Dc mtanda asikitishwa na taarifa ya polisi arusha kuwanyima waandishi wa habari ushirikiano

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda
Waandishi wa habari wanachama wa APC waksikiliza DC Mtanda (hayupo pichani)
Waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu mbele akimtoa hotuba ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha Said Mtanda
Waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja na DC Mtanda

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mkuu wa wilaya ya Arusha Said Mtanda ameshangazwa na taarifa ya Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha Claud Gwandu juu ya jeshi la Polisi kukataa kukutana na waandishi wa habari kwa lengo la kujenga mahusiano na kusema waandishi wa habari sio wa kuwakimbia kwa kuwa wamekuwa msaada mkubwa kwenye ulinzi na usalama wa nchi.

Akimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya kwenye mkutano wa wanahabari Arusha Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu alimweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa kumekuwepo na misuguano ya mara kwa mara kati ya waandishi na jeshi la polisi lakini waandishi wakiandaa mikutano na   RPC amekuwa akisingizia kuwa na kazi nyingi na hata anapoombwa kutuma mwakilishi amekuwa akigoma kufanya hivyo jambo ambalo limekuwa likitoa tafsiri mbaya miongoni mwa wanahabari na jeshi hilo.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, RPC wetu amekuwa tofauti sana na makamanda wengine zaidi ya10 ambao wameshapata hapa Arusha tangu mimi nilipofika, yeye amekuwa anapiga picha ofisini kwake na waandishi wake anatuma kwenye makundi ya whatsap, kitaaluma sio sawa kwa kuwa tunakosa haki ya kuhoji, lakini kumekuwepo na misuguano ya hapa na pale kati ya waandishi na Polisi lakini amekuwa hatoi ushirikiano, tunaomba ukamweleze tunataka kukutana naye,”amesema Gwandu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha waandishi wa habari kuhusu masuala ya uhuru wa habari,ulinzi na usalama, haki za binaadam, utawala bora na demokrasia na waandishi wa habari wanawake na changamoto wanazokabiliana nazo,  Mtanda  amesema ukiona kiongozi anamkimbia mwandishi wa habari atakuwa na matatizo katika utendaji wake wa kazi au kuna mambo ambayo anayaficha hataki yajulikane.

” Mimi Waandishi wa habari ni marafiki zangu siwezi kuwaogopa kwa kuwa mimi sili rushwa na wala sipendi Majungu, waandishi kwangu ni sehemu ya msaada wakija na maswali ndio nafurahi kwa kuwa wananisaidia kujua eneo lenye upungufu  fulani na linatakiwa kufanyiwa kazi, kama nikiwakimbia matatizo ya wananchi nitayatatuaje?,” Alihoji Mtanda.

Amesema kwa kuwa yeye anafanyakazi ngazi ya wilaya hivyo anayo mamlaka ya kuwasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya hivyo atamuagiza akutane na waandishi wa habari na kufanya nao mazungumzo kwa mambo yanayohusu ngazi ya Wilaya.

“Malalamiko yenu nimeshapokea, lakini mimi ninayo mamlaka na Mkuu wa Polisi Wilaya, nitamuagiza aje kuwasikiliza tena leo leo atakuja hapa na kwa mambo yanayohusu Mkoa nitayafikisha ngazi husika yenye Mamlaka na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,”aliahidi DC Mtanda.

Pia DC Mtanda amewataka waandishi wa habari kuandika habari kwa kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari na kuepuka  kuwa wafuasi wa watu ili kulinda hadhi na taaluma zao kwa maslahi ya nchi na siyo ya mtu binafsi.

Amesema anatambua na kuthamini Kazi zinazofanywa na waandishi wa habari hivyo kuwataka kumshirikisha  muda wowote kwa jambo lolote lenye maslahi kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia amesema tangu alipoanza kutekeleza majukumu wilayani humo,  amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kila changamoto inayowakabili wananchi inatatuliwa kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao ya msingi kupitia Serikali yao.

 “Msiogope kufanya Kazi zenu iwapo mtafanya kwa kufuata misingi ya habari, kwa niaba ya Serikali ya wilaya yangu tutatoa ushirikiano wa kutosha kwa waandishi wa habari ila na ninyi mtumie kalamu zenu vizuri kwani kalamu ni kama risasi iwapo hazitatumika vizuri” alisema Mhe. Mtanda.

Awali Mwenyekiti wa chama hicho, Claud Gwandu alimweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa jeshi la polisi kupitia kwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha limekuwa likinyima ushirikiano na waandishi wa habari licha ya kuitwa mara mbili kukutana na waandishi hao.

Hata hivyo amemshukuru Mkuu huyo wa wilaya kwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari na kusema chama hicho kitahakikisha waandishi wanafuata maadili ya uandishi wa habari Ili kuwapa walaji habari zenye ukweli na uhakika