Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akizungumza kwenye ufunguzi wa mashindano ya FEASSSA leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha
Rais wa FEASSSA Justus Mugisha akizungumza kabla ya ufunguzi wa mashindano ya FEASSSA leo katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa bwana Tixon Nzunda akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa mashindano hayo leo jijini Arusha
Picha mbalimbali zikionyesha matukio ya ufunguzi wa mashindano ya FEASSSA leo jijini Arush
Na Mwandishi Wetu APCBLOG ARUSHA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amelitaka Shirikisho la Michezo kwa shule za Sekondari za Afrika Mashariki (FEASSSA) kuwa na mipango ya pamoja ya kuendeleza vipaji vya watoto vinavyoibuliwa kupitia mashindano ya FEASSSA.
Akifungua mashindano hayo leo kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mhe.Jafo amesema lazima viongozi wa michezo kutoka nchi wanachama za Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa wabnakwenda kuvilea vipaji vya wanamichezo vitakavyopatikana kupitia mashindano hayo.
Amesema kuna tabia imejengeka kwamba watoto wenye vipaji wanaibuliwa kupitia michezo hiyo lakini vipaji hivyo vinapotea kwa kukosa matunzo na hivyo kupotea.
“Niwaombe nchi wanachama kila mmoja katika nchi anayotoka twende tukavilee vipaji mbalimbali vitakavyoibuliwa kupitia mashindano hayo,” amesema na kuongeza:
“Ninaamini tukifanya hivyo tutatenda haki sawa na changamoto kubwa ipo kwa wasichana ambapo taarifa zinaonyesha kuwa vijana wengi mahiri wasichana licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kimichezo lakini mdondoko umekuwa ni mkubwa.”
Mhe.Jafo amewataka waratibu wa nchi mbalimbali zinazoshiriki michezo hiyo kwenda kuwalea vijana wenye vipaji ili kuweza kuendeleza vipaji vya vijana hao kwa maendeleo ya michezo katika nchi zao.
Amesema jukumu la viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki katika sekta ya michezo ni kuhimiza na kuwajengea mazingira rafiki vijana ili waweze kukuza vipaji vyao na kujiendeleza katika michezo, kutanua wigo wao wa ushindani ndani na nje ya nchi, kanda na bara la Afrika.
Aidha Waziri Jafo amewataka wanamichezo wanaoshiriki michezo hiyo ngazi ya kanda kudumisha nidhamu wakati wote wa mashindano hayo.
“Mtambue kuwa nidhamu ina mchango mkubwa katika mafanikionkatika michezo na maisha kwa ujumla. Katika kushindana mtambue kuwa kuna kushinda na kushindwa,” amesema.
Pia amewataka vijana hao kuitumia fursa hiyo ya kukutana na wenzao kutoka nchi nyingine za Afrika Mashariki kubadilishana uzoefu wa masomo pia kwa ajili ya kuinua taaluma zao.
Waziri Jafo amewataka viongozi kutoka nchi za Afrika Mashariki wanaoshiriki mashindano hayo ya FEASSSA kuitumia fursa hiyo ya kuwepo nchini kuona uwezekano wa kutembelea vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini hususani kutembelea mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama za Tarangire na Ngorongoro ambazo zinapatikana katika mkoa wa Arusha kunapofanyikia mashindano hayo mwaka huu.
Mapema Rais wa FEASSSA Justus Mugisha amesema nchi za Afrika Mashariki hazina budi kuweka misingi mizuri ya michezo shuleni ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Amesema hatua ya nchi za Afrika Mashariki kupeleka nchi nne katika mashindano ya AFCON yaliyomalizika hivi karibuni nchini Misri ni dalili njema kuwa nchi hizo zimejipanga kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya kimataifa.
“Ni lazima tuwekeze katika michezo kwa vijana kama hawa wanaoshiriki mashindano ya FEASSSA kama kweli tunataka kupata mafanikio kwenye michezo ya kimataifa,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu bwana Tixon Nzunda jumla ya wanamichezo 3500 kutoka mataifa ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani na wenyeji Tanzania bara na Zanzibar watashiriki michuano hiyo huku nchi ya Malawi ikishiriki michuano hiyo kama mwalikwa.
Amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha michezo ya soka, riadha, netiboli, mpira wa mikono, mpira wa mikapu, vinyoya, raga, mpira wa magongo, mpira wa meza, na mpira wa kengele.
Bwana Nzunda ameongeza kuwa malengo ya mashindano hayo ni kukuza fani za michezo kwa wanafunzi kwa kuwashindanisha ili kubaini vipaji vya wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki na pia kudumisha na kuendeleza mshikamano kwa nchi wanachama miongoni mwa wanafunzi, walimu na viongozi wa shule kutoka Afrika Mashariki.
Mara baada ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo, kulifanyika mchezo wa kwanza wa soka wavulana baina ya timu ya soka ya Lindi ambao walikuwa washindi wa tatu wa UMISSETA mwaka 2019 ambayo ilicheza na mabingwa wa mashindano kama hayo wa nchini Kenya timu ya St.Antony ya Trans zoia ambapo matokeo yalionyesha mabingwa hao wa Kenya waliibugiza Lindi kwa magoli 4 kwa 0.
Michezo hiyo itaendelea kuchezwa kila siku hadi tarehe 24 agosti, 2019 ambapo fainali za michezo hiyo zitafanyika.
Ufunguzi wa mashindano hayo pia ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.Mrisho Gambo na viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka mkoa wa Arusha na nchi wanachama wanaoshiriki mashindano hayo.