Afungwa miaka 30 kwa kubaka mwanafunzi

 

A Mwandishi Wetu, NJOMBE
Furaha Samweli Ligate (26) Mkazi wa Kijiji cha Unyangala Wilayani Makete mkoani Njombe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mara mbili mtoto mwenye umri wa miaka 15 ( jina linahifadhiwa) aliyekuwa amehitimu darasa la 7 mwaka 2021 akisubiri kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wa 2022
Hukumu hiyo imetolewa na mahakama ya wilaya ya Makete Machi 14 mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Ivan Msacky na mwendesha mashitaka Inspekta Msaidizi wa Polisi  Benstad Samson Mwoshe
Imeelezwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 24, 2021 majira ya saa 12 jioni na kurudia tena Desemba 25, 2021 kinyume na kifungu cha 130 (1)(2)(e) kikisomeka pamoja na Kifungu cha 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019
Mshtakiwa huyo anadaiwa kumwita chumbani kwake mtoto huyo ambaye ni mjomba wake na  kumbaka na kisha kumtishia kumdhuru  endapo angesema kwa yeyote ambapo alishindwa kuvumilia na kutoa taarifa ambapo mshtakiwa alikamatwa na alipopimwa hospitali mtoto akakutwa mjamzito. 
Mwendesha mashitaka wa serikali Inspekta Msaidizi wa Polisi Benstard Mwoshe ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho  kwa watu wengine kwani kitendo ni ukatili na kimemuathiri mtoto kwakiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kukatisha ndoto yake  kimasomo
Akizungumza mahakamani hapo kabla ya hukumu kutolewa mshtakiwa huyo ameiomba mahakama hiyo imuonee huruma na kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea ikiwemo mama yake mzazi ambaye ni mzee pamoja na watoto watatu ambao wanamtegemea na amewaacha bila utegemezi wake
Hakimu Mkazi Msacky amesema mahakama hiyo imezingatia maombi ya mshtakiwa ya kupunguziwa adhabu hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani kwa kosa la ubakaji na kumhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani.