Egidia Vedasto
APC Media, Arusha
Wananchi jijini arusha wametakiwa kuwa na imani na serikali yao, kwani inaendelea kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa vyumba vya madarasa, kujenga na kuboresha vituo vya afya na mambo mengine mengi yanayofanana na hayo.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini arusha Mstahiki Meya Maxmillian Iranqhe amesema baraza la madiwani lililofanyika Nov 6 jijini arusha, limeazimia manunuzi ya greda na mitambo kwa ajili ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara na mitalo inayoendelea, ambapo imetengwa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya manunuzi ya mitambo tajwa.
Aidha ameongeza kuwa, baraza limeelekeza utoaji wa vibali vya ujenzi unaozingatia sheria pamoja na maendeleo ya mji, sehemu ya jiji ambayo ina mitaa kuu ya biashara na majengo makuu ya umma ikijumuishwa na viwanda, makazi, biashara, utawala na matumizi (CBD).
“Baraza la madiwani limeazimia upangaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza, uzingatie umbali na urahisi wa usafiri ili kupunguza adha kwa wanafunzi na kuboresha kiwango cha elimu na ufaulu, miradi ya ujenzi wa madarasa kukamilika kwa wakati, sambamba na ujenzi wa vivuko ili kuunganisha mitaa ya jiji na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla” amesema Iranqhe.
Hata hivyo amesema baraza limeelekeza uitishwe mkutano wa dharura wa baraza la madiwani kwa kuwashirikisha TARURA TANROADs na AUWSA ili kujadili kwa kina changamoto ya barabara kwenye mitaa ya jiji la arusha.
Vile vile amewakumbusha wananchi kuendelea kupanda miti, kufanya usafi katika maeneo yao, wadau wa maendeleo kuendelea kufunga taa walau mbili mbele ya ofisi au makazi yao na kupamba mji kwa miti ya krismas msimu huu wa sikukuu.