VETA yatekeleza Agizo la Rais Samia, wazindua mtambo wa Gesi asilia wa Biogas

  • Waanza na Veta Oljoro, kusambaza nishati hiyo nchi nzima

Na Seif Mangwangi, Arusha

CHUO cha elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini (VETA), kimeanza kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan lililoagiza taasisi  za elimu zenye watu zaidi ya mia moja kubadilisha mfumo wa matumizi ya nishati ya kupikia katika taasisi zao baada ya kuzindua mtambo wa kwanza nchini wa matumizi ya nishati ya gesi jadidifu ya Biogas.

Mtambo huo wenye thamani ya zaidi ya Milioni 156 umezinduliwa rasmi leo Februari 12, 2025 katika chuo cha VETA Oljoro ikiwa ni msaada wa taasisi ya kikorea ya Umoja wa wanasayansi wasiokuwa na mipaka ‘Science Engineering Without boarder (SEWB)’, na kuhudhuriwa na watendaji wa taasisi mbalimbali chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mgeni rasmi, Profesa Ledislaus Mnyone ambaye ni Mkurugenzi wa sayansi, teknolojia na ubunifu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi nchini, akimwakilisha Katibu Mkuu wizara hiyo amesema Mradi huo unaakisi maono mapana ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuhakikisha matumizi ya nishati ya kupikia inafikiwa.

Aidha ametoa wito kwa taasisi zilizokuwa chini ya wizara hiyo kuhakikisha teknolojia hiyo inasambazwa kote nchini ili kuokoa gharama kubwa ya matumizi ya kuni, muda lakini pia kuokoa uharibifu wa mazingira.

Pia amewataka wasimamizi wa teknojia hizo kuzifanya kuwa endelevu na kuondokana na tabia ya miradi ya namna hiyo ikishazinduliwa kuaribika na kushindwa kuendelezwa jambo ambalo limekuwa likiipatia serikali hasara kubwa ya fedha.

Profesa Ledislaus Mnyone, Mkurugenzi wa sayansi, teknolojia na ubunifu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi nchini

“Nawapongeza sana VETA kwa ubunifu huu, kinachoonekana hapa ni matokeo ya agizo alilolitoa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambalo nyie mmelitekeleza kwa vitendo, naomba  mradi huu uwe endelevu na kuondokana na ile kasumba mradi ukishazinduliwa haufuatiliwi hadi unakufa, hii imekuwa ikiipatia serikali hasara kubwa sana, na sasa tutakuwa tunafuatilia maendeleo ya miradi hii ,”amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini, CPA Anthony Kasore amesema mradi huo ni wa majaribio na kwamba baada ya kuanza kufanyakazi na kupata ufanisi wake wataendelea kujenga mitambo mingine katika vyuo vyote vya VETA nchini ili kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais lakini pia kuokoa gharama za uendeshaji na kutunza mazingira.

Mkurugenzi wa Veta CPA Anthony Kasore

“Mradi huu ni mwanzo wa miradi mingine ambayo tunafikiria kuijenga katika vyuo vyetu, tunaenda kuanza mazungumzo na wenzetu wa Korea kuona namna watakavyotusaidia kujenga miradi mingine zaidi,”amesema.

Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini Monica Mbele amesema  wataangalia namna ambavyo mfumo huo wa uzalishaji wa gesi wa Biogas utakavyoweza kutumiwa kufundishia wanachuo watakaojiunga na vyuo hivyo ili kuwajengea uwezo na ujuzi wa kutengeza gesi majumbani pindi wanapomaliza chuo.

Mkurugenzi wa taasisi ya Science Engineering without boarder (SEWB), Wiin Soo Maeng ambaye pia ni profesa katika chuo kikuu cha Donkook Nchini Korea amesema mradi huo ni sehemu ya misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikitolewa na taasisi hiyo kutokana na teknolojia bunifu nchini Tanzania.

Amesema mradi huo ni matokeo ya mazungumzo kati ya ofisi yake na taasisi ya sayansi teknolojia na ubunifu nchini (Costech), ambayo iliomba msaada wa kusaidiwa kujengewa mtambo huo wa mfano ikiwa ni agizo la Mheshimiwa Rais Samia.
 Mkurugezi wa taasisi ya Envisol Technology Company Limited, Profesa Karoli Njau ambao ndio waliopewa kandarasi ya ujenzi wa mtambo huo amesema mtambo huo unauwezo wa kuzalisha gesi mita za ujazo 50 kwa siku na kuhudumia zaidi ya watu 1000.

“Kupitia uzalishaji unaofanyika hivi sasa, tumesambaza gesi maeneo mengi ya chuo kuanzia jiko la shule hadi kwenye nyumba za walimu, mtambo huu ni mkubwa ambao unaweza kuzalisha gesi zaidi ya mita za ujazo 50 kwa siku na sasa hapa matumizi ni mchana tu hivyo usiku gesi inakuwa imehifadhiwa kwenye mfuko maalum na ikijaa inatoka yenyewe bila kuleta madhara,”amesema.

Mwanaisha Kanjanja mpishi wa chuo hicho amesema ujio wa gesi hiyo umerahisisha shughuli zake za upishi chuoni hapo pamoja na kuepusha gharama kubwa ya ununuzi wa kuni ambazo walikuwa wakitumia hapo awali pamoja na kuokoa muda wa kutayarisha chakula kwaajili ya wanafunzi.

Mwanaisha Kanjanja akiendelea na mapishi ya chakula cha wanafunzi kwa kutumia nishati ya gesi ya Biogas iliyoanza kuzalishwa chuoni hapo