Apc,mct wakutana kujadili ukiukwaji wa maadili ya waandishi wa habari


Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura katikati mwenye tai, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa APC, Mwenyekiti Claud Gwandu wa pili kutoka kulia, Zulfa Mfinanga katibu Mtendaji wa kwanza kulia, Saumu Mwalimu kutoka MCT wa kwanza kushoto na Cynthia Mwilolezi Mwekahazina wa APC

Na Seif Mangwangi 

Arusha

Baraza la Habari Tanzania (MCT), limekutana
na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), leo Machi
19,2024 na kujadiliana namna ya kutatua tatizo la ukiukwaji wa maadili miongoni
mwa waandishi wa Habari mkoani humo.

Ujumbe wa Baraza la Habari
ulioongozwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Ernest Sungura umekutana na
viongozi wa APC ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa APC kutamka
hadharani kuwa Wadau wamekuwa wakilalamikia Waandishi wa Habari kutumia taaluma
yao vibaya ikiwemo kuvamia kwenye mikutano na kulazimisha kupewa fedha kinyume
na maadili ya uandishi.

Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu akizungumza katika kikao hicho, katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Ernest Sungura na anayefuatia ni  Saumu Mwalimu Afisa Programu wa MCT

Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu
amesema malalamiko ya wadau yamekuwa yakitia doa taaluma ya Habari nchini jambo
ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuweza kukomesha vitendo hivyo
na kurejesha imani ya wadau kwa wanahabari nchini.

“Kila klabu ya habari nchini kupitia
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kuna kamati za maadili,
lakini kumekuwa na changamoto kubwa ya namna ya kudhibiti waandishi wa habari
wanaokiuka maadili kwa kuwa, sio wote ni wanachama wa klab za Waandishi wa habari
za Mkoa na uanachama ni hiyari, alisema na kuongeza:

Katika ngazi ya klabu mnaweza kumpatia
Mwandishi wa Habari adhabu lakini ni nani atakaye kazia hiyo adhabu?, hili limekuwa
tatizo kubwa sana, ambalo hapo nyuma tulishajaribu kufukuza waandishi waliokiuka
maadili na mwisho tulishindwa kuwadhibiti,” amesema.

Amesema ni lazima Taasisi zote za
kihabari nchini kuunganisha nguvu ili kudhibiti hali hiyo, ikitokea mwandishi
amefungiwa basi hakuna sehemu atapeleka kazi yake na hata hakuna sehemu ataweza
kuirusha kazi hiyo ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania, Ernest Sungura akisaini kitabu cha wageni

 

Kwa upande wake Ernest Sungura
amesema Baraza la Habari nchini linaangalia namna ya kuweza kukutanisha taasisi
za Habari nchini ili kujadiliana suala hilo ambalo ni miongoni mwa programu za
MCT ambazo imekuwa ikiziendesha ili kuhakikisha taaluma ya Habari nchini
inaheshimika.

Amesema uvunjifu wa maadili ni
sumu mbaya ambayo imekuwa ikipingwa na taaluma mbalimbali hivyo Waandishi wa Habari
kukiuka maadili ya uandishi ni jambo la aibu ambalo halipaswi kufumbiwa macho.

“Mimi nina kikao na watu wa TCRA ,
nikikutana nao tutajadili namna bora ya kusimamia maadili kwenye hivi vyombo
vya Habari mtandaoni, ili kuona namna watakavyoweza kudhibiti wanaovunja
maadili ya Habari, lakini pia nimeona kuna haja ya kuendelea na ziara katika
taasisi zingine ili kukusanya maoni yao na kuona namna bora ya kudhibiti hali
hii,”amesema.

Hata hivyo Mwenyekiti Gwandu amewataka wadau kutoogopa kuleta kazi zao Mkoani Arusha kwa kuwa tayari hatua za kudhibiti Hali hiyo imeanza kuchukuliwa.

APC Pamoja na MCT wamekubaliana
kuchukua hatua za haraka kukabiliana na tatizo hilo la uvunjifu wa maadili
miongoni mwa waandishi wa Habari nchini ambapo hatua mbalimbali zinatarajiwa kuchukuliwa hivi karibuni.