Dkt.biteko aagiza soko la madini lianzishwe bunda

Na Steven Nyamiti-WM

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Bunda Joshua Nasari, Afisa Madini Mkazi Nyaisara Mbaya, na Katibu Tawala wa Mkoa Albert Msovela kuhakikisha wanafungua Soko la Madini wilayani  Bunda Mkoa wa Mara ili kuwarahisishia wachimbaji na  wafanyabiashara wa madini kupata huduma hiyo karibu.

Agizo hilo amelitoa leo Desemba 28, 2021 wakati akizungumza na wachimbaji katika eneo la Kinyambwiga lililopo Kata ya Guta wilayani Bunda mkoani Mara.

Dkt. Biteko amesema kuwa, haiwezekeni mchimbaji ana dhahabu yake mfukoni anaenda hadi Musoma kutafuta soko.

Amesema, ni lazima soko la madini lianzishwe Bunda ili watu wafanye biashara ya madini kwa urahisi.

“Natoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya, Afisa Madini na Katibu Tawala wa Mkoa ambaye kwa mujibu wa kanuni ya uanzishwaji wa masoko ya madini ndiye mwenye kutafuta eneo sahihi ya kuweka soko la madini,” ameongeza Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, bado kuna umbali mkubwa hivyo kutoka eneo la machimbo mpaka Bunda na kuwataka kianzishwe kituo kidogo cha kununua madini katika eneo la Kinyambwiga. Amesema, eneo litaandaliwa kwa wafanyabiashara wa madini ( Brokers) ili biashara yote ifanyike katika eneo hilo la wachimbaji.

Aidha, Dkt.Biteko amesema, ni lazima utaratibu mzuri uwekwe ili mialo igawanywe kwenye makundi ili uwepo uongozi utakaosimamia na kuhifadhi vizuri takwimu.

Amesema kuwa, uanzishwaji wa soko na kituo cha kuuzia madini kutasaidia kupata takwimu kwa wote watakaotorosha madini katika mialo husika.

“Ukitaka ufanikiwe kwenye Sekta ya Madini ni lazima kuwe na utaratibu, ukiruhusu utaratibu wa kila mmoja kusema anachosema hamwezi kusimamia Sekta ya Madini,” amesema Dkt. Biteko.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa huduma za kijamii katika eneo la Kinyambwiga, Dkt. Biteko ameweka utaratibu kuwa, halmashauri ikutane na wachimbaji wote ili uwepo utaratibu wa CSR kwa ajili ya kuchangia maendeleo kwa ajili ya watu wa Kinyambwiga.

Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko ameagiza ifikapo tarehe 7 Januari, 2022 wamiliki wa mashamba na wenye leseni za uchimbaji kufikia makubaliano ya kumaliza migogoro waliyonayo ili kuwezesha shughuli za uchimbaji madini kuendelea katika eneo hilo. 

Amesema, mgogoro huo unasababisha madhara na kuwafanya wenye maduara kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Amesema, endapo mgogoro huo hautatatuliwa Serikali itasitisha shughuli za uchimbaji katika eneo la Kinyambwiga.

Naye, mmoja wa wamiliki wa leseni hiyo, Titus Kabua amesema, wako tayari kukutana na wamiliki wa wenye mashamba ili kutatua mgogoro huo. 

Amesema, agizo la Dkt. Biteko litatatuliwa ndani ya muda waliopewa ili pande zote mbili zifikie makubaliano hayo.

Katika ziara hiyo, ilihudhuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassari, Mbunge wa Jimbo la Bunda, Viongozi wa Serikali, Chama na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.