NA MASHAKA MHANDO, Mkinga
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman amekerwa na utekelezaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh. Bil 3.155 na amemuagiza Waziri wa Maji na Mkuu wa Mkoa Tanga kuutembelea mradi huo na kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa kutabainika ubadhilifu wowote .
Mradi huo unaosimamiwa na wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo(RUWASA) ambao umeonekana hauna ufanisi wala tija kwa wananchi zaidi elfu kumi wanaokabiliwa na adha ya maji Wilayani humo licha ya serikali kutoa fedha nyingi.
Mwenyekiti huyo alitoa maagizo hayo jana, akiwa Wilayani Mkinga katika mwendekezo wa ziara yake iliyokuwa na lengo la kukiimarisha chama hicho pamoja na kukagua miradi ya maendeleo na kusema watendaji watakaobainika kufanya ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Lazima tunyooshane mapema hasa kwa wale watumishi wazembe na chama chetu ndio kinachopata taabu wakati wa kampeni sasa sisi tunaanza kuchukua hatua kabla ya kukutana na maswali toka kwa wananchi” alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza
“natoa wito wataalamu wote wa serikali mkoani hapa ni vema mkatumia vizuri fedha zinazoletwa na serikali ili changamoto na kero za wananchi zipate majawabu”.
Aidha alisema kitendo kinachofanywa na Mamlaka hiyo ya Maji Wilayani Mkinga cha kujenga Tank la maji na miundombinu yake kwa wananchi bila ya kuwa na chanzo cha uhakika wa maji ni uchonganishi wa Rais na wananchi wake kwasababu ujenzi huo ungekwenda sambamba na ukarabati wa bwawa.
“Kinachoonekana hapa mradi wa tank utakamikika halafu maji ya uhakika hakuna, mwisho wa siku Serikali itamlipa mkandarasi pesa nyingi huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma hiyo ilhali wameona tenki likiwa limejengwa,” alisema.
Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akihangaika mchana na usiku kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo itakayowasaidia wananchi kuondokana na kero mbalimbali jambo la kusikitisha watendaji waliopewa dhamana hiyo hawatekelezi walichoagizwa.
Alisema hadi sasa mkoa wa Tanga umepokea kiasi cha sh 356,830,194,471 huku pia ikiwa inatarajia mradi mkubwa wa maji ya miji 28 Tanga zikiwa wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani ambao utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 181 kwa wilaya hizo.
Meneja wa RUWASA Wilayani Mkinga Thomas Kaijage, alisema bwawa hilo linachangamoto na linahitaji kufanyiwa ukarabati ili liweze kutunza maji ya kutosha yatakayoweza kuhudumia Wananchi hao na kuongeza kuwa wanategemea kupata fedha kwa bajeti ya mwaka 2023/2024.
Kaijage alisema kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kazi ya ukarabati wa bwawa hilo zitafanywa na wakala wa uchimbaji wa mabwawa na visima (DDCA) baada ya usanifu kukamilika.
Aidha alisema mradi huo unaojengwa Wilayani humo unakwenda sambamba na ujenzi wa Tank la maji litakaloweza kuhifadhi mita za ujazo 300,vituo 28 vya kuchotea maji,Ofisi ya Chombo Cha watoa huduma ngazi ya jamii(CBWSO),Machujio ya Maji(treatment Plant),uchimbaji na ulazaji wa mabomba na ufukuaji wa mitaro mita 48,000 na ukarabati wa Nyumba ya Pampu(pump house).
Mbunge wa wilaya ya Mkinga Dastan Kitandula alisema Rais ameridhia kata ya Gombero kuboreshewa miundombinu ya usambazaji wa maji na ujenzi wa tank ili kuweza kuwahudumia wananchi wanaokabiliwa na adha ya Maji kwa kipindi kirefu.
Aidha alisema upo mradi wa maboresho ya Bwawa la Gombero ambalo ndio chanzo kikuu cha maji utakaogharimu Shs Bil 4,na mradi mkubwa utakaotoa maji mto Zigi kuelekea Horohoro ambao utagharimu zaidi ya Shs Bil 34 na kuifanya Wilaya hiyo kuondokana na adha hiyo ya maji.
Ziara ya Mwenyekiti huyo itadumu kwa takriban siku 20 ambapo atatembelea Wilaya za Mkinga,Muheza,Korogwe Mji na Korogwe Vijijini na Wilayani Lushoto kama alivyoahidi kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa Tanga mara baada ya kuchaguliwa na kushika wadhifa huo.