Smaujata mkoa wa shinyanga yawasihi wanafunzi bugweto kuepuka vishawishi vya ukatili

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii
Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga imewasisitiza wanafunzi kuepuka
vishawishi ambavyo husababisha ukatili, wawapo shuleni na katika jamii.

Hayo yamebainishwa na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga
wakati wakitoa elimu ya ukatili kwa wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto kata
ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.

Wamewasihi wanafunzi hao kuepuka vishawishi vibaya  ikiwemo kupewa zawadi ama kununuliwa vitu
mbalimbali na watu wasiowafahamu na kwamba hatua hiyo itawasaidia kuepuka ukatili,
mimba na ndoa za utotoni.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa
wa Shinyanga, Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana
Solomon Nalinga Najulwa pamoja na mambo mengine amewasisitiza wanafunzi wa
shule ya msingi Bugweto kuepuka makundi ya watu wasiofaa ambao wanajihusisha na
uvutaji wa madawa ya kulevya pamoja na vitendo vya uhalifu.

Mwenyekiti idara ya wanawake na watoto SMAUJATA Mkoa
wa Shinyanga Mwinjilisti Esther Emmanuel amewasisitiza wanafunzi hao kujiepusha
na vishavishi mbalimbali wanavyokutana navyo ili waweze kutimiza malengo yao na
kwamba hatua hiyo itawasaidia kuwa salama katika maisha yao ya kila siku.

“Ili
uwe salama kaa mbali na mtu anayekupa zawadi usiyemjua, watoto wa kike wanapewa
zawadi mtu anakwambia naona unanjaa njoo nikununulie chakula njoo nikupe soda
mwambie nyumbani nitazikuta mezani hata kama huna uhakika wa chakula nyumbani,
kataa zawadi unayopewa bila kujua makusudi ya ile zawadi kwani zawadi hiyo ni malengo
ya kukuvuta usogee ili akufanyie ukatili bila wewe kujua”.
amesema
Mwinjilisti Esther

Kwa upande wake katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga
Bwana Daniel Kapaya amewasisitiza wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto kupaza
sauti juu ya ukatatili huku akiwataka kujiepuka na tamaa ya pesa ambapo amesema
hatua hiyo itawasidia kujiepusha na vitendo vya ukatili.

“Wapo
baadhi ya wanafunzi mnafanyiwa ukatili lakini hamsemi mnanyamaza tu kuanzia leo
msiwe na siri mtu yoyote akikupa hela humjua zikatae usiwe na tamaa ya pesa lakini
pia mjitahidi kuwasikiliza walimu shuleni, wazazi lakini pia wapeni taarifa mtakapoona
viashiria vya ukatili, unaweza pia kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa au
tujulishe sisi SMAUJATA tutakusaidia au piga namba ya bure 116 utapata msaada
usikubali wewe au rafiki yako kufanyiwa ukatili”.
amesema
Katibu Bwana Kapaya

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Bugweto amesema
watahakikisha wanazingatia maelezo yaliyotolewa na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa
Shinyanga.

Naye Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugweto Yusuph  John Mbundi amewapongeza viongozi wa SMAUJATA
Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa elimu ya ukatili ambapo pia ameishukuru serikali
kupitia wizara ya maendeleo ya jamii jinsia, wanawake na makundi maalum ambayo
inaongozwa na Waziri Dkt. Dorothy Gwajima.

Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga
Bwana Solomon Nalinga Najulwa akitoa elimu ya ukatili kwa wanafunzi katika
shule ya msingi Bugweto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.