Balozi wa uswizi kushiriki wiki ya azaki arusha

Na Seif Mangwangi, Arusha 

Balozi wa Uswizi nchini, Didier Chassot, anatarajiwa kuwa miongoni mwa washiriki wa kongamano la wiki ya Azaki inayotarajiwa kuanza kesho Jijini Arusha ambaye atatoa neno la ufunguzi.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo Oktoba 22, 2023 jijini hapa Mkurugenzi Mkazi wa CBM ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya wiki ya AZAKI, Nesia Mahenge amesema madaa kuu na hotuba ya siku ya ufunguzi itatolewa na Abuubakar Ally, Mtanzania na mwanateknolojia anayefanya kazi katika kampuni ya simu ya Apple Inc yenye makao makuu Nchini Marekani.

Nesia amesema wiki ya azaki mwaka huu imelenga kukutana na Serikali, wananchi, wanazuoni pamoja na sekta binafsi kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya Taifa kiteknolojia.

” Tarehe 25, tutakua na mada maalumu itakayofanyika In this session, Water for People and The Nelson Mandela African Institution of Science and Technology’s (NM-AIST) ambapo wanaazaki watakutana pia na wanachuo kujadili ,kuchunguza suluhu na mbinu za kisasa zenye lengo la kukuza uwazi na uwajibikaji uendelevu wa usimamizi wa rasilimali za maji,”amesema.

Nesia Mahenge amesema majadilianao hayo ni fursa ya kipekee ya kuchangamana na wadau wa maendeleo kwani wamelenga kuangalia jamii ilipotoka, ilipo hivi sasa na inakwenda wapi katika nyanja ya teknolojia ili kuelewa mabadiliko yaliyopo, kukabiliana na changamoto pamoja na kutumia fursa zinazotolewa.

“Kauli mbiu ya wiki ya AZAKI mwaka huu wa 2023 ni Teknolojia na Jamii, ambapo suala kubwa ambalo tutalizungumzia ni kujitathmini ni kwa kiasi gani tumeweza kutumia teknolojia katika miradi na kazi zetu, ikiwa ni pamoja na kuangalia ni maeneo gani ambayo tumejifunza na ni maeneo gani yana changamoto” amesema Mahenge.

Amesema lengo kuu la wiki ya AZAKI 2023 limebaki kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi, serikali na wananchi ambapo mijadala itakayojadiliwa imejikita zaidi katika ujumuishwaji wa teknolojia kwenye kazi za AZAKI, kuziwezesha na kuzipa nguvu jamii zilizotengwa, utetezi ushirikiano pamoja uchechemuzi wa kidigitali.

Mijadala mingine ni matumizi ya takwimu kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika jamii ikiwemo ukusanyaji wa takwimu na uchambuzi, teknolojia na maadili, ubunifu wa teknolojia kwa maendeleo endelevu pamoja na kujadili ni kwa kiasi gani wameweza kufanikisha na ni katika maeneo gani wanahitaji kuboresha utendaji kazi wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dr. Anna Henga amesema mijadala hiyo pia itajikita katika masuala ya kimaadili katika kupokea matumizi ya maarifa bandia (Artificial Intelectual) ili kuhakikisha kuwa maarifa hayo yanalenga kukabiliana na changamoto za kijamii na kuleta manufaa kwa jamii nchini Tanzania.

Mwakilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Deogratius Temba amesema katika kuhakikisha kauli mbiu ya mwaka huu ya Teknolojia na Jamii inakuwa jumuishi kwa jamii yote, watahakikisha makundi yaishio pembezoni hususani wanawake nao wanafikiwa.