Dit washiriki mashindano ya kitaifa ya sayansi, teknolojia na ubunifu (makisatu) 2021

Na Mwandishi Wetu.

Leo Mei 8,  2021 Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam (DIT) imeshiriki  katika kilele cha Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2021. 


Dkt. Richard Joseph Masika (aliyevaa Koti la kijivu na shati jeupe)  ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi akiwa katika banda la DIT leo.



Mashindano hayo  yameratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  yaliasisiwa mwaka 2019 kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yakiwa na lengo la  kuibua, kutambua, kuadhimisha, kujenga, kukuza na kuendeleza ubunifu wa Watanzania katika nyanja za Sayansi na Teknolojia ili kuchangia juhudi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini. Ikiwa ni  sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuimarisha na kuendeleza teknolojia na maarifa asilia ya ndani ili yaweze kuchangia katika uchumi wa nchi. Kwa mwaka huu kaulimbiu ni  ”Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Uchumi Endelevu”. 



Katika ufunguzi wa Mashindano hayo Kitaifa  Jana Mei 7,  Jijini Dodoma Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisema Serikali imepata Mafanikio makubwa katika kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa kuibua na kuendeleza wabunifu wachanga 1066 kupitia MAKISATU 2019 na 2020 ambapo kati yao wabunifu mahiri 130 wanaendelezwa na serikali ili ubunifu na teknolojia wanazozalisha zifikie hatua ya kubiasharishwa.