Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof. Faustin Kamuzora kumuondoa Efraz Mkama katika nafasi ya Uratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoa wa Kagera kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Dkt. Mwanjelwa ametoa maagizo hayo kwa Katibu huyo baada ya kutembelea walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Bukoba kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kukutana na Watumishi wa Umma kuhimiza uwajibikaji.
Naibu Waziri huyo, amesema utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unapaswa kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambayo ina dhamira ya dhati ya kuziwezesha kaya maskini kuboresha maisha.
Dkt. Mwanjelwa ameonyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mratibu huyo wa TASAF Mkoa wa Kagera na hivyo kutaka nafasi hiyo apewe mtumishi mwingine ambaye ana vigezo na uwezo wa kutekeleza maagizo ya Serikali kikamilifu kupitia utaratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanjelwa amedai kuridhishwa na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika nyanja za elimu, afya, uzalishaji mali na ujenzi wa nyumba unaofanywa na walengwa wa mpango huo mkoani Kagera.
“Nimejionea namna wanufaika wanavyotumia ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba bora za kuishi, kujishughulisha na kilimo, ufugaji na kugharamia mahitaji muhimu ya elimu na afya,” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa amesema, kwa kutambua mchango wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Serikali imeamua kutekeleza sehemu ya pili ya Mpango huo ambayo itatilia mkazo zaidi kwa walengwa kufanya kazi katika miradi itakayoibuliwa kwenye maeneo yao na kupata ujira kama njia mojawapo ya kuijiongezea kipato.
Akizungumzia suala la kutotekelezwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika baadhi ya maeneo, Naibu Waziri huyo amesema, Serikali imeamua kutekeleza Mpango huo katika maeneo yote nchini ili kuwafikia wananchi wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na umaskini.
Dkt. Mwanjelwa yuko mkoani Kagera katika ziara ya kikazi kujionea utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo.