Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004, inasema ni kosa kuajiri watoto kinyume na sheria na adhabu hutolewa chini ya kifungu cha 102 (2) ambacho kinampa Hakimu wa Wilaya na Mkazi kutoa adhabu sawa na faini isiyozidi shilingi milioni 5 au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa wakati mmoja kwa jinsi mahakama itakavyoona kulingana na mazingira ya kesi yenyewe.
Hata hivyo Sheria ya mtoto katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi zote zinakataza mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 kuajiriwa kufanya kazi ngumu katika maeneo ya migodi, viwanda, au mabaharia katika meli na kazi nyingine yeyote inayotambulika kama hatarishi.
Wazazi na walezi wanatakiwa kuzingatia wajibu wa kuwapa watoto wao malezi bora yatakayowawezesha kuwa watu wema katika jamii, kuwa wenye maono na mtazamo chanya kwa kesho waitakayo, ikianzia mtoto anapokuwa tumboni mwa mama mpaka kufikia umri wa kujitegemea.
Wazazi wote wawili wanahusika katika uwajibikaji na ukamilifu wa malezi ya watoto yanayoweza kugawanywa katika sehemu mbili ambayo ni malezi ya kimwili na malezi ya kimaadili.
Kifungu cha 4 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2004 kinamuelezea mtoto kama mtu mwenye umri chini ya miaka 14 isipokuwa kwa ajira zilizo katika sekta hatarishi mtoto maana yake ni mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18.
Hata hivyo, sheria inaruhusu ajira kwa watoto wa miaka 14 katika kazi nyepesi ambazo sio hatarishi kwa afya ya watoto na maendeleo, isiyokinzana na mahudhurio shuleni na ustawi wao kwa ujumla.
Katika Jiji la Arusha Sheria hizo zinaendelea kuvunjwa hadharani, kwa kuwatumikisha watoto kubeba mizigo katika masoko ya Kilombero, Samunge na Soko Kuu.
Kwa muda mrefu wafanyabiasha na wanunuzi katika masoko hayo wamekuwa wakiwatumikisha watoto kubeba mizigo mizito na kuwalipa ujira mdogo, hayo yote yakifanyika muda ambao watoto hao walitakiwa kuwa shule ili kupata haki yao ya elimu.
Mashuhuda waliozungumza na chombo hiki wamebainisha jinsi watoto hao wanavyobebeshwa na kupakua mizigo katika magari makubwa katika masoko pamoja na kufanywa walinzi wa magari ya wanunuzi pindi wanapoingia sokoni kufanya mahemezi, huku wakilipwa ujira mdogo kuanzia shilingi mia mbili hadi shilingi mia tano, hatua hii ikipelekea kuwaathiri kisaikolojia watoto hao.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Watoto (UNICEF) limeripoti kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaotumikishwa kwa kazi mbalimbali ambapo watoto milioni 160 wanatumikishwa.
Mama Chambua anayefanya biashara za mbogamboga katika soko la Kilombero Jijini Arusha, amebainisha uwepo wa kundi kubwa la watoto wenye umri kuanzia miaka 7 na kuendelea, wanaofanya kazi za kubeba mizigo ya wateja kutoka sokoni kwenda kwenda Stendi au kwenye magari yao binafsi pamoja na kupakua mizigo kwenye magari makubwa kuingia sokoni.
Amesema idadi ya watoto wanaobeba mizigo katika soko la Kilombero inaongezeka kila kukicha ikichangiwa na wazazi na walezi kutowajibika ipasavyo kutunza na kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi kama chakula, mavazi na malazi.
“Sheria kali zikiwekwa na kusimamiwa ipasavyo, utumikishwaji kwa watoto sokoni unaweza kukomeshwa, mfano miezi michache iliyopita uongozi wa soko hili ulikuwa ukitoa tangazo asubuhi na mchana kwamba watoto wasipewe kazi za kubeba mizigo na watu walizingatia, kwa sababu iliwekwa adhabu kali kwa watakaobainika wakiwatumikisha watoto sokoni hapa…..ukatili huu uliisha lakini leo hii watoto wamerudi upya kwa sababu sheria imelegalega tena” ameeleza Mama Chambua.
Mama Chambua amefafanua jinsi wanaume wamekuwa wakiwaachia majukumu ya kulea familia akina mama peke yao, hatua inayochangia watoto kuamua kutafuta riziki yao sokoni na maeneo mengine ili kutunza familia zao.
“Ninashuhudia kila siku watoto hawa wakinunua mahitaji ya nyumbani ikiwemo mchele, mafuta, sukari na sabuni, na hata akiba ya pesa kuwapelekea wazazi wao, kwa hali hii mzazi anawezaje kumzuia mtoto asifanye shughuli hizi? pia mtoto atakubali kwenda shule badala akatafute riziki ili ashibe? Serikali kwa jicho la pekee inatakiwa kufanya kazi kubwa kuhakikisha vitendo hivi vinakomeshwa” ametoa ombi Mama Chambua.
Mama mmoja ambaye hakutaka jina lake kutajwa, amesema watoto hao licha ya kufanya kazi za kubeba mizigo na kupakua, wamekuwa wakifanya udokozi katika magari ya wateja wanaopaki kando ya soko kwa ajili ya kufanya manunuzi.
“Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wateja wengi kwamba watoto hawa wamekuwa wakifanya udokozi katika magari pale wanapoachiwa kuyalinda ili wapate ujira, iwapo mteja huyo atajisahahu kufunga milango sawasawa watoto hudokoa na kutokomea” amesema na kuongeza,
“Si hivyo tu bali kuna kesi nyingi za wateja wetu kipindi cha sikukuu, baadhi ya watoto hukimbia na mizigo ya wanunuzi na kutokomea pasipojulikana, hii hatua ni mbaya maana wanajifunza wizi na wanakomaa kwa tabia za uporaji, nashauri wazazi katika jamii wawajibike kutekeleza majukumu kwa watoto wao” ameeleza mama huyo.
Mwenyekiti wa soko la Kilombero (Na.68) Bakari Mwalim amekiri kuwepo kwa kundi kubwa la watoto wanaobeba na kupakua mizigo sokoni hapo, na ksema kwamba mwarobaini wa kukomesha vitendo hivyo unaandaliwa licha ya vikwazo vilivyopo vinavyochangiwa na wazazi wengi kudai hali ya usalama ni mdogo mitaani kutokana na matukio ya wizi na ukatili wa watoto hatua inayopelekea wazazi kuambatana na watoto wao muda wote wawapo sokoni.
Aidha Bakar ameitaka jamii nzima kushirikiana bega kwa bega kukomesha tabia ya kuwatumikisha watoto maeneo yote yenye mikusanyiko kama stendi, viwandani na sokoni, kwamba kila mmoja abebe uzito na kuwaza juu ya kesho ya kundi hili la watoto ambao huwajibika kutunza familia wakiwa katika umri mdogo.
“Naahidi kushirikiana na Uongozi wa Ofisi ya Kata ya Levolosi na viongozi wengine ili kuondoa taswira mbaya katika soko letu, kipekee inaniumiza akili kuona watoto wadogo wanashinda sokoni badala ya kwenda shule, kila mmoja avae uhusika wa kutoa elimu katika jamii juu ya madhara ya watoto kuzurura mitaani ambayo kwa asilimia kubwa yanachangia ukatili wa kijinsia kwa watoto hao” amesema,
“Nitoe wito hasa kwa wanaume, acheni kuwaza pombe badala ya kulea na kuangalia familia zenu, unakuta baba anakunywa pombe tangu asubuhi mpaka usiku, atapata wapi muda wa kuzungumza na watoto? wazazi jitafakarini na kukumbuka kuwa ukimtunza mtoto leo, atakutunza kesho” amesema Bakar.
Jitihada za kumpata Mkuu wa Soko la Kilombero ili atoe ufafanuzi kwa nini wamefumbia macho suala hili na nini mpango wao wa kumaliza tatizo la utumikishwaji wa watoto katika soko la Kilombero ziligonga mwamba baada ya Mtu mmoja aliyekuwa Ofisini kwa Mkuu wa Soko hilo ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake na alitoa maneno haya na kuhoji.
“Wewe ni nani? Umetoka chombo gani na Kitambulisho chako cha kazi kiko wapi? Siko tayari kuzungumza chochote na utaratibu hauniruhusu, kwa hiyo unaweza kwenda….kwanza utaratibu unanikataza kuzungumza na yeyote kama hana kitambulisho cha kazi, kwa hiyo siko tayari kuzungumza unaweza kuondoka” alisema mtu huyo.
Gazeti la Jamhuri liliwahi kuripoti vitendo vya ukiukwaji haki za watoto katika masoko ya Jiji la Arusha, hali ilitulia baada ya Mkuu wa wilaya ya Arusha kutoa onyo kali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika soko la Samunge Jovin Zawadi mwenye umri wa miaka Tisa (siyo jina lake halisi) alieleza namna ambavyo amekuwa akijipatia fedha kutokana na kubeba mizigo, ilimradi apate chakula walau milo miwili kwa siku.
Ameeleza namna anavyopitia wakati mgumu vipindi vya mvua kutokana na baridi pamoja na tope huku akielezea kudhulumiwa kwa kutolipwa ujira wake sawasawa na baadhi wateja baada ya kufikisha mizigo yao eneo husika.
“Nina wazazi wote wawili ni mtoto wa tatu kati ya watoto wanne, nilianza shule ya msingi lakini baada ya miezi sita niliacha shule kutokana kila nikirudi nilikuta hakuna chakula nyumbani, hivyo nilishinda njaa pamoja na kaka zangu, ndipo kaka yangu aitwaye James (sio jina halisi) alishauri tuanze kwenda soko la Samunge kubeba mizigo, tulianza kazi hiyo na sasa huu ni mwaka wa tatu, kaka zangu wanafanya kazi hiyo katika soko la Kilombero na mimi nimebaki hapa Samunge”,
“Natamani kurudi shule, naumia kila nikiona wenzangu wamevalia sare za shule, lakini najua siwezi tena kusoma kwa sababu wazazi wangu ni walevi na hawajali kuhusu malezi yetu, inatuumiza sana, sasa ndio tunalea familia kwa maana ya kupeleka chakula na kumnunulia nguo mdogo wetu wa kike aitwaye Emma ( jina limefichwa), kwa sasa tuna nafuu ya maisha tofauti na kipindi cha nyuma” ameeleza Jovin.
Wateja wanena
“Nimezoea kila nikija sokoni kununua bidhaa watoto hawa hunisaidia kubeba mizigo kupeleka kwenye gari na kuwapa kitu kidogo (ujira), kwa upande wangu sioni kama ni tatizo kwani hawafanyi kazi bure nawalipa”alieleza na kuongeza,
“Wazazi wanatakiwa kuwajibika kulea na kutunza watoto wao, licha ya baadhi ya wazazi kufurahia kupelekewa zawadi, ikumbukwe kuwa ni hatari zaidi maana idadi kubwa ya watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili ni wale wasiokuwa na uangalizi wa kutosha” ameeleza Mama Focus.
Said Hussein anaeleza” Unajua kwa dunia ya sasa maisha yamebadilika mno, hakuna jinsi inabidi tukubaliane na hali, kwamba wazazi wanazaa hawataki kulea watoto, na pia kuna watoto hawataki kutulia nyumbani kuwasikiliza wazazi wao, kama mtoto atafanya kazi sokoni akawa na akili basi anaweza kutimiza malengo yake, kikubwa asijiingize katika makundi mabaya, ni kweli kwamba kuna wanaofanikiwa kupitia hapa bila kupata elimu ya shule” anaendelea kufafanua,
Ingawa haikubaliki moja kwa moja kwamba watoto katika umri mdogo watumikishwe katika kazi ngumu badala ya kwenda shule kupata haki ya elimu, lakini sisi jamii na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali tuna wajibu kuwalea watoto hawa na kuwakanya, hata kama sio wako msaidie kumrudisha shule ili tuandae kizazi bora kwa taifa la kesho” amefafanua Hussein.
Takwimu kutoka Wizara ya Kazi na Ajira za mwaka 2020 zinaonyesha asilimia 18.7 ya watoto wenye umri kuanzia miaka 5 hadi 17 bado wanatumikishwa katika ajira hatarishi nchini licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali za kudhibiti vitendo hivyo.