SHIRIKA lisilo la kiserikali la afya Plus kupitia mradi wa maabara ya Hedhi salama unao lenga kuondoa vikwazo wanavyovipata binti wakati wa hedhi wakiwapo shule limetoa msaada wa mashine 15 na vifaa vya kuzalishia taulo za kike shuleni kati ya mashine 50 zitakazotolewa Kwa shule lengwa mkoani Iringa .
Akitoa taarifa ya mradi huo wakati wa kukabidhi mashine hizo jana ,mkurugrnzi wa shirika la Plus Suzan Yumbe alisema kuwa kutokana na tafiti ambazo shirika hilo limefanya katika shule mbali mbali ndani ya mkoa wa Iringa na nje ya mkoa wa Iringa zimebaini uwepo wa vikwazo vya ufaulu kwa watoto wa kike pindi wanapokuwa katika siku zao za hedhi.
Hivyo kutokana na changamoto hiyo waliona njia pekee ya kumsaidia mtoto wa kike kusoma kwa raha wakati wote ni kuja na mkakati wa kumsaidia upatikanaji wa taulo za kike wakati wote awapo shule na njia rafiki ya kumwezesha kupata huduma ya taulo hizo bure ni kuanzishwa miradi ya ushonaji wa taulo za kike ambazo zitakuwa za kufua .
Mkurugenzi huyo alisema shirika hilo na wadau mbali mbali kama Malala Fund na wengine waliweza kujitolea vyerehani kwa ajili ya kuziwezesha shule kuanzisha miradi ya ushonaji wa taulo za kike katika shule ili kuwapatia bure mabinti wote wawapo shule .
” Kutokana na mkakati huo Afya Plus tumeamua kutoa mashine tano kwa kila shule kwa shule 15 za kuanzia kati ya shule 50 zitakazonufaika na mradi huo ili kuanza kuzalisha taulo za kike mashuleni ili kumwezesha mtoto wa kike kuwepo darasani wakati wote wa siku zake “
Hata hivyo alisema shirika hilo linatoa shukrani kwa serikali ngazi ya wilaya hadi Taifa kwa kutoa baraka za kuendelea na mradi huo mashuleni na wao wanaamini kupitia mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza wastani wa ufaulu kwa watoto wa kike wakiwemo wale waliokuwa wakishindwa kuhudhuria vipindi wakati wa siku zao .
Kwani utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) na mashirika mengine ulionesha kuwa watoto wa kike wengi wanashindwa kwenda shule kwa kipindi cha kati ya siku tatu hadi tano kutokana na kukosa uwezo wa kifedha wa kununua taulo za kike lakini pia kukosekana kwa maji mashuleni .
Kwa hali hiyo wao kama shirika la Afya Plus waliamua kuja na mkakati wa kuanzisha maabara ya Hedhi salama kwa kutoa mashine 45 ambazo kwa kila shule itapata mashine tano na wameanza na shule 15 kati ya shule hizo 50 zilizopo kwa mradi huo utakaofikia mabinti zaidi ya 36600 ndani ya mkoa wa Iringa .
Kwa upande wake mwalimu wa afya shule ya Sekondari Ipogolo Iringa Munira Mabruki alisema msaada huo uliotolewa na Afya Plus utakuwa ni ukombozi mkubwa kwa changamoto za mtoto wa kike awapo shule na kuongeza umakini wa masomo kwa watoto .
Hivyo aliomba wadau wengine kuendelea kujitokeza kumsaidia mtoto wa kike kuondokana na changamoto za Hedhi awapo shuleni ili kumfanya atumia muda wake mwingi kufuatilia masomo .
Mgeni rasmi katika tukio hilo Martha Luhambano aliye Muwakilisha Afisa elimu mkoa wa Iringa amesema kuwa vifaa na elimu inayotolewa na shirika la afya Plus vitasaidia kuondoa changamoto za hedhi kwa Watoto wakike shuleni na kuokoa afya zao kwa kuwaepusha kupata madhara ya kutumia vifaa ambavyo si salama na kuwataka walimu kuhakikisha vifaa walivyopokea vinatunzwa na vinafanya kazi .