Fiti watakiwa kusimamia maadili

 FITI WATAKIWA KUSIMAMIA MAADILI

Na Anangisye Mwateba-Moshi

Watumishi wa Chuo Cha Viwanda vya Misitu (FITI) wametakiwa kusimamia misingi ya maadili, miongozo na taratibu za kiutumishi ili wawe  watumishi bora wenye kuleta tija katika chuo hicho.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa akiongea na watumishi wa chuo hicho kilichopo katika Manispaa ya Mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mhe. Kitandula amewaasa watumishi hao kuacha kutamani mafanikio ya haraka na badala yake kuwa chachu au sehemu ya mafanikio yatakayopatikana chuoni hapo.

Amewapongeza watumishi hao waliokitumikia chuo hicho kwa muda mrefu kwa sababu wamekilea na kukitunza chuo hicho.

Mheshimiwa Kitandula pia ameutaka uongozi wa chuo hicho kutumia changamoto walizokuwa nazo kama fursa ya kujiletea maboresho katika kutengeneza wataalamu na  utafutaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa katika chuo hicho.

“Wizara ya Maliasili na Utalii iko kwenye mkakati wa  kuboresha vyuo vyake vyote ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi, maslahi, utendaji wa kazi na kutoa wahitimu bora wanaoweza kuingia kwenye soko la ajira iwe kwa kujiajiri au kuajiriwa” aliongeza Mhe. Kitandula.

Mhe. Kitandula pia aliutaka uongozi wa chuo hicho kuanza kufukiria namna ya kutumia akili bandia(artificial intelligence) katika kuendesha shughuli zake maana kwa dunia ya sasa mambo yamebadilika hivyo vyema mtazamo wa chuo ukaendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Awali, akimkaribisha Naibu Waziri, Mkurugenzi wa Idara ya utafiti na Mafunzo, Dkt. Edward Kohi ameutaka uongozi wa chuo hicho kutengeneza mkakati wa kujiendesha ili kuzalisha pato la taifa lakini pia kiweze kujiendesha chenyewe.