*TBL yaibuka kidedea ikifuatiwa na TCC
Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan, amelipongeza Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) kwa namna namna linavyokuwa mwaka hadi mwaka na kuboresha tuzo za wenye viwanda ambazo zimetimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake.
Aliyasema hayo jana usiku kwenye ukumbi wa The Super DOM Masaki wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa wenye viwanda waliofanya vizuri iitwayo President Manufacturer of the Year (PMAYA), ambazo huandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI).
Kwenye shindano hilo ambalo mdhamini mkuu alikuwa benki ya NBC, mshindi wa jumla kwenye tuzo hizo alikuwa Tanzania Breweries TBL akifuatiwa na Tanzania Cigarette Public Company (TCC) na kampuni ya Totalenergies Marketing Tanzania.
Alisema tofauti na jumuiya nyingi ambazo huanzishwa na kufa CTI imeendelea kuwa imara mwaka hadi mwaka na kuipongeza kwa kuendelea kutoa na kuboresha tuzo za PMAYA huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kushirikisha na shirikisho hilo kuhakikisha vikwazo vyote vya wenye viwanda vinapatiwa majibu.
Alisema CTI aliyoiona wakati akiwa Makamu wa Rais ni tofauti nay a sasa kwani inaonekana kukomaa zaidi na kufanya mambo makubwa ambayo yamekuwa msaada kwa wenye viwanda.
“Kuna jumuiya nyingi tu zinaanzishwa lakini hazifiki mbali zinakufa, lakini CTI tangu ianzishwe imesimama imara na inazidi kuwa imara siku hadi siku ikisimamia maslahi ya wenye viwanda vizuri,” alisema
Aidha, aliipongeza CTI kwa kuendelea kutoa tuzo hizo kwa muda wa miaka 17 na aliahidi kuwa serikali itaendelea kushirikisha na shirikisho hilo kuhakikisha vikwazo vyote vya wenye viwanda vinapatiwa majibu.
Alisema mwezi Januari utawashwa mtambo mmoja kuanza kuzalisha umeme na kisha mwezi wanne utawashwa mtambo mwingine hali itakayosaidia kupatikana umeme wa kutosha na kuondoa malalamiko ya uhaba wa nishati hiyo.
“Ile mitambo iko tisa, sasa kwa kuanzia itawashwa mitambo miwili ambayo itasaidia sana kuongeza kiwango cha umeme hapa nchini na kupunguza malalamiko ya upungufu wa nishati hiyo,” alisema
Alisema ingawa takwimu duniani zinaonyesha kwamba sekta ya viwanda ilidorora miaka miwili iliyopita lakini kwa Tanzania inaonyesha kwamba inakuwa hata kama si kwa kiwango kikubwa.
“Takwimu zinaonyesha tunakwenda vizuri sana kwenye sekta ya viwanda ila kama kuna changamoto sasa ni kuchukua hatua za haraka kuzitatua ili twende kwa kasi zaidi,” alisema
Aidha, Rais Samia alisema lazima jitihada zifanyike kuondoa utegemezi kwa wenye viwanda nchini kutegemea malighafi kutoka nje ya nchi na badala yake wawe wanatumia malighafi zinazopatikana hapa nchini.
Alisema iwapo viwanda vitaondokana na utegemezi huo vitazalisha bidhaa nyingi na ambazo zitauzwa kwa bei nafuu kwenye masoko ya ndani na yale ya kimataifa hivyo kusaidia kupata fedha za kigeni.
Rais Samia alisema amefurahishwa kusikia kuwa kuna kiwanda cha kuunganisha magari Mkuranga mkoani Pwani ambacho kimekuwa kikitumia malighafi kutoka Tanzania.
Akizungumzia uhaba wa dola za Marekani, Rais Samia alisema kwa Tanzania hali ni nzuri kulinganisha na mataifa ya jirani na aliwaomba wenye viwanda kusaidia kuzalisha bidhaa nyingi na kuuza nje ya nchi ili kupata fedha nyingi za kigeni.
Alisema serikali imeendelea kuongeza kiwango cha wafanyabiashara nchini kutoa Dola za Marekani kwa siku kutoka dola 500, 000 kwa siku hadi kufikia dola 2,00,000 kwa siku.
“Ukilinganisha na wenzetu sisi tuna ahueni kidogo kwasababu tulianza na kikomo cha dola 500,000 kwa siku tukaenda dola 1,000,000 na sasa ni dola 2,000,000 kwa siku sasa kuna majirani zetu hata kutoa dola 500,000 kwa siku hawaruhusu,” alisema
Alisema serikali imechukua hatua kadhaa za kulinda hifadhi ya dola zilizopo nchini ikiwemo kupunguza manunuzi ya bidhaa nje ya nchi na imeingia kwenye kilimo cha mazao ya haraka haraka yatakayouzwa nje ya nchi na kupata fedha za kigeni.
“CTI na wanachama wenu mnaweza kutusaidia sana kupunguza tatizo la uhaba wa dola kwa kuzalisha bidhaa nyingi sana na kuziuza nje ya nchi ili kupata fedha nyingi za kigeni,” alisema Rais Samia
Alisema mwakani Tanzania itakuwa inajitosheleza kwa sukari na itauza ziadaa nje ya nchi.