Katambi atoa maagizo mazito, ni katika ziara kutembelea ujenzi wa madarasa shinyanga

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu  kazi, vijana na ajira Paschal Patrobas Katambi amewasisitiza viongozi wa jimbo hilo  kufanyakazi kwa kuangalia maslahi ya wananchi kwa lengo la kuleta maendeleo ili kufikia hatua iliyokusudiwa kwenye jamii na Taifa kwa ujumla. 

Naibu Waziri Katambi ameyasema hayo wakati alipotembelea na  kukagua ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali za sekondari na shule za msingi shikizi ambapo amesema ameridhisha hivyo ametaka viongozi kuendelea kufanyakazi kwa kuangalia maslahi ya wananchi.

“Kikubwa tu ni sisi kushirikiana ili mipango hii itimie tukianza kuvurugana hapa inakuwa ni kazi kweli tunapaswa kuangalia kazi tusiangalie mavazi tunataka tufanye kazi yaani lazima tuwe na mipango ambayo inatekelezeka maneno tuzungumze kwenye sehemu zingine vijiwe lakini kuhusu maendeleo yetu wazee wetu wapo watusimamie tufanye maendeleo kwenye maeneo yetu na ndiyo maana mimi nimewaambia tutaheshimiana na kiongozi kama kazi zinaenda vizuri na unafanya mambo ambayo yanamaslahi kwa wananchi wa Shinyanga tufauti na hapo hatuwezi kukuelewa lakini kama tunaona maendeleo sisi hatuna shida tena na wewe tena tunamwambia na Rais akuongezee muda ili utuhudumie zaidi”. 

Akiwa ameambatana na kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga mjini pamoja na viongozi wa serikali Katambi ametembelea kata zote zilizopo kwenye jimbo lake ikiwemo kata ya Mwawaza, Ndala, Masekelo, Chibe, Mwamalili pamoja na kata ya Old Shinyanga ambapo amewahakikishia wananchi kuzifanyia kazi changamoto zilizobaki hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi hiyo.

“Shukurani zangu ziende kwanza kwa mheshimiwa Rais Samia ambaye ndiyo kwa kweli tulilia na fedha tukapewa na zahanati mnaziona,mabarabara tunatengeneza na madarasa mnayaona kwa hiyo tutaendeleo kufanya hivi ili kuhakikisha mambo yote yako vizuri”.

Kwa upande wake Kaimu afisa elimu sekondari Manispaa ya Shinyanga Chibugu Mugini amesema ujenzi huo wa vyumba vya madarasa umekamilika kwa asilimia zote ambao utasaidia kuondoa adha ya watoto waliokuwa wakikosa nafasi ya kusoma hivyo ameiomba jamii kupeleka watoto shule na kwamba hakuna changamoto ya upungufu wa madarasa. 

“Tulipokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi huu umekamilika kwa asilimia mia moja na inakidhi kupokea wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka ujao 2022 lakini pia na wale wa shule shikizi madarasa haya yamepunguza upungufu mkubwa na sasa wanafunzi wote wataingia darasani wito wangu kwa jamii ambao watoto wao wamefaulu wawalete watoto wao shuleni hakuna upungufu wa jambo lolote lile  waje wasome hakuna mwanafunzi na wote watapata sehemu ya kukaa vipo viti na meza”.

Baadhi ya viongozi  wakiwemo madiwani na mstahiki meya wa Manispaa ya Shinyanga wameeleza kuwa kukamilika kwa madarasa hayo ni moja ya hatua za kuondoa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa watoto wanaaotarajia kujiunga kidato cha kwanza Mwaka wa masomo 2022.

Baadhi  ya wakazi `wa Manispaa ya |Shinyanga wameipongeza Serikali kwa hatua nzuri ya kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya madarasa hali ambayo wamesema imelenga kutoa huduma bora kwa jamii na kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi wote kupata fursa ya elimu.

Ziara ya mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia kazi, vijana na ajira Paschal Patrobas Katambi anamaliza leo ambapo atafanya mkutano wa hadhara eneo la miti mirefu mtaa wa Majengo kata ya Kambarage.

Ziara hiyo ya Katambi ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika jimbo lake ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa kupitia fedha za ruzuku ya UVIKO-19  zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   SAMIA SULUHU HASSAN.