Mkurugenzi mpya wa UTPC, Keneth Simbaya (kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa UTPC Deo Nsokolo(katikati), na Abubakar Karsan mkurugenzi wa UTPC anayestaafu |
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Sasa ni rasmi umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), umepata mkurugenzi mpya, Kenneth Weston Simbaya akichukua nafasi ya Abubakar Karsan ambaye anastaafu.
Kwa mujibu wa Rais wa UTPC Deogratius Nsokolo kupitia katika mtandao wa twitter, Keneth Simbaya alitambulishwa rasmi jana kwenye kikao kazi kati ya bodi ya wakurugenzi ya UTPC na mfadhili SIDA katika kikao kinachoendelea Jijini Dodoma.
Simbaya ambaye alishawahi kuwa Rais wa umoja huo wa klabu za waandishi wa habari nchini, anashika nafasi hiyo kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwa umoja huo na Karsan kuteuliwa kuwa mkurugenzi wake.
Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha imepongeza uteuzi wa Keneth Simbaya na kumtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake hayo mapya.
Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu amesema uteuzi wa Simbaya umefanyika kwa kuzingatia sifa, Historia na uchapakazi aliokuwa nao.
“Kenneth Simbaya anastahili kushikilia nafasi hii, anazo sifa zote, sisi kama APC tunamkubali na tunaamini atafanya mambo makubwa zaidi kwa nafasi aliyokuwa nayo hivi sasa, alishawahi kuwa Rais wa UTPC na aliyoyafanya tuliyaona na tunaendelea kuyafaidi hadi sasa,”amesema.