Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwa wamechanganyikana na wanafunzi wa kawaida ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sera ya Elimu Jumuish |
Jumatano Desemba 20, 2023
Na Abby Nkungu, Singida
UANDIKISHAJI wanafunzi wa darasa la kwanza kwa watoto wenye mahitaji maalumu Manispaa ya Singida, umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 7 kwa kipindi cha mwaka mmoja hali inayoonesha jamii imeanza kutambua na kuelewa umuhimu wa elimu kwa kundi hilo.
Takwimu za idara ya elimu katika Manispaa hiyo zinaonesha kuwa, kiwango cha uandikishaji darasa la kwanza kwa watoto wenye mahitaji maalumu kimeongezeka kutoka wanafunzi 66 mwaka 2022 hadi kufikia 71 mwaka huu ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 7.5 tu.
“Zipo sababu nyingi za mafanikio haya ya uandikishaji lakini kubwa zaidi ni matokeo chanya ya Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) iliyoanza kutekelezwa Januari 2021” alisema Mwl Omary Maje, Ofisa elimu katika Manispaa ya Singida.
Alisema, kutokana na Programu hiyo kujihusisha na maeneo yote matano ya mfumo wa Malezi Jumuishi kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8; ambayo ni Afya bora, Lishe, Malezi yenye mwitikio, Fursa za ujifunzaji wa Awali na Ulinzi na Usalama; hivyo hamasa na elimu inayotolewa kwa wazazi na walezi imeibua ari kwa jamii kusomesha watoto hao kwa hiari.
“Kwa mwelekeo ninaouona na kazi kubwa iliyofanywa na Programu hii, nina imani kubwa ka uandikishaji wa watoto hao utaongezeka zaidi mwaka ujao 2024. Ndio maana sisi pia tumeweka mikakati madhubuti ya kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa ajili ya watoto hao” alieleza.
Mwl Maje anakiri kuwa katika shule za msingi ambazo zinatekeleza mfumo wa Elimu Jumuishi ambapo watoto wenye mahitaji maalumu wanasoma na wenzao wa kawaida, bado kuna uhaba mkubwa wa vifaa na zana za kufundishia na kujifunzia: hali inayoleta ugumu katika ufundishaji na ujifunzaji darasani.
“Pamoja na kushughulikia upatikanaji wa vifaa na zana hizo, kwa upande wa walimu tumejipanga kuanzisha programu ya kujengeana uwezo katika fani zote za elimu maalumu; hususan kwenye ujuzi wa lugha ya alama na kutumia maandishi ya nukta nundu kuandika na kuyasoma ili kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu wenye taaluma ya kufundisha watoto hao” alisema
Alieleza kuwa hatua hiyo itakwenda pamoja na kufanya zoezi la kufuatilia mtaa kwa mtaa kwa kushirikiana na wenyeviti, mabalozi na mamlaka nyingine ili kuwatambua watoto wenye ulemavu na kuhakikisha wanaandikishwa. Piia, kuchukua hatua kwa wazazi na walezi wenye tabia ya kuwaficha wenye ulemavu wasisome.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Tumaini Viziwi ya mjini Singida, Francis Edward anasema pamoja na kuchukua hatua za kisheria, cha msingi ni kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wazazi na walezi juu ya umuhimu wa kusomesha watoto wenye mahitaji maalumu badala ya kuwafungia ndani.
“Zamani, baadhi ya wazazi na walezi walikuwa wakiwaficha majumbani watoto wao wenye mahitaji maalumu ili wasiende shule na hata tunapowapata walikuwa tayari wamevuka umri wa kuanza shule kwani wanakuwa na miaka 10 hadi 15. Kwa sasa tunaandikisha walio kwenye umri lengwa yaani miaka 5 na 6” alisema kisha akafafanua kuwa hiyo yote imetokana na jamii kuanza kupata uelewa juu ya umuhimu wa elimu kwa wenye ulemavu.
Baadhi ya wazazi na walezi wanaunga mkono kauli hiyo ya mwalimu Francis wakisema hakuna mwarobaini mwingine wa kumaliza changamoto hiyo zaidi ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kutumia sheria ndogo zilizopo na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia watoto hao.
“Tuendelee kuwaelimisha na kutumia sheria ndogo zilizopo kuwabana wazazi na walezi wakorofi wachache wasiopenda kusomesha watoto wao wenye mahitaji maalumu. Kwa maoni yangu, pia Serikali iwekeze zaidi kwenye kuboresha miundombinu, vifaa na zana kwenye shule zinazopokea watoto hawa kwani wanateseka mno” alisema Daudi Bura mkazi wa Kibaoni, Singida mjini.
Bura anashauri kuwa ni muhimu shule zinazotoa elimu Jumuishi kuwa na vyoo maalumu kwa watoto wenye ulemavu na miundombinu mingine rafiki, miwani kwa wenye uoni hafifu, wataalamu wa lugha ya alama na nukta nundu ili kuwawezesha kusoma bila kikwazo.
Mzazi mwingine, Raheli Ramadhani mkazi wa Ginnery Singida mjini anasema mazingira rafiki kwenye shule hizo yatavutia wazazi na walezi kupeleka watoto wao bila Serikali kulazimika kutumia nguvu.
Ingawa wadau wanasema changamoto bado ni kubwa katika utekelezaji wake, Sera ya Elimu Jumuishi ya mwaka 2014 inataka watoto wenye ulemavu, wenye mahitaji maalumu na walio kwenye mazingira magumu kusoma pamoja na wenzao wa kawaida kwenye shule moja bila kubaguliwa ili kumwezesha kila mtoto wa Kitanzania kupata haki ya elimu bila kikwazo chochote.