Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Herman Batiho |
Na. Edmund Salaho ARUSHA
Kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na makampuni ya waongoza watalii imepanga kuwapeleka watanzania katika kilele cha Mlima Kilimanjaro lengo likiwa ni kusherehekea miaka 62 ya Uhuru, tukio hili la kihistoria hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 9, Disemba.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA Herman Batiho amewaeleza wanahabari katika mkutano na Vyombo vya Habari Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha kuwa, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru wa Tanganyika tangu ulivyopatikana mwaka 1961.
Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kwa kupandisha bendera ya nchi yetu katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Tukio hili limekuwa likihusisha kikundi cha wanajeshi wachache wakishirikiana na askari wa Hifadhi za Taifa Tanzania kwa utaratibu wa kampuni ya utalii ya ZARA ambapo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita maadhimisho haya yalipata sura mpya ya ushiriki wa wananchi na kutambulika kwa jina la “Twenzetu Kileleni” ambapo kwa sasa ni msimu wa tatu.
Aidha, Kamishna Batiho aliongeza kupitia hamasa kubwa na mwamko wa watanzania wengi katika kipindi hicho ambapo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania limeongeza wigo kwa kushirikiana na mawakala wote wa utalii kuratibu kampeni za twenzetu kileleni kwa lengo la kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani wakati wa maadhimisho ya Uhuru tarehe 9, Disemba.
Lengo likiwa ni kuongeza wigo wa utangazaji wa njia nyingi za kupanda Mlima Kilimanjaro na fursa zaidi kwa watanzania kuchagua kampuni na njia wanazotaka kupanda mlima na sio njia ya Marangu tu kama ilivyozoeleka.
“Kati ya kampuni zote tulizozialika kushiriki katika uratibu wa maadhimisho haya ni kampuni tatu ndio zimejitokeza kushiriki kampeni hii katika msimu huu wa tatu. Kampuni hizo ni ZARA, African Zoom na African Scenic.” Alisema Kamishna Batiho.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro Angela Nyaki ametoa rai kwa watanzania wote kushiriki kuadhimisha sherehe hizo za uhuru katika kilele kirefu zaidi barani Afrika.
“Niwakaribishe wananchi wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kuja kushiriki nasi katika sherehe hizi za Uhuru katika Paa la Afrika. Nina imani watanzania wengi wana shauku kubwa ya kushiriki haya maadhimisho, kwa kulipa kidogo kidogo na kwa wale watanzania wenzetu ambao wamewahi kupanda kwa njia ya marangu nitoe wito sasa tuhamie njia nyingine ili tuuone mlima wetu kwa upande mwingine pia” aliongezea Kamishna Nyaki.