Cords kusaidia longido kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Longido.

Wananchi wa wilaya ya Longido mkoa wa Arusha, wanatarajiwa kukabiliana kidigitalia na athari za mabadiliko ya tabia katika mradi ulioandaliwa na Shirika la utafiti na huduma za jamii(CORDS) kwa kushirikiana na taasisi ya Microsoft ,chuo kikuu cha kilimo(SUA) na Serikali.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la CORDs Lilian Looloitai amesema wilaya ya longido ni miongoni mwa wilaya ambazo zimeathirika sana na mabadiliko ya tabia nchi na kuharibu nyanda za malisho ya mifugo na kuvamiwa  na magugu vamizi ambayo yanasambaa kwa  kasi.

Amesema katika mradi wa miaka mitatu,wa uboreshaji wa nyanda za malisho, utakuwa katika vijiji saba vya wilaya hiyo..

Amesema taasisi ya Microsoft itasaidia kidigital kutoa  taarifa juu ya  kumbukumbu ya hali ya mazingira, uoto wa asili, masuala ya hali ya hewa na maji ambazo zitakuwa zikitumiwa na wataalam na wananchi katika mradi huo.

“kuna ambao watapewa elimu juu ya kufatilia hali ya mabadiliko ya tabia nchi kidigitali na kuweka kumbukumbu ambazo zitasaidia mpango wa kukabiliana na athari hizo”amesema

Looloitai amesema katika mradi huo,wanatarajia kung’oa magugu vamizi ambayo yamevamia ardhi ya Longido lakini pia kuchimba maeneo ya kutuama maji ya robo mwezi ambayo yatasaidia kurejesha uoto wa asili na kutunza mazingira.

“mradi huu utaanza katika vijiji saba ambavyo ni mundarara,Olbomba,Olpukei,Orgira,Olteoesu,oldonyo na a Leremet”amesema

Mkurugenzi halmashauri ya Longido, Jumaa Mhina amesema mradi huo umekuja wakati muafaka katika kusaidia wakazi wa Longido ambao wengi ni jamii ya wafugaji na wanategemea mifugo katika maisha yao ya kila siku.

Mmoja wa wafugaji Naiman Laizer amesema wafugaji wanaathirika sana na mabadiliko ya tabia nchi kwani sasa malisho yamepungua,njaa inaongezeka katika jamii na wamekuwa wakitumia muda mrefu kusaka malisho kwani magugu vamizi mifugo hawali.

Mradi huu umefadhiliwa na shirika la kimataifa la The Charitable foundation(TCF) la Australia.