Kijana Andrew Mwakyoma wa pili kulia akiwa darasani akipata mafunzo ya ujasiliamali na wenzake
KIJANA Andrew Mwakyoma (17) mkazi wa Ibwanzi kata ya Ihanu wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ameshindwa kuendelea na masomo ya sekondari kidato cha tano kutokana na mama yake mzazi aliyekuwa akimsomesha kukosa sifa ya kuendelea kukopeshwa kwenye vikoba baada ya kuwa na mkopo sugu wa Tsh 500,000.
Andrew ambae alifaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2020 kwa kupata Divisheni 3 ya 24 ameendelea kukaa nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa akilima vibarua ili kutafuta fedha .
Akizungumza jana na mwanadishi wa habari hizi mara baada ya mafunzo ya ujasiliamali kwa vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu waliopo katika mradi wa Youth Agency Mufindi (YAM) kijana Andrew alisema kuwa toka alipoanza elimu ya sekondari kidato cha kwanza mahitaji ya shule ikiwemo ada aliyekuwa akihusika ni mama yake mzazi ambae alikuwa akikopa fedha hizo katika vikundi vya vikoba .
“Katika familia yetu tupo zaidi ya watoto na mimi nina mdogo zangu watatu kwa baba mmoja na hawa wawili baba tofauti na kati ya hao mmoja ameanza sekondari mwaka huu kidato cha kwanza na mmoja yupo shule ya msingi na wawili bado kuanza shule”
Hivyo alisema kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi wa mama yao amelazimika kusubiri kwenda kidato cha tano ili kupisha mdogo wake kwenda kuanza elimu ya sekondari kidato cha kwanza .
” Bado naendelea kusubiri mama apate fedha ili niende kuendelea na masomo yangu ya kidato cha tano na nina tamani sana kwenda shule ila sina uwezo wa kipato na mama ndio hivyo tena hana kitu kwa sasa nafikiri hata kwenda chuo cha maendeleo ya jamii ili nikapate elimu ya chuo hicho ila sina fedha kiasi cha Tsh 800,000 za kulipia “
Andrew alisema kwa sasa amechukuliwa na mradi wa Youth Angecy Mufindi (YAM) kama kijana anayetoka kwenye mazingira magumu na anaendelea na mafunzo ya ujasiliamali ili kufanya shughuli za ujasiliamali kama mtaji kwake kuendelea na ndoto yake ya masomo .
Mama mzazi wa kijana huyo Joyce Mtovano akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi alisema kuwa bado ana mpango wa kuwendeleza kimasomo kijana huyo ila hana uwezo wa kifedha na hivyo anaomba wasamaria wema kumsaidia kijana wake kurudi shule .
Joyce alisema hadi kijana huyo amefanikiwa kufika kidato cha nne ni kutokan na jitihada zake za kutafuta fedha kwa njia ya kulima mashamba pia kupika pombe za kienyeji .
Kuwa hali yake ya kiuchumi si rafiki kwani hata awali alifanikiwa kumsomesha kijana huyo sekondari kutokana na kupika pombe na kuzungusha fedha kidogo aliyoipata kwa kuweka kwenye vikundi vya Vikoba ambao waliweza kumpa mkopo wa Tsh milioni 1.7 mkoapo ambao hakuweza kuulipa kwa wakati hivyo kukosa sifa ya kuendelea kukopa na hadi sasa ameendelea kulipa mkopo huo toka mwaka 2020 na bado anadaiwa kiasi cha shilingi 500,000.
Alisema pindi atakapomaliza mkopo huo ataweza kuomba msamaha kwenye kikundi ili aweze kurejea na kuomba mkopo tena utakaowezesha kijana wake huyo kuendelea na elimu ya chuo ama sekondari.
Meneja mradi wa YAM Zilipa Mgeni alisema lengo la mradi wa YAM ni kuwapatia elimu ya ujasiliamali vijana waliopo kwenye mazingira magumu na wale walioacha shule ya msingi kama watoto hao wanarejeshwa shule kuendelea na masomo .
“Mradi wetu ni wa miaka minne umeanza mwaka jana unafadhiliwa na taasisi ya Deacones chini ya serikali ya Finiland na unatekelezwa na taasisi ya Foxes Community and Wildlife Trust kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na unatekelezwa kwenye vijiji 16 vya kata tatu za Ihanu, Mdabulo na Luhunga wilaya ya Mufindi na vijana 770 na watoto ndio watakaonufaika na maradi huu “