Mkuu wa shule hiyo, Karama Khalid akifurahia na wanafunzi wa shule hiyo ilipotangazwa kuwa ya nne kwa Mkoa wa Dar es Salaam na shule yao ya Dodoma kuongoza Mkoa huo kwenye matokeo ya darasa la saba. |
*Yashika nafasi ya kwanza Mkoa wa Dodoma
Na Mwandishi Wetu
SHULE za Fountain Gate Academy zimeendelea kufanya vizuri ambapo kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka huu zimefanikiwa kufanya vizuri zaidi na kuzipita baadhi ya shule kongwe nchini kiwilaya, Mkoa na kitaifa.
Kwenye matokeo hayo yaliyotangazwa na NECTA mwishoni mwa wiki, shule ya Fountain Gate Dodoma imekuwa ya kwanza kati ya shule 552 za Mkoa huo, ya kwanza pia kwenye halmashauri yake kati ya shule 104 na ya 171 kitaifa kati ya shule 11,909 .
Kwenye matokeo hayo kwa upande wa Fountain Gate Tabata imefanikiwa kuwa ya nne kati ya shule 92 za Wilaya ya Ilala na imekuwa ya 25 kati ya shule 498 Mkoa wa Dar es Salaam wakati kitaifa imekuwa ya 111 kati ya shule 11,909.
Mkurugenzi wa shule hizo, Japhet Makau alisema kwa upande wa shule hiyo Tabata wanafunzi 141 ndio walifanya mtihani huo na kati yao, 114 wamepata wastani wa alama A na 27 wamepata wastani wa alama B na hakuna C wala alama D.
Makau alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa shule yake kwani imefanikiwa kuzipita shule kongwe ambazo zilikuwa zikishika nafasi ya kwanza na aliwapongeza walimu kwa namna wanavyojituma kufundisha mpaka kupatikana kwa matokeo mazuri kama hayo.
Makau alisema haikuwa kazi rahisi kupata matokeo mazuri kiasi cha kuzipita shule kongwe hivyo walimu wa shule hizo wanastahili pongezi kwani wamekuwa wakifanyakazi usiku na mchana kuhakikisha wanafunzi hao wanaandaliwa vizuri kwaajili ya mitihani ya kitaifa.
“Nawashukuru wazazi kwa kuendelea kutuamini na kutupa watoto wao tuwaleee na kwa mafanikio haya napenda kuwaahidi kwamba hatutabweteka tutaendelea kufundisha kwa bidii kuhakikisha shule zetu zinaendelea kuwa juu kitaaluma na hata siku moja kushika nafasi ya kwanza kitaifa,” alisema Makau.
4. Mwalimu wa shule hiyo Said Mkila akionyesha tuzo mbalimbali ambazo shule hiyo iliwahi kupata kutokana na kufanya vizuri sana kitaaluma kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na kitaifa