Father on duty: mkakati mpya wa kutokomeza ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume arumeru

Baba wa zamu akiwa kwenye majukumu yake ya kutoa elimu kwa mmoja wa wanafunzi anaowahudumia katika shule ya msingi katika kata ya Kiranyi

 

“Nilipohamishiwa hapa shuleni kama Mwalimu Mkuu miaka sita iliyopita nilikuta baadhi ya Watoto
wa kiume wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wengine wakiwa kwenye
hali ya hatari sana. Nilijiuliza maswali mengi 
ya namna gani nitaweza kuwa
okoa watoto hawa  kwenye hili tatizo,”.

 

“Nilijikuta naingia kwenye maombi
na sala,  nikiwa namuomba sana Mungu anisaidie niweze
kufaniwa kwa kuwa hili tatizo ni hatari sana kwa mustakabali wa maisha yao ya
mbeleni hasa ukizingatia vijana hawa ndio tunaowatayarisha kuwa Baba wa familia
wa baadae,’’.

 

” Hata hivyo nilifarijika
sana siku moja baada ya kupokea ujumbe kutoka Halmashauri yetu ya Arusha ukiongozwa
na Afisa maendeleo ya Kata kuwa nimeletewa mradi wa kumsaidia mtoto wa kiume na kumlinda dhidi ya vitendo
vya ukatili ikiwemo ulawiti chini ya shirika la Center for Women and Children
Development (CWCD). Niliwapokea
kwa furaha kubwa nikijua  kabisa sasa tatizo
hili litakomeshwa na tutaokoa Watoto wetu,”.

 

Hayo yote si ya mwingine bali ni
maneno ya Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kiranyi, Mwalimu Hussein Mamboli
ambaye anasema shule yake ni miongoni mwa shule ambazo wanafunzi wa kiume walikuwa wamefanyiwa ukatili wa
kingono ambao una
madhara makubwa kiafya na kisaikolojia kitu ambacho kinawapelekea kushuka
kimasomo.

 

Anasema alipofika shuleni hapo
alikutana na kesi za wanafunzi kulawitiwa huko katika familia zao lakini
alishindwa kuwabaini kwa kuwa wengi walikuwa wakiogopa kutoa taarifa kwa
uongozi na hivyo walijikuta kuwa wanyonge wakati wote, huku wakiendelea
kuathirika kimya kimya.

 

Hata hivyo anasema mradi wa ‘Father
On Duty’ au ‘Baba wa Zamu’ ambao umeanzisha 
mfumo unaoitwa ‘Maabara ya Watoto’ umeweza kubaini Watoto wa kiume
walioathiriwa na vitendo vya ulawiti, wahusika wa vitendo hivyo na umeweza
kuwachukulia hatua za kisheria wote waliotajwa kuwafanyia Watoto hao vitendo
hivyo ya kikatili.

Baba wa Zamu

 

Anasema pia watoto ambao wamekuwa
wakinyanyaswa majumbani aidha kwa kupigwa na wazazi au walezi au kutendewa
vitendo vya kikatili vya namna yoyote ile wamekuwa wakiripoti matukio hayo
shuleni hapo na hatua zimekuwa zikichukuliwa.

 

Mwalimu Mamboli anasema ‘Maabara
ya Watoto’  imekuwa ikiendeshwa na ‘Baba
wa Zamu’ ambaye amekuwa  akikutana na
mtoto mmoja baada ya mwingine na kuzungumza nae kirafiki zaidi ili kubaini
matendo ya kikatili ambayo wamekuwa wakikutana nayo mtaani.

 

“Kwa kweli ‘Baba wa Zamu’
ameweza kubaini vitendo vingi vya unyanyasaji wanavyofanyiwa Watoto, sisi
walimu tulikwama kwa kwasababu wanafunzi wamekuwa
wakiogopa kutueleza kutokana na hofu ya  pengine watachapwa lakini
wamemueleza Baba wa Zamu’ kila kitu.  Na hapa ndipo tulipobaini hali halisi ya ukatili dhidi ya Watoto iliyopo
shuleni kwetu,”

 

Anasema katika shule yake kupitia
maabara ya Watoto’, kumeundwa kikundi Cha Watoto wa kiume 30 ambao miongoni
mwao wapo wale wote walioathirika na vitendo vya ukatili ikiwemo ukatili wa
Kingono kwa waliolawitiwa na wengine walionyanyasika kwa namna moja ama
nyingine na jamii.

 

Mwalimu Mamboli anasema kupitia
maabara hiyo mbali ya  Watoto kuweka wazi
vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa pia wamekuwa wakifundishwa aina ya vitendo
vya kikatili, namna ya kuepuka navyo na namna ya kuwaripoti wote wanaofanya
vitendo hivyo.

 

“Hivi sasa wanafunzi wangu
wamebadilika sana, wamekuwa wakija kuripoti mambo ya ajabu yanayoendelea huko
mtaani, na kama Kuna mwanafunzi anafanya au amefanyiwa vitendo vya ajabu
wanatoa taarifa, hii imekuwa
ikitusaidia kupinga vitendo hivi viovu
,” anasema Mwalimu Mamboli.

 

Anasema sababu mojawapo ya watoto
kujikuta wakilawitiwa ni ugumu wa maisha ya wazazi wa mtoto na kusababisha
mtoto kushinda na njaa, hivyo anapokutana na watu wabaya huwashawishi kwa
kuwapa pesa kidogo na kuwafanyia kitendo hicho cha kikatili.

 

Mwalimu Mamboli anasema yeye
binafsi amekuwa akisaidia Wanafunzi waliojikuta wamelawitiwa kutokana na
ushawishi wa pesa kwa kuwapatia nafasi ya kula chakula bure shuleni pamoja na
kuwanunulia vifaa vya shule ili kuwaepusha na kadhia wanayokutana nayo mtaani.

 

“Unajua tumebaini kuwa
sababu kubwa ya Watoto kufanyiwa ukatili wa Kingono ni umaskini wa baadhi ya
familia, unakuta mtoto anashinda njaa bila ya kula chochote, shuleni hapati
chakula kwa kuwa mzazi hajalipa, sasa akitokea mtu mmoja na fedha zake akamshawishi basi
mtoto anajikuta kaingia kwenye mtego, “anasema.

 

Anasema pia Wazazi wamekuwa
wakisababisha Watoto wao  kufanyiwa
vitendo hivyo kutokana na wengi wao kuishi maisha ya malezi ya upande mmoja (Single
Mother), na hivyo wakati mwingi kujikuta wakiwa kwenye mizunguko ya kutafuta
fedha huku mtoto akikosa malezi sahihi.

 

” Unakuta Mama yuko sokoni
tangu asubuhi mtoto anarudi nyumbani anaendelea kucheza kwenye makundi ya ajabu
ajabu  huko mtaani wakati mwingine
anakuwa na njaa, Mama akirudi usiku ndio akutane na mtoto wake, sasa huu muda wote lolote linaweza kutokea
na huku nyuma mtoto anakuwa hana ulinzi wowote,” anasema Mwalimu Mamboli.

 

Daktari Wilson Nyiti ni ‘Baba wa Zamu’ maarufu
kama ‘Father on duty’ anayesimamia Kata ya Kiranyi
ambayo ni miongoni
mwa Kata sita zilizopo kwenye
mradi huo chini ya shirika la CWCD kusaidia kutoa elimu ya ukatili kwa Watoto
na kubaini vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa Watoto katika Kata hiyo
ambaye
anasema hali ni mbaya.

 

Hata hivyo anasema kupitia mradi huo wameweza
kuzuia madhara ambayo bila jitihada za haraka na nguvu ya ziada yangeweza
kuendelea kutokea hususani vitendo vya Watoto wa kiume kulawitiwa.

 

Anasema alipopewa jukumu la kusaidia kubainisha
vitendo hivyo mashuleni, alijiuliza maswali mengi ya namna atakavyofanikisha
utekelezaji wake lakini kutokana na uzoefu na umri mkubwa aliokuwa nao aliweza
kukaa na wanafunzi hao ambao walifunguka kwa kumweleza mambo mengi.

 

“Watoto walinieleza mambo makubwa sana,
kazi kubwa tuliyoifanya ni kuwapatia ushauri wa a
thari ya hivyo vitendo na pia tumetoa taarifa
kwenye shirika la CWCD ambao na wenyewe wamekuwa wakiripoti Polisi na wahusika
wanaofanya ukatili huo kukamatwa,”amesema.

 

Anasema pia wamekuwa
wakiwafundisha watoto majukumu ya Baba wa familia na kuwajenga kisaikolojia
kuwa wato ni wazazi watarajiwa na wanapaswa kuwa na watoto na kikubwa kuwa
walinzi wa familia hivyo kama watafanyiwa vitendo vya kikatili kwa umri
waliokuwa nao watapoteza nafasi hiyo.

 

“Pia tumekuwa tukiwafundisha
maandiko ya Mungu yanasemaje kuhusu nafasi ya mwanaume katika familia, lakini
pia tumekuwa tukiwafundisha elimu ya ujasiriamali kama kilimo n.k, “anasema Dkt
Nyiti.

 

Hata hivyo anaiomba Serikali
kuweka mkazo kwa watuhumiwa kuweza kufuatiliwa kwa karibu pindi wanapokamatwa
na kushtakiwa kwa kuwa kesi nyingi huishia njiani na watuhumiwa kutochukuliwa
hatua jambo ambalo linafanya matukio kama hayo kuendelea kushamiri mitaani.

 

Kwa upande wake Mwalimu Mamboli
anaiomba Serikali kuongeza ruzuku kwa shule hususani kwenye suala la chakula
ili watoto wote waweze kula bure shuleni ili kuwaepusha na vishawishi vya pesa
kutokana na njaa wanazokuwa nazo.

 

Akizungumzia Mradi wa ‘Father On
Duty’ Mratibu wa mradi huo kutoka taasisi ya CWCD, Epifania Josephat
anasema  mradi huo ambao umefadhiliwa na
asasi ya Foundation For Civil Society (FCS), umetoa matokeo makubwa lakini pia
umepokelewa kwa furaha kubwa na Halmashauri ya Arusha.

 

“Mafanikio ya mradi ni makubwa
sana, Halmashauri imepokea kwa furaha na kwa kuwa bajeti yetu ya kuendesha
mradi ilikuwa ni kata sita pekee,lakini Serikali ndani ya Halmashauri ya Arusha
wilayani Arumeru imeelekeza kata zote zianzishe mradi huo wa ‘Baba wa Zamu’ na
tayari wameanza,”anasema.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Dkt Ojung’u Salekwa anakiri vitendo vya
ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume umeshamiri sana wilayani Arumeru na
kusema mradi wa ‘Baba wa Zamu’ ni mkombozi mkubwa kwa Halmashauri yake.

 

“Mimi niliposikia habari za mradi
huu kweli nilifurahi sana, niliupokea kwa mikono miwili na niliufikisha kwenye
baraza la madiwani na kukubaliana kuunganisha nguvu kwa kuwa hii ni vita ya
pamoja, kwa hiyo mradi huu umeshasambaa wilaya nzima, lengo ni kupambana na
vitendo hivi hatari kwa watoto wetu,”anasema.

 

Amesema Serikali wilayani kwake
inataka watoto wote walioko shuleni wapewe elimu ya ukatili na kuishauri Wizara
ya Elimu kuanzisha mtaala wa somo la ukatili mashuleni na kwamba itapendeza pia
elimu hiyo ikashushwa hadi kwenye nyuma za ibada, kanisani na msikitini.

 

Dkt Ojung’u anatoa wito kwa
familia kuwa makini na ndugu wa karibu hasa wageni wanapowatembelea kwa kuwa
watoto wengi wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ulawiti na ndugu wa karibu
wakiamini hawataweza kuwakatili watoto wao kumbe ni tofauti.