Jafo afurahishwa na maonyesho ya wanawake wafanyabiashara Dar
·Asema bidhaa zinakidhi viwango vya kimataifa
· Ataka zijazwe kwenye supermarket nchini
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Selemani Jafo amepongeza maonyesho ya wafanyabiashara wanawake yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri Jafo aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua maonyesho hayo ambayo yanaendelea kwenye viwanja hivyo ambayo yanatarajiwa kufikia kilele siku ya Almahisi ijayo kwa wanawake mbalimbali kupewa tuzo.
Maonyesho hayo yameandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake (TWCC) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ na wafadhili mbalimbali.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo jana jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo alisema baada ya kutembelea mabanda mbalimbali amejionea bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wafanyabiashara wanawake ambazo nyingi zinaviwango vya kimataifa.
“Nimefarijika sana kuona bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na nyingi zina nembo ya ubora wa Shirika la Viwango TBS zinahadhi ya kuuzwa kwenye maduka mbalimbali makubwa hapa nchini mnastahili pongezi kubwa sana,” alisema
Alisema wanawake hao wameonyesha ujasiri wa hali ya juu kuanzisha vikundi vya uzalishaji bidhaa mbalimbali hali ambayo imechangia kuongezeka kwa nafasi za ajira kwa vijana, anawake na hata kwa wanaume wengi nchini.
Alisema pamoja na janga la ugonjwa wa COVID uchumi wa Tanzania umeendelea kufanya vizuri na wanawake wametoa mchango mkubwa sana kwenye kutengeneza fursa za ajira kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kimataifa.
Alisema amefarijika sana kuona wanawake wakiwa kwenye vikundi mbalimbali vilivyopata mikopo ya asilimia 10 zinazotoka kwenye halmashauri mbalimbali na kufanikiwa kuanzisha biashara zao ambazo zinakwenda vizuri.
“Kuna mabanda nimepita wameniambia wanauza bidhaa ndani nan je ya nchi hongereni sana kwa hatua hii kubwa mliyopita mafanikio haya tuliyofikia ni sababu ya wanawake kuwa mahiri ya kurejesha mikopo kwa wakati,” alisema Waziri Jafo.
Alisema anatamani sana kuona bidhaa hizo zinasambazwa kwenye maduka yote makubwa hao nchini na zingine kusafirishwa nje ya nchi kwani zinasifa ya kuvuka mipaka ya Tanzania.
Aidha, Waziri Jafo aliwataka wanawake hao kutumia fursa ya ujenzi wa miradi mikubwa kama ule wa kuzalisha Megawati 2,150 wa Julius Nyerere kwenda kuuza bidhaa zao kwa watu wanaofanyakazi kwenye mradi huo.
“Wakina mama nawaomba sana msiwe wanyinge nyinyi ni mashujaa kwasababu nyinyi ndiyo mnajenga msingi wa nchi hii na mchango wenu kwenye maendeleo ya nchi ni mkubwa sana. Tuendelee kufanyakazi tumsaidie rais wetu kutimiza ndoto zake za kujenga uchumi imara,” alisema Jafo