Na Seif Mangwangi, Arusha
ELIMU ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari katika jamii ndio dawa peke inayoweza kuchangia katika kujenga jamii yenye habari sahihi, demokrasia imara, na haki za binadamu zinazoheshimiwa na hivyo kujenga taifa, lenye umoja, mshikamano na amani, mambo muhimu katika kuleta maendeleo katika nchi.
Hayo yameelezwa leo Novemba 2,2023 na Rais wa UTPC Deo Nsokolo katika hotuba yake ya ufunguzi wa mjadala wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kukomesha Uhalifu Dhidi ya Waandishi wa Habari, (International Day to End Impunity for Crimes against Journalists) uliokuwa ukifanya kupitia mtandao wa Zoom.
Aidha Nsokolo ameutaka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC), kutumia klabu za Waandishi wa Habari nchini kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari katika jamii ili kusaidia kupunguza hali ya uhasama dhidi ya waandishi wa habari.
“Naomba kusisitiza umuhimu wa kuelimisha umma juu ya umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya waandishi wa habari katika jamii. UTPC na klabu zake zote na kwa kushirikiana na wadau wengine tunapaswa kuhakikisha kwamba umma unaelewa umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na jukumu la waandishi wa habari,”Amesema.
Amesema kwa kufanya hivyo ufahamu wao juu ya jinsi vyombo vya habari vinavyochangia kujenga jamii yenye habari na taarifa sahihi na uelewa sahihi utaongezeka na kusaidia kuzuia misimamo ya upande mmoja na kupotosha habari.
Nsokolo amesema umma ulioelimishwa unaweza kushiriki zaidi katika mchakato wa kisiasa na kijamii na hivyo kuwa na mchango mzuri sana katika ujenzi wa taifa. “Kwa kuelewa jukumu la waandishi wa habari katika kuchunguza masuala ya umma, umma unaweza kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wao”.
Amesema vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kufichua uhalifu na ufisadi hivyo kuelimisha umma juu ya jinsi waandishi wa habari wanavyochunguza na kuripoti masuala hayo kunaweza kusaidia katika kupambana na vitendo hivyo visivyo vya maadili.
“Umma unaoheshimu na kuelewa umuhimu wa vyombo vya habari huru unaweza kuchangia katika kudumisha demokrasia thabiti kwa kushiriki kwa ufahamu katika mchakato wa uchaguzi na kutoa maoni kuhusu sera na masuala ya umma, ambayo ni muhimu katika ujenzi wa taifa”. Amesema.
Pia amesema vyombo vya habari vina jukumu la kuchunguza na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadam ambapo kusaidia kugundua na kusimamia haki za binadamu kunaweza kusaidia katika kuzuia vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Nsokolo pia amezishukuru taasisi mbalimbali ikiwemo Ubalozi wa Uswiss hapa Tanzania, kwa ufadhili wa miradi mbalimbali, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camillus Wambura, kwa kuendelea kushirikiana na UTPC katika kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari hapa nchini unakuwepo na hivyo kuwawezesha kuendelea kutimiza jukumu lao la kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kuanzia mwaka jana, UTPC na Jeshi la Polisi tunaendelea kufanya midahalo na Jeshi la Polisi na kukubaliana mikakati ya ulinzi na usalama wa waandishi. Waratibu wa klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC), kwa kuendelea kuratibu na kuyatolea taarifa matukio matukio ya ukiukwaji wa uhuru wa kupata na kutoa taarifa na madhila yanayo wapata waandishi wa habari hapa nchini,” Amesema.
Nsokolo amemalizia hotuba yake kwa kutoa wito kwa vyombo vya dola vyenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, vichunguze matukio ya uhalifu dhidi ya waandishi wa habari.