Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Wakala wa Misitu Nchini TFS wamehimizwa kuimarisha ushirikiano wao na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi ya misitu nchini kote ili kwa pamoja waweze kulinda na kusaidiana kuibua vitendo vya ujangili.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano mkuu wa mwaka 2024 wa Makamanda na Viongozi mbalimbali wa TFS, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba, amesema maelekezo ya Wizara ni kuhakikisha hakuna migogoro kati ya Wananchi na Wahifadhi wa misitu ili kwa pamoja waweze kushirikiana kukuza uchumi wa taifa kupitia misitu.
Aidha amesema kwamba, iwapo migogoro itahusisha Wizara nyingine, Wizara yake itakuwa tayari kuweka msukumo wa kumaliza migogoro hiyo ili wananchi wajenge imani na TFS.
“Ikumbukwe kuwa, Wahifadhi mnayajua maeneo ya hifadhi kwa nadharia na taaluma lakini jamii inayajua maeneo yale kwa asili kutokana na kutumia mazingira hayo kwa muda wote wa maisha yao, nawakumbusha kuzingatia utendaji unaofuata sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi wa misitu nchini” amesema Kamishna Wakulyamba.
Hata hivyo amefafanua kuwa, TFS ipo kwenye maboresho kutoka katika utendaji wa Kiraia kwenda Kijeshi, kwamba watumishi wote watatakiwa kuzingatia mila na desturi zake, ambazo misingi yake ni nidhamu, uadilifu maisha na misingi ya Kiaskari.
“Simamieni vizuri maeneo yenu ya uzalishaji, pingeni rushwa na mtakaporudi katika maeneo yenu ya kazi jikumbusheni kila wakati mambo haya muhimu mliyojifunza katika Mkutano huu” Amesisitiza Kamishna Wakulyamba.
Kwa upande wake Kamishna wa Wakala wa Misitu Nchini Profesa Dos Santos Silayo ameeleza matarajio yao kuhusu mkutano wa tatu wa TFS, namna utakavyoleta mabadiliko na matokeo chanya kutokana na kubadilishana uzoefu, mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili na kujengeana uwezo.
“Katika mkutano huu tumepata nafasi ya kukutana na watoa mada na wabobezi katika masuala ya sheria, uchumi na mambo mengine mengi, hii ni fulsa mhimu kwetu na ya mabadiliko ya kufikia uchumi tunaoutarajia” amesema Profesa Dos Santos.
Katika namna hiyo hiyo, Naibu Kamishna wa Huduma za Hifadhi Misitu Saidizi Emmanuel Kiboko, amebainisha jinsi TFS imekuwa na utaratibu wa kuandaa motisha kwa watumishi, kuwajengea uwezo kazini, uwepo wa vitendea kazi vya kutosha, upandishwaji madaraja na malipo ya posho mbalimbali katika kuhakikisha watumishi wanakuwa na motisha ya kutekeleza majukumu yao.
Mkutano huo umeendana na ugawaji tuzo kwa Vituo na Watumishi waliofanya vizuri katika maeneo haya; usimamizi wa rasilimali za misitu, usimamizi wa rasilimali za nyuki, makusanyo ya maduhuri, usmamizi wa utalii, ikolojia na malikale pamoja na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.
Hatahivyo tuzo zaidi ya kumi zilizotolewa kwa vituo a Watumishi mbalimbali wa Wakala wa Misitu Nchini TFS, Mshindi wa kwanza ametoka katika Hifadhi ya Misitu ya Kanda ya Ziwa aliyeibuka kidedea katika ugawaji wa miche ya miti zaidi ya milioni 10 katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, wakati huo tuzo ya pili ya ngao ikienda Kanda ya Kati Dodoma kwa usimamizi wa rasilimali nyuki ambao wamevuna asali kilogramu 8259.2 sawa na wastani wa kilogramu 8 kwa mzinga mmoja.