Viongozi mbalimbali wakiwa meza kuu katika siku ya pili ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari duniani |
Na Zulfa Mfinanga,Arusha
Mkuu wa wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Said Mtanda amewakikishia usalama waandishi wa habari wanaohudhuria maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani ambayo kwa Kanda ya Afrika yanaadhimishwa kesho Jijini Arusha.
“Tunatambua waandishi wengi wa habari wametoka sehemu mbalimbali duniani, naomba niwaondoe hofu kuwa Mkoa wa Arusha upo salama na tulivu, kama mlivyokuja salama, mtaondoka salama pia” Amesema Mkuu wa wilaya.
Kwa upande mwingine, Mtanda amesema ujio wa ugeni huo ni Neema kwa wananchi na Mkoa wa ujumla kwani umesaidia kuongeza kipato Cha mwananchi mmoja mmoja na Serikali kupitia huduma mbalimbali wanazopata na kwamba Serikali itahakikisha huduma hizo ni bora na za viwango vya kimataifa.
Kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo kwa Kanda ya Afrika yanafanyika nchini Tanzania katika Mkoa wa Arusha.
Maadhimisho hayo yalianza jana Mei1,2022 ambapo mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwemo ukuaji wa teknolojia unavyoathiri tasnia ya habari huku kauli mbiu ya mwaka huu ikisema Uandishi wa habari na changamoto za kidigitali.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho hayo ya Kanda ya Afrika kesho Mei3,2022 Jijini Arusha.