Watoto 3,870 chini ya miaka mitano ikungi waugua malaria

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dk Dorisila John akitoa maelezo kwa Mwandishi wa habari (hayupo pichani) juu ya hali ya ugonjwa wa malaria ilivyo katika wilaya hiyo kwa watoto walio na umri wa maiaka 0 -8 

 Na Abby Nkungu, Singida 

Zaidi ya watoto 3,870 wenye umri  chini ya miaka mitano wameugua ugonjwa wa malaria katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa kipindi cha Januari 2022 hadi Juni mwaka huu.

Hayo yalibainishwa na Mganga Mkuu wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Dk Dorisila John katika mahojiano maalumu na Mwandishi wa habari hizi juu ya hali ya malaria kwa watoto pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na idara yake na wadau wengine kukabiliana na changamoto hiyo.

Dk Dorisila alifafanua kuwa idadi hiyo ya watoto waliokumbwa na malaria ni sawa na asilimia 40 ya watu wote waliougua ugonjwa huo kwa kipindi hicho katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

“Kama nilivyosema watoto waliougua malaria kwa kipindi hicho ni 3,877 lakini wengi wao walipona baada ya kupatiwa matibabu kwenye vituo vyetu vya huduma isipokuwa watatu tu, sawa na asilimia 0.08 ndio waliofariki baada ya kucheleweshwa kwenye matibabu” alieleza Dk Dorisila.

Alisema kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo wameelekeza nguvu zaidi  katika kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kulala ndani ya vyandarua vyenye viuatilifu na kutumia njia nyingine za kujikinga na malaria.

Aidha, alieleza kuwa kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyojengwa kwenye maeneo mbalimbali nchini; hasa vijijini, ni fursa nyingine ya kusaidia kutoa elimu ya kuzuia maambukizi ya malaria sanjari na tiba kwa watoto wanaougua ugonjwa huo ili kupunguza vifo.

Mganga Mkuu huyo pia amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaotumia vyandarua kufugia samaki, kuku au kuoteshea mboga za majani badala ya kujikinga dhidi ya malaria.

“Hilo halikubaliki, tena halikubaliki kabisaa, nyandarua hivi vimetengenezwa maalumu kwa ajili ya  kuzuia mbu. Wanaofugia samaki, kuku au matumizi mengine wanafanya kosa kama havijaisha muda wake wa matumizi…… Waache mara moja” alisema na kuongeza kuwa viongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji wasaidie kwenye hilo.

Kwa upande wake, Joshua Ntandu ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika  lisilo la Kiserikali ESTL linalotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto anasema wamejipanga kusaidia kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza tatizo hilo.

“Ujue mtoto anaposhambuliwa na malaria madhara yake ni makubwa tofauti na mtu mzima maana mtoto kinga za mwili wake bado hazijaimarika. Kwa hiyo, sisi kama wadau wa masuala mtambuka kwa watoto tunaangalia namna ya kujikita zaidi kwenye kuzuia mazalia ya mbu na  kuhimiza matumizi sahihi ya vyandarua vyenye viuatilifu “ alisema.

Alifafanua kuwa lengo ni kuhakikisha “zero malaria” kwa watoto kama ilivyo madhumuni ya Programu hiyo inayoangazia masuala ya afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama kwa watoto wa miaka 0 hadi 8.

Hata hivyo, baadhi ya wazazi na walezi wanasema kuwa pamoja na kuzuia malaria kwa vyandarua na kudhibiti mazalia ya mbu, bado kuna changamoto nyingine ya mila potofu katika jamii; hasa vijijini.

“Mtoto anaugua malaria badala ya kupelekwa kituo cha huduma za afya wao wanasema ni degedege anakimbizwa kwa mganga wa jadi” a

Mhudumu wa afya akimpatia mtoto chanjo mpya ya malaria na rubella huku mama wa mtoto akishuhudia

Alisema mmoja wa maafisa wa Serikali katika kata ya Mgungira ambaye hakupenda kutajwa jina lake kwa kuwa sio msemaji kisha akaongeza;

“Hii ni mbaya sana huenda hata  idadi ya vifo ikawa kubwa zaidi. Sisi tunaoishi na wafugaji ndio tunayaona hayo yakitendeka” 

Anna Ndua, mkazi wa kijiji cha Siuyu wilayani humo anaunga mkono kauli hiyo akitaka viongozi wa dini, wazee wa mila, viongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji washirikishwe katika kutokomeza mila potofu kwa jamii inayopeleka watoto kwenye tiba asili badala ya vituo vya huduma ya afya.

Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria unataka kuharakishwa mchakato wa kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 kwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025