani Manyara ni moja ya matokeo chanya ya mkataba huo hapa nchini.

Janeth ambae ni Mke na Mama wa Watoto watatu ni miongoni mwa wanawake saba waliopo katika kikosi kazi cha
askari 40 wa uhifadhi wa Burunge WMA inayolinda na kuendeleza viumbe pori
katika ushoroba wa Kwakuchinja.

Ushoroba wa Kwakuchinja ni sehemu
muhimu ya makazi na mapitio ya Wanyamapori kati ya hifadhi mbili za Taifa za
Tarangire na Ziwa Manyara.

Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise anasema ushoroba wa
Kwakuchinja wenye kilomita za mraba 283 ni miongoni mwa shoroba nchini Tanzania
ambazo zimeharibiwa zaidi na shughuli za binadamu ikiwemo ukataji wa miti na
uwindaji haramu wa viumbepori.

“Changamoto zinazoikabili Burunge WMA ni pamoja na ujangili
hasa ujangili wa kitoweo, migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, ongezeko la
makazi ya watu na shughuli za kibinadamu, mimea vamizi pamoja na miundombinu ya
barabara kuathiri mapitio ya Wanyama,” anasema Mwaise.

 

Wafugaji kuingiza mifugo yao ndani ya Jumuiya
ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Burunge imekuwa changamoto katika uhifadhi wa
ushoroba wa Kwakuchinja. Hali hii imekuwa ikichangia migogoro kati ya wafugaji
na askari wa uhifadhi wanyamapori.
(Picha na Zulfa Mfinanga)

Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania ina
jumla ya shoroba 61 ambapo 41 zipo hatarini kutoweka kutokana na kuvamiwa na
shughuli za kibinadamu huku shoroba 20 kati ya hizo zikiwa zimezibwa kabisa.

 

Kuanzishwa kwa Burunge WMA mwaka 2005 ndio ikawa mwanzo wa
kurejeshwa kwa maeneo yaliyoharibiwa, kazi ambayo inafanyika mpaka sasa.

Janeth pamoja na askari wenzake wamekuwa wakifanya doria,
misako na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa bioanuai
katika eneo hilo ili kupunguza uharibifu wa ushoroba huo.

“Doria tunazofanya ndani na nje ya hifadhi zinalenga
kudhibiti ujangili wa wanyama na mimea unaosababisha uharibifu wa rasilimali za
Taifa pamoja na uharibifu wa mazingira, lakini pia kukagua mipaka ya eneo
tengefu ili lisivamiwe,” anasema Janeth aliyeanza kazi hiyo mwaka 2006.

Umuhimu wa Wanawake katika Jeshi la
Uhifadhi

Janeth ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa kambi ya Burunge WMA
anasema mbali na kufanya doria za mara kwa mara ndani ya hifadhi lakini jukumu
kubwa ni kutoa elimu kwa jamii huasa wanawake wanaozunguka vijiji vya hifadhi
hiyo juu ya uhifadhi wa mazingira.

Janeth ni kiungo muhimu kati ya Wanawake na Jumuiya hiyo kwa
sababu kundi hilo limekuwa likitengwa katika maamuzi ya masuala yanayohusu
uhifadhi wa bioanuai.

“Jambo la kujivunia ni kuona Wanawake wameanza kubadilika
kupitia mimi, huwa nawaambia mimi ni Mwanamke kama ninyi, nahitaji nishati kwa
ajili ya kupikia, nahitaji fedha kwa ajili ya kuendesha maisha, lakini vyote
hivyo havijanifanya nivunje sheria za uhifadhi kwa kukata miti ama kushiriki
kwenye biashara ya kuuza ama kununua nyamapori,” anasema Janeth.

Janeth anasema Wanawake wamekuwa wakitumika zaidi kwenye
ujangili wa Wanyamapori kwa ajili ya kitoweo kwa kununua na kuuza kupitia
biashara ya mama lishe hivyo amekuwa akitembelea minada mbalimbali kwa ajili ya
kufanya doria pamoja na kutoa elimu kwa wanawake ili kukomesha biashara hiyo.

Sheria ya Uhifadhi namba 5 ya mwaka 2009  inaelekeza kwamba mtuhumiwa wa kike akamatwe
na askari wa kike na mtuhumiwa wa kiume akamatwe na askari wa kiume.

“Kazi hii naipenda ingawa ina changamoto zake kwamba
kuna baadhi ya watu hawatupendi lakini hao ni wale wasiopenda kutii sheria za
wanyamapori, lakini kwa upande mwingine kazi yangu inaendelea kuivutia
jamii,” anasema askari huyo.

 

Janeth Sanga akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) walipomtembelea katika kambi ya Burunge
WMA baada ya mafunzo ya kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni
ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
(Picha
na Baraka Ndoto).

Janeth Ameacha alama isiyofutika

Janeth anajivunia kuwashawishi Wanawake watano kuingia
katika shughuli za uhifadhi kutoka vijiji tofauti.

Anasema wote hao walikuwa wanamuuliza maswali mbalimbali ya
uhifadhi ikiwemo nafasi ya Mwanamke katika uhifadhi hivyo kupitia kwake
walishawishika zaidi na walipata sehemu ya kuanzia.

“Kuna dhana kwamba ukiajiriwa huwezi kutimiza majukumu
ya familia yako kama Mama, naomba niwatoe hofu, mimi nina zaidi ya miaka 10
kwenye hii kazi lakini familia yangu naihudumia ipasavyo na majukumu ya kazi
yanaenda vizuri kabisa,” anasema Janeth.

Askari huyo alikuwa akihojiwa hivi karibuni na Mwandishi wa
makala haya katika mafunzo ya vitendo ya kuripoti habari za bioanuai
yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Africa chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi
Maliasili. 

Monica Lugiriza (23) ni miongoni mwa askari watano
waliojiunga na Jeshi la Uhifadhi mwaka huu kwa ushawishi wa Janeth licha ya
kuwa tangu akiwa mdogo aliipenda kazi hiyo.

“Shauku yangu iliongezeka zaidi baada ya kumuona Janeth, na
nikiri kwamba hadi kufikia hapa leo kuna mchango wake mkubwa,” anasema Monica.

Monica anasema kile ambacho alikuwa akiwaza kabla ya
kujiunga na jeshi hilo ndicho alichokutana nacho ambacho ni kutoa elimu ya
uhifadhi wa maliasili kwa jamii na kulinda maeneo tengefu.

Familia na jamii yake inaendelea kumpa hamasa ya kufanya
kazi kwa bidii.

Kikosi kazi cha askari wa uhifadhi kimekuwa
nguzo muhimu ya kutokomeza ujangili na kuufanya ushoroba wa Kwakuchinja kuanza
kuwa kivutio cha wanyamapori na watalii.
(Picha na Baraka Ndoto).

Askari wanawake wanavyotambuliwa
katika uhifadhi

Kikosi kazi cha kukabiliana na ujangili chenye askari 40
kimeundwa na taasisi nne za Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), shirika
lisilo kuwa la Serikali la Chem Chem Association, Burunge WMA na Halmashauri ya
Wilaya ya Babati.

Meneja Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kutoka Chem Chem
Association, Martin Mung’ong’o anasema kwa kushirikiana na taasisi hizo nne
wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja ya kutoa elimu, kufanya doria na kuhakikisha
watuhumiwa wa ujangili wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

Mung’ong’o anasema mafanikio ya kikosi kazi hicho
yamechangiwa na askari wanawake akiwemo Janeth ambao wamekuwa wakifanya kazi
nzuri hasa kuwabaini na kuwakamata wanawake wanaojihusisha na ujangili.

“Wateja wakubwa wa biashara ya nyamapori ni wanawake wa
majumbani pamoja na Mama lishe. Kuwatumia askari wetu hususani askari wanawake
tumefanikiwa kuwatia nguvuni baadhi ya wanunuzi na wauzaji, na hadi sasa
biashara hii inaendelea kukoma kabisa,” anasema Mung’ong’o. 

Mahema yanayotumiwa na askari na wanyamapori wa Burunge WMA
katika moja ya kambi zao wanazotumia kupanga mikakati ya namna ya kukabiliana
na majangili. 
(Picha na Baraka Ndoto)

Sera ya Wanyamapori ya Tanzania ya mwaka 2007 inaitaka
Serikali na wadau wa uhifadhi kulinda shoroba za wanyamapori, njia za uhamaji,
maeneo ya usalama wa wanyama, na kuhakikisha kwamba jamii zilizo katika maeneo
hayo ya wanyama zinafaidika vilivyo kutokana na uhifadhi wanyamapori.

Mtaalamu wa masuala ya bioanuai na Mhadhiri Msaidizi kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Angelmercy Baltazary anasema lengo la kuhamasisha
wanawake wengi kuingia katika uhifadhi ni kuweka usawa wa jinsi zote kushiriki
katika utunzaji wa bioanuia.

“Makundi yote kwa maana ya wanawake, vijana na watu
wenye ulemavu wana mchango mkubwa sana katika utunzaji wa mazingira kwani
wasiposhirikishwa itasababisha kukosa haki juu ya ardhi yao ikiwemo uwakilishi
mdogo katika maamuzi ya maliasili na uongozi,” anasema mtaalam huyo.

Angelmercy aliyekuwa akizungumza katika mafunzo ya siku tatu
ya kuripoti habari za bioanuai kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na
kampuni ya Nukta Afrika chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili
anasema  wanawake washirikishwe katika
ngazi zote za maamuzi ili kutoa mchango utakaosaidia kuimarisha shughuli za
uhifadhi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoingia na
zinazotekeleza Mkataba wa Lusaka wa kukabiliana na ujangili na usafirishaji
haramu wa mazao ya wanyama na mimea ndani na nje ya bara hilo (Lusaka Agreement
Task Force-LATF) ulioanzishwa mwaka 1994.

Kufuatia mkataba huo, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele
kwa uhifadhi wa rasilimali za misitu na wanyamapori kwa kuimarisha ulinzi na
nidhamu kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuanzisha Jeshi Usu la Uhifadhi (JU)
mwaka 2018.

Ramani
inanyoonyesha eneo la hifadhi ya Burunge WMA pamoja na maeneo ambayo imepakana
nayo
(Picha kwa hisani ya Google earth)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki aliyekuwa
akizungumza katika Kongamano la kwanza 
la kitaifa la kujadili usimamizi wa shoroba Disemba 14, 2023 jijini Dar
es Salaam alisema wizara yake itaendelea kushirikisha wadau na makundi
mbalimbali kwenye jamii ili kuokoa shoroba zisiharibiwe.