Hatua zisipochukuliwa, watoto 7000 kubakwa mwakani: dkt rose reuben, wadau watakiwa kuchukua hatua

Dkt Rose Reuben, Mkurugeni Mtendaji TAMWA

  

Na Seif Mangwangi, Arusha

KUFUATIA kuongezeka kwa matukio ya
ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake nchini chama cha Wanahabari Wanawake
nchini (TAMWA), kimesema endapo hatua za haraka za kukomesha matukio hayo
hazijafanywa, kuna uwezekano wa watoto 
7000 kubakwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.


Katika taarifa yake iliyochapishwa
kwenye mtandao wa taasisi hiyo, Tamwa imesema pia endapo hatua za haraka
hazitachukuliwa, watoto 12,000 watakuwa 
wamefanyiwa ukatili katika kipindi
cha mwaka mmoja ujao jambo ambalo ni hatari na linatakiwa
kupatiwa ufumbuzi wa haraka.


Taarifa za jeshi la Polisi kupitia taarifa yake
iliyochapishwa kwenye tovuti ya Taifa ya takwimu inaeleza kuwa katika kipindi
cha Januari hadi Desemba, 2020 jumla ya makosa 11,001 yaliripotiwa
ikilinganishwa na makosa 12,223 kwa mwaka 2019, ikiwa ni  upungufu wa makosa 1,222 sawa na asilimia
10.0.


“Makosa yenye ongezeko kubwa la idadi ni Kunajisi (23),
Kutupa watoto (5) na Usafirishaji haramu binadamu (1). Aidha, makosa
yaliyopungua sana kiidadi ni Kubaka (574), Mauaji (394) na Kulawiti (278),”ilisema
taarifa hiyo.


Katika taarifa yake TAMWA imesema takwimu hizo mpya
zinaogofya na kutoa wito kwa wadau, Serikali, wazazi na walezi kukubaliana na
kutamka kuwa ubakaji nchini kwa hivi sasa ni janga.


“Tamwa tunaona ni wakati sahihi sasa, kwa wadau wa masuala ya
ukatili wa kijinsia, kukaa pamoja na kupanga mikakati mipya na madhubuti zaidi
ya kumaliza au kupunguza matukio haya kwani sheria na sera nzuri zipo lakini
ukatili huo bado unaendelea katika jamii yetu,”imesema taarifa hiyo
iliyosainiwa na Dkt Rose Reuben Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA.


Dkt Rose amesema “ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni
njia mbadala na mpya za kukabiliana na janga hili. Tunaliita janga kwa sababu,
watoto 3524 kubakwa si lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo
linaharibu kabisa mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho”.


Amesema Tamwa inaipongeza mahakama kwa kutoa hukumu na kufuatilia
kwa ukaribu kesi za ubakaji, na kwamba  ipo mifano ya waliohukumiwa kwa kufanya
matukio ya ubakaji sanjari na kutoa pongezi kwa madawati ya jinsia kwa
kusimamia upelelezi na kutoa ushauri kuhusu matukio au kesi za ubakaji na
ukatili mwingine. 

 

Dkt Rose alisema pamoja na jitihada zote hizo bado matukio ya
ukatili wa kijinsia yanaendelea kuongezeka kila kukicha na kuhoji tatizo liko
wapi na kudai ni muhimu kwa taifa, sasa kuendelea kubuni njia mbadala na mpya
za kukabiliana na janga hili.

 

“Tunaliita janga kwa sababu, watoto 3524 kubakwa si
lelemama, bali ni tatizo kubwa katika jamii yetu ambalo linaharibu kabisa
mustakabali wa maisha ya kizazi kijacho,”amesema.

 

 Amesema mbali ya ukatili wa kijinsia kwa watoto
kinamama wanaendelea kupokea vipigo, kubakwa, kupewa lugha dhalilishi katika
jamii yao hali inayowafanya kuwa kundi linaloomboleza na wakati mwingine
kuichukia jinsia yao. 

 

“Ukatili huu, una madhara ya muda mfupi, muda mrefu,
kiuchumi, kimwili na kisaikolojia kwa wanawake na wasichana na watoto wote kwa
ujumla, kwani inawazuia kushiriki kikamilifu na kwa usawa katika jamii
yao,” Amesema Dk Rose Reuben. 

 

“Hakuna namna nyepesi ya kuelezea madhara haya ya
ukatili wa kijinsia, tumewahi kuona, pengine tumesikia lakini bado jamii nzima
haijajua madhara yake kwa kina labda kwa sababu, matukio haya hayatokei kwa
wingi mara moja. Lakini tungewapata waathirika hawa na kuwakusanya pamoja, basi
Tanzania ingelia,” Dkt Reuben.

 

“Ubakaji huu wa watoto ni janga. Serikali itambue kuwa
hili ni janga kwa sababu madhara yake yanaweza yasionekana kwa sasa lakini
yataonekana baadaye wakati ambapo kizazi hiki cha sasa kitakapokuwa kimeshika
usukani” amesema Dkt Reuben.

 

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia
wanawake(UN-Women)zinaonyesha kuwa ukatili wa wanawake aghalabu hufanywa na
mwenza, mume wa zamani au wa sasa. Inaelezwa kuwa wanawake zaidi ya milioni 640
wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea waliwahi kufanyiwa ukatili na
wenza.

 

Ukatili huu unatajwa kusababisha msongo wa mawazo, kihoro,
mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa ikiwamo UKIMWI na wakati mwingine
waathirika kujiua. Takwimu hizo kadhalika zinaeleza kuwa, zaidi ya wanawake
87,000 duniani waliuawa na nusu yao, (50,000) waliuawa na mwenza au
mwanafamilia. Zaidi ya thuluthi, waliuawa kwa makusudi na mwenza/mume wa sasa
au wa zamani. 

 

Dkt Rose anasema TAMWA imeona zaidi kuwa unyanyasaji huu kwa
hapa Tanzania umeendelea kujikita pia katika mashindano ya ulimbwende, vyuo
vikuu, vyombo vya habari ikiwemo  mitandaoni pamoja na mahala pa kazi na
kusema kuwa yote hayo yasipofanyiwa kazi, basi tutakuwa na dunia isiyo salama
kwa kundi hili.

 

“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye
ameonyesha wazi kuwa anasimamia vyema haki za wanawake na watoto, tumemuona na
kumsikia akipinga lugha dhalilishi kwa wanawake na udunishwaji wa kundi hilo
katika nafasi za siasa na uongozi. Kongole Rais wetu,” Amesema Dkt Rose
Reuben