KILOSA
Vikundi 18 vya wanawake, watu wenye ulemavu na vijana vimekabidhiwa hati ya malipo yenye thamani ya shilingi 242,910,000 ikiwa ni takwa la kiserikali linalotaka Halmashauri kufanya hivyo kwa makundi hayo ambapo hati hizo zimekabidhiwa kwa makundi hayo kwa lengo la kuongeza tija ya kiuchumi.
Akikabidhi hati hizo Agosti 12 Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mh. Majid Mwanga amesema hati hizo ni sehemu ya alama ya Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2021 wenye kaulimbiu TEHAMA ni msingi wa Taifa Endelevu itumie kwa usahihi na uwajibikaji.
Ametaka vikundi hivyo kutumia fedha kwa kadri walivyoomba na kwamba anategemea kuona uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo huku akitoa onyo kwa watendaji wote wenye kutoza fedha kwa ajili ya kugonga muhuri jambo ambalo ni kosa kisheria na atakayekiuka endapo atabainika hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha ametoa rai kwa vikundi mbalimbali kuchangia miradi ya maendeleo katika maeneo yao huku akitoa ombi kwa vikundi vya bodaboda kuchangia mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi ya Mazinyungu.
Naye Kamanda wa TAKUKURU Wilaya Gwakisa Mwaikela amesisitiza juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo kwani zinatokana na wananchi walipa kodi na dhumuni lake ni kujenga uchumi huku akitoa angalizo kwa watakaokiuka sheria haitosita kuchukua mkondo wake.
Akisoma taarifa ya mikopo hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii Neema Solomon amesema mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi hivyo katika kata za Rudewa, Parakuyo, Kimamba, Magubike, Kitete, Mtumbatu, Mkwatani, Magomeni, Uleling’ombe, Msowero, Lumbiji, Kasiki, Vidunda na Mvumi ambapo shughuli zinazotarajiwa kufanyika kupitia fedha hizo ni ufyatuaji tofali, ufugaji na usafirishaji kwa njia ya bodaboda.
Wakitoa shukrani zao viongozi wa vikundi hivyo wameushukuru uongozi wa Wilaya na Halmashauri kiujumla kwa kuwathamini na kuwatazama kwa jicho la tatu hivyo wanatarajia utaleta tija kwenye shughuli zao na wilaya kiujumla kwani watazalisha na kulipa mapato/kodi/ushuru stahiki.