Serikali wilaya ya kishapu kuendelea kushirikiana na smaujata mkoa wa shinyanga katika kutokomeza ukatili

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Serikali ya Wilaya ya Kishapu imesema itaendelea
kushirikiana na Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga katika kuibua na kukemea ukatili unaoendelea kufanyika
kwenye jamii.

Hayo yamezungunzwa na viongozi mbalimbali wakati wa
ziara ya viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, ambapo leo wametembelea  Wilaya ya Kishapu kwa lengo la kuimarisha
uhai wa kampeni hiyo.

Viongozi hao akiwemo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Kishapu Bwana Sabinus Chaula, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu Esther
Zephania Gesogwe pamoja na kaimu katibu tawala wa Wilaya ya Kishapu Bwana Geven
Noah wamewapongeza viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwa juhudi
wanazozifanya huku wakiahidi kuendelea kushirikiana katika kutokomeza ukatili.

Wamesema jamii katika Wilaya hiyo bado inauelewa mdogo
juu ya haki zao za msingi ambapo wamesema baadhi ya familia ukatili bado
unaendelea ikiwemo mila na desturi kandamizi, mifumo dume pamoja na ndoa za
utotoni.

Wameiomba kampeni ya SMAUJATA Wilaya na Mkoa wa
Shinyanga kuendelea kushirikiana na serikali katika jitihada mbalimbali za
kupambana na ukatili ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ukatili, kuandaa
mabonanza mbalimbali, kufanya mikutano ya hadhara pamoja na kutembelea familia
ili kuibua ukatili unaoendelea kufanyika.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa
wa Shinyanga, Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana
Solomon Nalinga Najulwa jila maarufu Cheupe kempeni hiyo itaendelea kushirikiana
na viongozi wa serikali, wadau mbalimbali pamoja na wananchi katika kuibua na
kupambana na ukatili unaoendelea kufanyika kwenye jamii.

Kwa upande wake katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga
Bwana Daniel Kapaya amewashukuru viongozi hao ambapo amesema kampeni hiyo
itaendelea kutoa elimu ya ukatili pamoja na kuibua ukatili kwa lengo la kuhakikisha
jamii inakuwa salama siku zito.

Aidha Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Kishapu Mwalimu
Shamika Hilaly Juma naye amesema uongozi wa SMAUJATA Wilaya hiyo utaendelea
kushirikiana na viongozi wa serikali wakiwemo Polisi kitengo cha dawati la jinsia
wanawake na watoto kwa kuhakikisha wanaifikia jamii husika ili kuepukana na
athari zitokanazo na ukatili.

Viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga leo wamefanya
ziara yao ya kikazi Wilaya ya Kishapu na kwamba ziara hiyo ni endelevu ambapo
wanatarajia kufanya ziara katika Wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga.

 

 

Viongozi wa SMAUJATA Wilaya na Mkoa wa Shinyanga wakiwa
katika picha ya pamoja na katibu wa mbunge jimbo la Kishapu Bwana Godfrey
Nchimika Mussa ikiwa ni sehemu ya ziara ya viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa
Shinyanga katika Wilaya ya Kishapu leo Ijumaa Septembe Mos Mwaka 2023.